Kwa muda mrefu sasa, Bunge la Afrika Mashariki limekuwa katika
mizozo isiyoisha kiasi cha wananchi wengi katika nchi wanachama kuhofia
kwamba Bunge hilo linaweza kusambaratika. Tulishuhudia miezi michache
iliyopita mzozo mkubwa ukiibuka, ambapo wabunge kutoka katika baadhi ya
nchi wanachama walisusia vikao wakipinga vikao hivyo kufanyika katika
makao makuu ya jumuiya hiyo pekee yaliyopo jijini Arusha, Tanzania.
Hata hivyo kwa busara za wakuu wa nchi wanachama
na uongozi wa Bunge hilo wakati huo, mzozo huo ulimalizika kwa kuboresha
kanuni husika na kuweka utaratibu wa kuwezesha vikao hivyo kufanyika
kwa mzunguko katika kila nchi mwanachama. Pamoja na kumalizika kwa
mgogoro huo pasipo madhara makubwa kisiasa na kiuchumi, sasa umejitokeza
mgogoro ambao wananchi wengi wa nchi wanachama wanahofu kwamba
utalisambaratisha Bunge hilo.
Wengi wa wabunge wamesema hawana imani na Spika,
Dk Margareth Zziwa na wanataka ang’oke kwa madai kwamba ameshindwa
kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Tofauti na
ilivyokuwa katika migogoro iliyotangulia, mgogoro huu hauna dalili au
hisia zozote za utaifa. Wabunge wanaompinga Spika na kutaka aondolewe
siyo tu ni zaidi ya theluthi mbili ya wabunge kama Kanuni
zinavyoelekeza, bali pia wanatoka katika nchi zote wanachama, ikiwamo
nchi yake ya Uganda. Pia hoja ya kumng’oa madarakani haina harufu yoyote
ya ubaguzi wa kijinsia kwa sababu wabunge wengi wanawake ndio wako
mstari wa mbele kutaka kiongozi huyo aachie madaraka.
Inasemekana kwamba Serikali ya Uganda nayo
imeridhia Spika huyo ang’olewe kutokana na sababu mbili kubwa. Kwanza,
ni madai kwamba Spika huyo hakuwa chaguo la chama tawala cha NRM ingawa
ni mwanachama wake. Pili, ni ukweli kwamba sasa ni zamu ya Uganda kutoa
Spika, hivyo hata kama Spika Margareth Zziwa aking’olewa
atakayechaguliwa lazima atokane na wabunge kutoka katika nchi hiyo.
Pamoja na hali hiyo, mzozo huo unakuzwa na utata unaotokana na Kanuni ya
9 ya Bunge hilo inayoeleza utaratibu wa kumwondoa Spika madarakani
iwapo itatokea haja ya kufanya hivyo.
Kwa vyovyote vile, hali hiyo haiashirii vyema hali
ya baadaye ya Bunge hilo, hasa kutokana na ukweli kwamba Spika huyo
sasa ameahirisha Bunge kwa muda usiojulikana kutokana na mvutano kati ya
wabunge wanaomuunga mkono na wale wanaotaka aachie madaraka. Mpaka
anachukua hatua hiyo, wabunge 33 kati ya 45 walikuwa wametia saini tamko
la kutaka ang’oke, lakini akatumia Kanuni ya 82(2) kuahirisha Bunge,
ambalo lilipangwa kumaliza shughuli zake hapo kesho.
Wapinzani wa Spika Zziwa wanamtuhumu kwa mambo
mengi, yakiwamo madai ya: Kuendesha Bunge kwa ubabe; kuwagawa wabunge;
kiburi; kuchukulia mambo kirahisi; na kuchelewa mara kwa mara katika
vikao vya Bunge. Tuhuma nyingine ni: Kuonyesha dharau kwa wabunge; na
Matumizi mabaya ya fedha. Hoja ya kumng’oa Spika Zziwa ilianza
kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari vya Afrika Mashariki kwa wiki
kadhaa sasa kabla ya Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya kuiwasilisha
bungeni.
Sisi tunasema mzozo huo unahitaji kutatuliwa kwa
busara, vinginevyo Bunge litasambaratika na kuirudisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki katika zama za kiza. Maoni yetu ni kwamba Spika ataonyesha
ustaarabu kwa kuheshimu uamuzi wa wabunge walio wengi ambao wanataka
aachie madaraka.
0 comments:
Post a Comment