NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameilalamikia
Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili iliyoongozwa na James
Lembeli kuwa taarifa iliyowasilisha bungeni na kuwang’oa mawaziri wanne
ilikuwa ya uongo.
Nyalandu alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na viongozi wa taaluma
mbalimbali pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma na
Manyara juu ya mgogoro wa mipaka kati ya hifadhi ya taifa ya Tarangire,
Pori la Akiba Nkungunero na vijiji vya jirani uliofanyika katika Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Alieleza kutokana na taarifa hiyo Tanzania kwa sasa imeonekana
kushuka kwa kiwango kikubwa katika utawala bora ikiwa ni pamoja na
ukiukwaji wa haki za binadamu.
Alisema kuna taarifa ambazo zilionyesha kuwa wapo watu ambao walibakwa jambo ambalo halikuwa la kweli.
Hata hivyo, alisema kwa sasa Rais Jakaya Kikwete amekubali kuunda
tume ya kimahakama ambayo itafanya uchunguzi juu ya kuwepo kwa matukio
hayo na itakapabainisha kuwa kuna watu walipotosha ni wazi watachukuliwa
hatua kali za kisheria bila kujali cheo cha mtu ambaye alihusika na
uongo au ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua nyingine, Nyalandu ametangaza kumsimamisha kazi ofisa
wanyamapori mwandamizi katika pori la akiba la Maswa, Lawrence Kileo,
kwa kutuhumiwa kupokea rushwa na kuwatoza faini wafugaji bila kuzingatia
taratibu.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu atangaze kusimamishwa kazi kwa watumishi 22 wa wizara hiyo.
Ofisa huyo anatuhumiwa kuwatoza faini wafugaji wanaoingiza mifugo yao
katika pori hilo bila kutoa risiti za serikali, na hivyo fedha hizo
kujinufaisha mwenyewe kinyume cha kifungu cha sheria namba 116[2]C cha
sheria ya kuhifadhi wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.
Nyalandu ametangaza kuanza kwa uchunguzi kwa Ofisa Wanyamapori wa
Wilaya ya Kasulu, Benjamini Mkosamali, kabla ya kuchukuliwa hatua za
kinidhamu kwa kuwaruhusu watuhumiwa wa ujangili kuondoka na nyara za
serikali walizokamatwa nazo kabla ya kukamatwa tena kwa msaada wa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Nyalandu
alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua zaidi kwa maofisa
wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vyovyote vile vya kukiuka
maadili ya kazi yao.
Watuhumiwa hao wa ujangili mkoani Kigoma ambao walikamatwa wakiwa
wamebeba wanyama aina ya tohe 12, madume watano na majike saba wakiwa
pia na insha wanne aina ya Oribi ambao hawakupaswa kuwinda kwa mujibu wa
leseni yao ya uwindaji namba B59921 iliyotolewa Kigoma.
Alisema awali watuhumiwa hao walikamtwa na kikosi cha doria cha
Kampuni ya Friedkin Conservation Fund na kumuita ofisa huyo kwa ajili
ya kuchukua hatua zaidi ambapo alipofika na kuzungumza na watuhumiwa
aliwaruhusu kuondoka na wanyama hao.
Nyalandu alisema Benjamini akiwa na taaluma ya kusimamia wanyamapori
huku akifahamu majangili waliokamatwa wamekutwa na nyara za serikali na
wamekutwa katika kitalu cha uwindaji sehemu ya Kibenge, baada ya kupata
taarifa kwa wahusika, aliamua kwa makusudi kuwaruhusu majangili hao
kuondoka.
“Hivyo nimeagiza mamlaka husika kukamilisha uchunguzi na kumchukulia
hatua za kinidhamu na za kisheria haraka sana ofisa huyo,” alisema
Nyalandu.
Alisema kuwa vita dhidi ya ujangili itaendelea kwa kasi na hata rais
ameishaahidi kuwa operesheni ujangili awamu ya pili itarejea hivi
karibuni baada ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika awamu
iliyomalizika.
Alifafanua kuwa kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita baada ya
kusitishwa kwa operesheni hiyo, tembo 60 waliuawa na majangili hao
kitendo ambacho hakitakiwi kuvumiliwa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment