LATEST POSTS

Tuesday, January 28, 2014

Operesheni Tokomeza yaburuta 516 kortini

OPERESHENI Tokomeza iliyoendeshwa na Serikali kusaka watu waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya ujangili imeweza kufikisha mashauri 516 yaliyofunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othuman Chande, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na maadhimisho ya Siku ya Sheria Duniani ambayo yatafanyika Februari 3, mwaka huu.
Alisema mashauri 516 yalifunguliwa katika mahakama mbalimbali kutokana na Operesheni Tokomeza ujangili iliyoanza Oktoba 4, mwaka jana hadi ilipositishwa Novemba Mosi, mwaka jana.
Alisema kuwa Mahakama ilipokea kesi 516 zilizohusika na Oparesheni Tokomeza ujangili ambapo mpaka sasa kesi 198 zimeshasikilizwa na kumalizika wakati wa operesheni.
Alisema kuwa katika kesi hizo mashauri yaliyofunguliwa chini ya sheria mbalimbali, sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 iliyorejeshwa mwaka 2002, sheria ya hifadhi ya wanyamapori sura ya 283, sheria ya mbuga za Taifa sura 282, sheria ya silaha na risasi sura 223, sheria ya misitu sura ya 323 na sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 na sheria ya kifo sura ya 24.
Hata hivyo alisema Mahakama za Hakimu Mkazi sita na Mahakama za Wilaya 19, zilihusika na kesi hizo ambapo kesi zilizosikilizwa na kumalizika wakati wa operesheni ni 198 sawa na asilimia 38.37.
Alisema vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuchoma Mahakama za mwanzo zimesababisha watu wengi kukosa haki yao ya msingi kutokana na majalada ya kesi kuungua.
Alisema kuwa kuanzia mwaka 2012 yamekuwapo matukio mbalimbali ya uchomaji moto majengo ya Mahakama za Mwanzo nchini na matukio hayo ni yale yaliyotokea Mahakama ya Mwanzo Mtwara Mjini, Mikindani, Lisekese na Mahakama ya Mwanzo Wanging'ombe katika mkoa wa Iringa.
"Januari 25, mwaka 2013 Mahakama ya Mwanzo Mtwara mjini ilichomwa moto na wananchi katika vurugu zilizotokea siku hiyo mjini Mtwara wakati wa mzozo wa rasilimali gesi na kusababisha jengo na majalada yote kuteketea kwa moto," alisema.
Alisema kutokana na matukio ya kuchomwa moto kwa mahakama za mwanzo kumesababisha wananchi wengi kukosa haki zao za msingi kutokana na kupotea kwa vielelezo muhimu pamoja na ushahidi.
Aliongeza kuharibiwa kwa majalada ya kesi kumesababisha kesi nyingi kusimama au kutoendelea kabisa katika baadhi ya mahakama na kuchangia wananchi kukosa haki.
Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 mahakama ya Tanzania imepanga kujenga majengo mapya 25 kwa ajili ya mahakama za mwanzo na kukarabati majengo mengine 10.
Hata hivyo, alisema kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi si kizuri kwani hawawezi kujenga mahakama eneo ambalo ilikuwepo lakini ikaunguzwa na wananchi wenye hasira. Pia alisema kuwa takwimu za mahitaji ya majengo ya mahakama za mwanzo nchini ni zaidi ya majengo 296 mapya na mengi mengine yanahitaji ukarabati.

Chanzo: Majira
 

0 comments: