LATEST POSTS

Friday, December 5, 2014

Fahamu jinsi Ukimwi ulivyoanza hata kusambaa kila kona duniani

Wakati ugonjwa wa ukimwi ukipamba moto katika mataifa mengi ya Afrika, miaka ya 1980, ilizuka hofu kubwa na maswali mengi juu ya lilikoanzia.
Kwa mfano, hapa Tanzania ulipewa majina mengi, kama vile Juliana, silimu (wembamba), fire (moto) na mdudu. Ni ugonjwa ambao walioupata walionekana kukonda hadi kubakia mifupa na nywele kunyonyoka.
Mbali na hali hiyo, mgonjwa alipata matatizo ya ngozi kuharibika kwa kuwa kavu, vidonda ambavyo viliacha madoa meusi na kuharisha.
Sura za wagonjwa zilikuwa zinabadilika na kuonekana za kutisha na walionekana kuwa katika hali ya mateso mengi ya kukumbwa na maradhi mengi kabla ya kufa.
Inafahamika wazi kuwa binadamu lazima utafika wakati atakufa, lakini kwenye miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa 1990, ulionekana kuambkizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) ni sawa na kupewa tiketi ya kifo. Wengine walidiriki hata kujiua mara baada ya kubaini wameambukizwa.
VVU inaweza kuchukua miaka mitano hadi zaidi ya 10 ili kuonyesha dalili za kuugua, hatua ambayo inafahamika kuwa ni ya ukimwi.
Wengi wa waliopimwa na kuonekana wameambukizwa wakati huo walifika hatua ya kukonda na kuugua mapema kutokana na wasiwasi na msongo wa mawazo juu ya kifo.
Zipo dhana nyingi katika jamii zinazohusu jinsi Viruzi Vya Ukimwi (VVU) vilivyoanza kuenea kwa binadamu, hususani kwa Waafrika ambao ndio wanaonekana kuathirika zaidi na janga hili.
Zilikuwapo dhana nyingi sana na zote zimefanyiwa kazi na wataalamu wa afya. Baada ya uchunguzi wa kina dhana nne ndizo zilizofanyiwa utafiti wa kina baada kuonekana kuwa mojawapo inaweza ikawa ni chanzo.
Dhana zilizofanyiwa kazi ni nne nazo ni za madai ya hujuma zilizofanywa na wataalamu ili kuwaua Waafrika, ukatili wa kikoloni, matumizi ya chanjo na shughuli za uwindaji.
Hujuma dhidi ya Waafrika
Hii ilitokana na hisia za Waafrika wenyewe hasa ikizingatiwa kuwa wao ndio waliokuwa wanaathirika zaidi.
Hapa ikaonekana kuwa huenda wazungu ndio wamefanya njama ili kuwaangamiza Waafrika kama siyo kuwapunguza.
Uvumi huo ulienea na uchunguzi uliofanywa ulibaini kuwa watu weusi wanaoishi Marekani, wengi wao waliamini VVU ni silaha iliyotengenezwa maabara ili kuwamaliza nchini humo.
Nchini Marekani wengi wa waliokufa ni watu weusi hasa waliokuwa wanajihusisha na ushogo na hata wanaoshirikiana nao.
Baada ya utafiti wa kina ulionekana kuwa huo ni uvumi tu kwa kuwa haukuwepo uthibitisho wa kisayansi kuthibitisha jambo hilo.
Vilevile ilibainika kuwa historia ya ukimwi ulianza kuenea kwa binadamu miaka ya 1920. Wakati huo taaluma ya sayansi ya afya ilikuwa haina ufundi wa uhandisi jeni ambao unawezesha kutengeneza virusi.
Kwa sababu hiyo, dhana hiyo ikaonekana haina mashiko na kuwekwa kando.
Ukatili wa wakoloni
Wapo waliodhani VVU ilianza kuenea kwa Waafrika wakati wa ukoloni, ambapo vilikuwapo vitendo vya kikatili vya kulazimisha watu wafanye kazi hadi kuwasababishia kuumia huku wakiishi mazingira magumu yasiyo safi wala chakula cha kutosha.
Iliaminika kuwa katika mazingira hayo mfumo wao wa kinga ulishuka na kuwa rahisi kuambukizwa maradhi mengi yakiwamo ya bakteria na virusi.
Isitoshe walipougua walidungwa sindano za tiba, huku zikiwa hazijachemshwa hivyo kuwa rahisi kuhamisha maradhi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Isitoshe, iliaminika kwamba baadhi ya kambi walisambazwa wanawake malaya ili kuwaliwaza wanaume baada ya kazi ngumu.
Kwa sababu hiyo, mazingira haya yote yalikuwa ya hatari na ambayo yangeweza kueneza virusi haraka kwa watu.

Hata hivyo vigezo hivyo vyote havikuzingatiwa kwa sababu hayakuwepo mazingira ya chanzo cha kirusi. Isitoshe baada ya taaluma kubaini VVU anatokana na kirusi aliyeanzia kwa sokwe hayakuwapo mazingira ya mahusiano na wanyama hao.
Utoaji wa chanjo
Baadhi ya wataalamu wa afya walifikiri kuwa VVU ilianza kuenea kwa binadamu kutokana na utoaji wa chanjo ya polio. Chanjo iliyopewa nafasi kubwa ya kueneza VVU ni ile iliyotengenezwa kwa figo za sokwe na ilitolewa kwa mtu aimeze.
Chanjo ya namna hiyo ilitolewa kwa mamilioni ya watu Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Rwanda na Burundi mwanzoni mwa miaka ya 1950.
Kwa sababu hiyo ikadhaniwa kuwa zilichukuliwa figo za sokwe na katika utengenezaji wa chanjo, vikawapo pia virusi.
Dhana hiyo ilionekana kuwa siyo chanzo kwa sababu VVU ilianza kuenea hata kabla ya miaka ya 1950. Jambo jingine ni kwamba kwa namna chanjo hiyo ilivyokuwa inatengenezwa isingeweza ikabeba VVU. Kwa sababu hiyo dhana hiyo ikatupwa.
Dhana ya uwindaji
Ilionekana kuwa uwindaji na utumiaji wa nyama ya sokwe umekuwa ukifanyika kwa miaka katika misitu ya eneo la Afrika ya Kati, hususani nchini DRC.
Wawindaji wakati wa pilika za kumuua sokwe waliweza kupata majeraha mbalimbali yakiwepo ya kujikata, kujikwaa na kuchubuka ngozi.
Wakati wa kuchuna ngozi ama kukatakata nyama, ilikuwa rahisi damu ya sokwe kufikia vidonda na hapo virusi kufanikiwa kuhamia kwa binadamu.
Dhana hii ilikubalika kutokana na desturi za wawindaji na kwamba ulikuwapo hata kabla ya miaka ya 1920, ambayo inaaminika kuwa watu wa kwanza kufa kwa dalili za ukimwi walionekana ingawa wakati huo ugonjwa ulikuwa haufahamiki.
VVU ilianzaje?
Wataalamu wa afya wamefanya tafiti mbalimbali na kujiridhisha kuwa VVU vinatokana na mfumo wa mabadiliko ya kijeni wa kirusi aliyekuwa anaenea miongoni mwa sokwe.
Kirusi huyu anajulikana kama Simian Immunodeficiency Virus (SIV). Ni kirusi ambaye kama ilivyo VVU naye anadhoofisha mfumo wa kinga ya sokwe. SIV anaaminika kuwa sawa na VVU, lakini yeye ana uwezo wa kushambulia tu mfumo wa kijinga ya sokwe.
Wataalamu wanaeleza kuwa VVU ni SIV ambaye amejibadili mfumo ili aweze kuendelea na uzalishaji kwa kupitia mfumo wa kinga wa binadamu.
Inaaminika VVU ilianza kusambaa kwa binadamu mwaka 1920 katika mji mkuu wa DRC, Kinishasa. Hata baada ya SIV kujibadili na kuwa VVU anayeweza kuenea kwa binadamu amekuwa akijibadili hivyo kusababisha aina kadhaa za virusi.
Hii imesababisha viwepo aina mbili za virusi, VVU1 na VVU2. VVU1 inatabia zinazofanana na za SIV zaidi kuliko VVU2. VVU1 inapatikana zaidi nchini DRC.
Wiki ijayo makala hii itaendelea kwa kukueleza jinsi VVU ilivyoenea kwa kasi pamoja na madhila yake.

Source: Mwananchi

0 comments: