|
HATIMAYE
mkali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nassib Abdul ‘Diamond Platinum’
ametimiza ahadi ya kuwasomesha watoto ambao walishinda shindano la
kucheza mtindo wake wa ‘Ngololo’ katika sherehe alizoziandaa maalumu
kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, Desemba 25, mwaka jana.
Diamond aliandaa shoo hiyo ili kuwakutanisha watoto kwa pamoja na
kuwashindanisha kucheza wimbo wake wa ‘My Number One’ ambao unafanya
vizuri katika ‘game’ na kuwaahidi kuwasomesha watoto zaidi ya watano
ambao walicheza vizuri wimbo huo.
Diamond kupitia mtandao wake wa ‘This is Diamond’, ameweka picha
ambazo zinaonyesha yupo shuleni akiwa na watoto pamoja na wazazi wao
wakiwaandikisha katika Shule ya East Africa International iliyopo
Mikocheni jijini Dar es Salaam.
“Nilipanga kuwapeleka shule watoto waliocheza vizuri na nilitaka
wapate elimu iliyo bora zaidi, nilikaa na uongozi wangu na kutafiti ni
shule gani ambayo itakidhi mahitaji ya watoto wale, yenye mazingira
mazuri ya kujisomea na kucheza, namshukuru sana Mkuu wa Shule hiyo, Bi.
Mercy Githirua, kwa kutupokea vizuri,” aliandika msanii huyo.
Diamond ni kati ya wasanii wanaofanya vizuri katika tasnia ya muziki
wa kizazi kipya, kutokana na ubora wa kazi zake ambazo zinakubalika
katika jamii inayomzunguka.
0 comments:
Post a Comment