LATEST POSTS

Friday, April 4, 2014

Mgomvi wa mke wa Zuma atishia kujiua

Akiwa amekaa mahabusu kwa zaidi ya miezi miwili, Mtanzania Steven Ongolo, anayeshikiliwa kwa kutishia kutoa siri za Nompumulelo Zuma (ManTuli), ambaye ni mke wa rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ametishia kujiua akidai anatishiwa kuuawa na haki kutotendeka katika kesi yake.
Ongolo alikamatwa na polisi jijini Durban Januari mwaka huu baada ya kudai kuwa ana siri nzito zinazomuhusu mke wa Rais Zuma, huku akitishia kuanika siri hizo.
Mapema wiki hii, Ongolo, ambaye anashikiliwa katika mahabusu ya Pietemaritzburg, aliomba kuonana na waandishi wa habari na kuwaambia kuwa atajiua wakati wowote kwa sababu ananyanyasika katika mahabusu hiyo.
“Nataka kumaliza kila kitu hapa kwa sababu najua sitapata haki katika kesi hii. Nimeandika barua na kueleza kila kitu,” alisema Ongolo. Kwa Afrika Kusini, mahabusu anaweza kupata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari kueleza malalamiko yake.
Pia Ongolo ambaye amenyimwa dhamana kwa mara ya pili, alieleza anapata shida zaidi kutoka kwa mahabusu wenzake ambao wanamtukana na kumsimanga, wakidai eti anamsababishia matatizo rais wao.
“Watu humu ndani wananiuliza kwa nini nasababisha matatizo kwa familia ya rais. Nahofia maisha yangu, chochote kinaweza kunipata,” alisema.
Hata hivyo, Ongolo licha ya kuahidi kuwakabidhi waandishi wa habari nakala ya barua yake ya kutaka kujiua, baadaye alisema barua hiyo imechukuliwa.
Pamoja na malalamiko mengine, Ongolo alisema anahisi kuna mchezo mchafu unaofanyika kwani hata wakili wake, Lekoko Lekoa ameacha kufika mahabusu kumsalimia ili kutimiza mipango waliyopanga.
“Nitajitetea peke yangu mahakamani. Katika nchi za watu najua haki haiwezi kutendeka,” alisema.
Ongolo alikamatwa Januari 24 mwaka huu baada ya kufanya mahojiano na gazeti la Sunday Tribune. la nchini humo na kueleza kuwa ana siri nzito zinazomuhusu mke wa Rais Zuma.
Mtanzania huyo alisema, ManNtuli anajua kwa undani sababu ya kifo cha mlinzi wake, Phinda Thomo, ambaye aliripotiwa kujipiga risasi bafuni kwake, Soweto mwaka 2009.
Ongolo alituma ujumbe wa baruapepe kwenye magazeti ya Afrika Kusini akidai kuwa Thomo hakujiua, bali aliuawa kutokana na siri za mahusiano kati yake na MaNtuli kuvuja.
Vilevile Februari mwaka huu Mkuu wa Uchunguzi wa Kesi, katika Jimbo la Kwa Zulu-Natal, Brigedia Clifford Marion alisema Ongolo anaweza kurudishwa Tanzania na azuiwe kuingia Afrika Kusini milele.

Chanzo: Mwananchi

0 comments: