LATEST POSTS

Friday, January 24, 2014

Mwinjilisti aua mkewe, ajinyonga

MWINJILISTI wa Kanisa la Anglikana, Elikia Daniel (35), mkazi wa Kijiji cha Gama, wilayani Bagamoyo, Pwani, amemuua mkewe, Mboni Patrick (28) kwa kumkata na panga kichwani na kisha kumfukia kwa magogo na yeye kujinyonga.

Tukio hilo lilitokea Januari 20, saa 10 jioni wakati Mboni na mumewe walipokuwa eneo wanalokatia magogo kwa ajili ya mkaa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kabla ya mwinjilisti huyo kufanya mauaji aliongozana na Sabina Gabriel (10) mtoto wa mkewe pamoja na mkewe kuelekea kwenye tanuri la mkaa.
Kamanda Matei alisema walipofika Daniel alimtuma mtoto huyo kurudi nyumbani kwa ajili ya kuandaa chakula, mbinu ambayo ilimsaidia kutekeleza mauaji ya mkewe na baadaye yeye mwenyewe kujinyonga.
Inaelezwa mtoto huyo alipokamilisha kuandaa chakula alirejea na kukuta damu nyingi zikiwa zimemwagika chini katika eneo hilo huku mkono wa mama yake ukiwa umejitokeza katikati ya magogo kwenye tanuri.
Baada ya kuona hali hiyo mtoto huyo alirudi kijijini na kutoa taarifa kwa wananchi ambao waliongozana naye hadi eneo la tukio na kisha kutoa taarifa polisi ndipo walipotoa mwili wa mama huyo ukiwa umelowa damu.
Mita 300 kwenye eneo la tukio ulipatikana mwili wa mwinjilisti huyo akiwa tayari amepoteza maisha kwa kujinyonga.
Miili ya marehemu hao imefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi, na uchunguzi wa awali unabainisha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi.

chanzo: Tanzania Daima

0 comments: