UMOJA wa Vijana wa
Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umemrushia kombora aliyekuwa Waziri Mkuu,
Edward Lowassa, kuwa hana sifa za kuwa rais wa Tanzania, hivyo aache
kukigawa chama hicho.
Kauli hiyo ya UVCCM imetolewa jijini Dar es
Salaam jana na Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi, Paul Makonda, wakati
alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kauli ambazo zimekuwa
zikitolewa na makada wa chama hicho kuhusiana na sakata la mawaziri
mizigo.
Alidai kwa sasa umoja huo hauna muda wa kupoteza wa
'kupambana' na watu wanaotoa kauli za kubeza na kumkatisha tamaa Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape
Mnauye, kuhusiana na kazi walizofanya za kukijenga chama.
"Tunafahamu
kuwa Guninita (John) na Mgeja (Khamis) hawana uwezo wa kumsema Kinana
wala Nape, kilichopo nyuma yao na kinachowapa nguvu ya kufanya hivyo ni
mtu anayewatuma na kuwafanya wao kumsaidia kutafuta madaraka...naye si
mwingine ni Edward Ngoyayi Lowassa," alisema Makonda na kuongeza kuwa;
"Kama
Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Marehemu Julius Nyerere) angekuwepo,
Lowassa asingepata nafasi ya kuyumbisha chama kiasi hicho...tunamweleza
kuwa UVCCM haiko tayari kumuona anakibomoa chama kwa kupenda madaraka."
Aliongeza
kwamba aendelee kuwasaidia viongozi wa dini na vijana wenye shida ya
fedha, lakini sifa ya kuwa rais na amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi
na usalama hana. "Chama hakiwezi kukosea njia na kumpa urais mtu ambaye
hana sifa," alisema Makonda.
Alisisitiza kuwa Chama ni sikio la
wananchi na kiungo cha kuwaunganisha Serikali na wananchi wake, hivyo
viongozi wa CCM wamefanya ziara na kubaini kero za wananchi.
"Inapofika
hatua wasimamizi wa kanuni za chama wanapigwa vita kwa uamuzi wao wa
kukisimamia chama UVCCM haiwezi kukaa kimya kwani wanaofanya hivyo
hawakitakii mema chama chetu," alisema.
Alisema wanashangazwa na
wanaomtuhumu Kinana na Nape kwa lengo la kuwachonganisha na Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ili jamii ione kuna tofauti ndani ya
sekretarieti, kwani lengo la kufanya hivyo ni kuwavunja moyo watendaji
hao katika juhudi ambazo zinafanywa kwa kutupa mawe hata kwenye vyombo
vya habari.
"Juhudi za kukiimarisha chama kutoka ngazi za chini kwa
mabalozi ni mkakati bora kwani kukirudisha chama kwa wanachama ni
kutimiza lengo la kuundwa kwa chama hicho cha wanyonge na maskini wa
Taifa hili na haiwezekani matajiri watake kukihodhi na waratibu mikakati
ya kukihujumu kwa pesa zao hali sisi vijana tukiwatazama tunasema
tutakilinda chama chetu na kuwalinda viongozi wetu waadilifu."
Aliwataka
wanachama kuelewa kuwa viongozi hao wanaobezwa ndio wameweza kurudisha
imani na matumaini ya wananchi kwa chama ambayo tayari ilishaanza
kupotea na kuonekana si chama cha wanyonge, wakulima na wafanyakazi.
"Ni
Comrade Kinana na timu yake ndio waliozunguka kwenda kukutana na
wakulima wa pamba kule mikoa ya Kanda ya Ziwa kumpeleka Balozi wa China
na kumshawishi kujenga viwanda ili kuboresha manufaa kwa wakulima".
Aidha
alifafanua kuwa viongozi hao hao ndio wamepelekea kukutana na wakulima
wa korosho na kushirikiana nao pamoja na bodi kutatua matatizo
yanayowakabili na kuibua kero nyingine ikiwemo za wafugaji, walimu na
wananchi kwa ujumla.
Alisema umoja huo tayari umewasilisha barua
yake kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, Philip Mangula kumtaka
kuchukua hatua kwani mtu anayebeza ziara hizo na kuwaita viongozi
waliozifanya waropokaji na wahuni ni mtu mjinga wa ovyo, hana maadili,
asiyekipenda chama, mhaini na mzandiki anayepaswa kuchukuliwa hatua kali
za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.
Mgeja ambaye ni
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alipoulizwa kuhusiana na madai ya
Makonda, alijibu kuwa hajapata taarifa hiyo. "Tunasubiri taarifa hiyo
ili tujue tunavuruga chama kwa namna gani na sijui kama Lowassa anatumia
fedha, anatumia fedha ili iweje?" Alihoji Mgeja.
Lakini baadaye
Mgeja , aliwasiliana na gazeti hili na kusema kuwa yeye ni mtu mzima,
hatishiwi nyau. Alisema Makonda anatafuta umaarufu kupitia migongo ya
wakubwa.
"Kamwe mimi si saizi yake kwani ninaelewa kijana huyo
anatumika kuwafurahisha wakubwa zake waliomtuma," alisema na kuongeza;
"Hakuna asiyejua kuwa kijana huyo ana hasira za kuangushwa nafasi ya
umakamu Mwenyekiti wa UVCCM na sasa anataka kulipa fadhila kwa
waliotafuta njia kumpa nafasi katika umoja huo, hivyo ajiandae kula
sahani moja na wazee wa chama hicho.
Mgeja alisema hatumwi na hatumiki kwa Lowassa, bali kijana huyo na wanaomtuma wanahangaika na kivuli cha Lowassa.
“Niliwaeleza
na nawasisitiza tusichaguliane marafiki na wala wasichanganyikiwe,
naelewa wana kiwewe kila siku Lowassa, Lowassa... kiwewe cha nini kwanza
huyo Makonda bado mchanga sana kujibishana naye ni kuvunja heshima zetu
ila kwakuwa damu inamchemka anatamani kula sahani moja na wakubwa
sawa,” alisema.
Alisisitiza kuwa hakuna dhambi kumuunga mkono
Lowassa na kama ni dhambi yeye yupo tayari kuhukumiwa kwa kuwa
anakubaliana na utendaji wake hasa katika kumtakia heri kwa kazi
anazozifanya katika kuwatumikia wananchi.
Alimtaka Makonda kufanya
kazi za kujenga chama na umoja huo kwa kuzungumzia changamoto zilizopo
ikiwemo tatizo la ajira na umaskini.
0 comments:
Post a Comment