Rais Jakaya Kikwete amempandisha cheo Mkuu wa Wilaya ya Karatu,
Daudi Ntibenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kuwahamisha vituo vya kazi
wakuu wengine sita wa mikoa kuanzia jana.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue ilisema Ntibenda ataapishwa leo, saa nne asubuhi,
Ikulu, Dar es Salaam.
Wakuu wa mikoa waliohamishwa ni Elaston Mbwilo
anayetoka Manyara kwenda Simiyu kuchukua nafasi ya Paschal Mabiti
aliyepewa likizo ya ugonjwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera anahamia
Manyara kutoka Morogoro na nafasi yake inachukuliwa Dk Rajabu Rutengwe
kutoka Tanga alikokaa kwa mwezi mmoja akitokea Katavi.
Magalula Magalula amehamishiwa Tanga kutoka Lindi
ambako naye alikaa kwa mwezi mmoja akitokea Geita na nafasi yake
inazibwa na Mwantumu Mahiza kutoka Pwani.
Mhandisi Evarist Ndiliko amehamishiwa Pwani kutoka Arusha alikohamia hivi karibuni kutoka Mwanza.
Katika taarifa yake, Balozi Sefue alisema wakuu wengine wa mikoa wanaendelea kubakia katika vituo vyao vya sasa vya kazi.
Uhamisho huo umekuja ikiwa ni mwezi mmoja kamili
tangu Rais Kikwete alipofanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa mikoa na
kuwahamisha sita huku wengine watatu wakipangiwa kazi nyingine.
Wakuu wa mikoa wanne wapya ni Dk Ibrahim Msengi
(Katavi), Amina Masenza (Iringa), Halima Dendego (Mtwara) na John
Mongella (Kagera).
Kabla ya kuteuliwa, Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya
ya Ilemela, Mwanza; Dk Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi,
Kilimanjaro na Mongela alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Walioachwa kwa ajili ya kazi nyingine ni Dk
Christine Ishengoma (Iringa), Kanali Fabian Massawe (Kagera) na Kanali
Joseph Simbakalia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ambaye tayari
ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya
Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Source: Mwananchi.
Source: Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment