Kampuni za Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) na
Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), zimewasilisha maombi ya kutaka
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) akamatwe kwa kukiuka amri ya
Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) kwa kufuta Hati za Malipo ya Kodi za Mauzo
ya Hisa (Capital Gain Certificate).
Kampuni hizo mbili, ambazo ziko kwenye mgogoro wa
umiliki, ndizo zinahusika kwenye sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni
kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kuhifadhi fedha za malipo
ya tozo ya kuuza umeme unaofuliwa na IPTL, kwa Shirika la Umeme
(Tanesco), wakati wa kusubiri uamuzi wa mahakama katika kesi ya kupinga
tozo hilo.
PAP, ambayo inadai imenunua hisa zote za IPTL,
ndiyo iliyolipwa fedha zote zilizokuwa kwenye akaunti hiyo na kuamsha
mjadala mkubwa bungeni ulioisha kwa Bunge kufikia uamuzi wa
kuwawajibisha kisheria wote waliohusika, wakiwemo mawaziri.
Lakini uamuzi huo wa Bunge haukuwa tamati la
sakata hilo baada ya kampuni hizo mbili kukata rufaa TRAB dhidi ya
Kamishna wa TRA na Msajili wa Kampuni na Leseni (Brela) zikipinga
kusudio la kufuta hati hizo.
Jana kampuni hizo mbili ziliwasilisha maombi ya
hati ya kutaka Kamishna Mkuu wa TRA akamatwe, zikidai kuwa amepuuza amri
hiyo iliyomzuia kutekeleza azma yake ya kufuta Hati za Malipo ya Kodi
ya Mauzo ya Hisa.
Katika maombi hayo walalamikaji hao wanadai kuwa
licha ya TRAB kutoa zuio hilo Novemba 26, 2014, Kamishna Mkuu wa TRA,
ambaye ni mlalamikiwa wa kwanza, alitoa amri ya kuziondoa hati hizo siku
iliyofuata, yaani Novemba 27, 2014, bila kujali amri hiyo.
Walalamikaji hao pia wanaiomba TRAB, baada ya
kumkamata Kamishna Mkuu wa TRA, itoe amri afungwe kwa kudharau amri
halali iliyotolewa na bodi na pia imwamuru akidhi matakwa ya amri ya
TRAB ya Novemba 26.
Pia walalamikaji hao wanaiomba TRAB imwamuru
mlalamikiwa huyo, kulipa gharama za uendeshaji wa shauri hilo pamoja na
amri nyingine ambazo itaona kuwa zinafaa.
Maombi hayo ya PAP na IPTL ya hati ya kumkamata na
kuamuru Kamishna Mkuu wa TRA afungwe yamepangwa kusikilizwa leo na
Katibu wa TRAB, Respicius Mwijage.
Hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo inaeleza
kuwa mlalamikiwa, akiwa ni raia wa Tanzania, siyo tu kwamba alipaswa
kuwa mtiifu kwa mamlaka ya bodi hiyo, bali pia alipaswa kutekeleza
sheria za nchi ambazo bodi hiyo ni sehemu yake.
Hati hiyo ya kiapo ya mkurugenzi wa operesheni wa
IPTL, Parthiban Chandrasakaran, inaeleza kuwa kwa kitendo hicho cha
kutotii amri ya bodi hiyo, mlalamikiwa amepoteza sifa ya kuwa mtumishi
wa umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia inaelea kuwa kama bodi hiyo isipotumia mamlaka
yake kukubali maombi hayo ya kutoa amri inayoombwa, basi walalamikaji
watapata hasara isiyoweza kufidiwa.
0 comments:
Post a Comment