Mtwara. Simanzi na huzuni vimetawaka katika
Shule ya Sekondari ya Mustapha Sabodo baada ya kutokea vifo vya
wanafunzi watano vilivyosababishwa na ajali ya gari juzi.
Wanafunzi watano wa shule hiyo, walifariki kwa
ajali ya gari huku 46 wakijeruhiwa na kati ya hayo, wanafunzi 20
waliumia vibaya na kuhitaji huduma za upasuaji. Waliofariki ni Khairath
Mohammed, Mwanahamisi Mohammed, Hasma Mpunja, Hilda Mathias na Farida
Ally ambao wote walizikwa jana.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Shaibu Maarifa
alisema jana kuwa hadi kufikia jana jioni, hakukuwa na ongezeko la vifo
na kuwa majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya
Rufani ya Ligula na Hospitali ya Misheni ya Nyangao.
Alisema kuwa majeruhi waliokuwa wamebaki
hospitalini hapo ni 20 na kwamba watatu wamehamishiwa katika Hospitali
ya Mission ya Nyangao ili kuokoa muda wa kusubiria foleni kwa ajili ya
upasuaji na wengine watano tunatarajiwa kuruhusiwa na wengine watabaki
kwa uangalizi.
“ Majeruhi wetu wanaendelea vizuri, tuliendelea
kuwahudumia kwa kushirikiana na wenzetu wa Hospitali ya Nyangao...,”
alisema Dk Maarifa.
Dk Maarifa aliongeza kuwa kutokana na ajali hiyo
zilihitajika damu salama chupa 25 na kwamba ziliweza kupatikana kwa
haraka kutoka katika Kituo cha Damu Salama cha Kanda ya Kusini ambacho
makao yake ni hospitalini hapo.
Rose Godwin (14) mmoja wa majeruhi aliyevunjika
mkono wa kushoto, akielezea mkasa huo, anasema: “Tulikuwa kwenye
mchakamchaka na wakati tunasubiri kuchukuliwa namba ili turudi shuleni
wakati huo tukiwa tumejipanga mstari jirani na shule ndipo nikaona gari
lililokuwa linatoka Mkoa wa Lindi na lingine Mtwara sikumbuki ilikuwaje,
wakagongwa na mimi nikajikuta naanguka na kuvunjika mkono.”
Eva Issaya, alisema: “Chanzo cha ajali ni magari
mawili kushindwa kupishana kutokana na barabara kuwa nyembamba na katika
kupishana na sisi tukiwa pembeni ya barabara gari moja likawagonga
baadhi ya wanafunzi waliokuwa njiani na sisi likatuangusha.”
Nao wakazi wa Kijiji cha Msijute jirani na
ilipotokea ajali hiyo, waliiomba Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na
Wakala wa Barabara, Tanroads kuangalia namna ya kupunguza ajali kwa
kuweka matuta eneo hilo.
“Tumepoteza vijana wetu wadogo ambao ndiyo taifa
tegemezi ambao ndiyo walikuwa wanaandaa maisha yao ila cha msingi
tunaiomba Serikali na hawa Tanroads watuwekee matuta na tahadhari kwani
eneo hili kwa sasa lina mwingiliano mkubwa wa watu na magari hasa tangu
ilipoanzwa ujenzi wa kiwanda hiki cha saruji cha Dangote,” alisema Juma
Namkopi.
Akizungumza Ofisa Uhamasishaji kutoka Mfuko wa Damu Salama wa Kanda ya Kusini,
Anania Lwoga alisema kuwa watu wanatakiwa kujitokeza kushiriki uchangiaji damu salama kwani huhitajika muda wote.
Akizungumza jana, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mustapha Ulaya
alisema kuwa ni majonzi na simanzi shuleni kwake na kwa sasa wamesitisha
masomo kuomboleza msiba huo mkubwa kuikumba shule hiyo.
“Tumesitisha kufundisha kwa muda, kila mmoja
anatafakari hali ilivyokuwa katika ile ajali. Ni watoto wengi kuumia na
kufa, imetushtua hali hii,” alisema Mwalimu Ulaya.
Hata hivyo alisema kuwa ana matumaini ya vijana wake kupata nafuu mapema na kurudi shuleni kuendelea na masomo.
Alisema pia kuwa hawataacha mchakamchaka kwa kuwa
ni utaratibu wa shule hiyo tangu ilipoanzishwa kwani ni sehemu ya
kuwatayarisha wanafunzi kwa siku.
0 comments:
Post a Comment