Tumeisoma kwa umakini mkubwa taarifa iliyotolewa juzi na Ikulu,
ikikanusha madai ya mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba kwamba Ikulu imeitupia virago Tume hiyo. Tumejaribu
kuisoma taarifa hiyo ya Ikulu tena na tena, aya kwa aya, mstari kwa
mstari na neno kwa neno. Lakini kadiri tulivyozidi kufanya hivyo ndivyo
tulivyozidi kugundua kuwa ni dhahiri Tume hiyo, siyo tu ilitupiwa
virago, bali pia ilidhalilishwa na kufadhaishwa kutokana na lugha ya
kejeli na masimango iliyokuwa katika taarifa hiyo ya Ikulu.
Jaji Warioba alikaririwa akilalamikia jinsi yeye
na makamishna wa Tume walivyoondolewa ofisini na kunyang’anywa magari
kwa namna ambayo iliwadhalilisha, kwani licha ya hatua hiyo kuchukuliwa
kwa haraka bila kusubiri siku ambayo Tume ilikuwa imepanga kufanya
makabidhiano, Serikali haikutaka kujipa muda wa kufanya maandalizi ya
kuwarudisha wajumbe makwao.
Katika kuhalalisha hatua hiyo ya Serikali, taarifa
ya Ikulu ilijikita zaidi katika kifungu cha 31(1) cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba kinachoelekeza kwamba shughuli za Tume zingekoma
rasmi baada ya mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge
la Katiba. Ikulu ilisema katika taarifa hiyo kwamba Jaji Warioba
aliwasilisha Rasimu hiyo bungeni Machi 18 na siku iliyofuata Rais alitia
saini tangazo la kuvunja Tume hiyo kwa mujibu wa sheria, hivyo
ilishangazwa na kitendo cha mtu “kujitia amesahau siku hiyo kwani hicho
ni kiwango cha juu sana cha unafiki”.
Hata hivyo, jambo linalomtatiza Jaji Warioba na
wenzake ni uharaka wa Serikali kuivunja Tume hiyo wakati ikijua kwamba
Tume ilikuwa haijamaliza kazi yake wakati ilipokabidhi Rasimu hiyo kwa
Rais. Jaji Warioba anasema Serikali ilikuwa ikijua kwamba Tume ilikuwa
ikiendelea na kazi ya kuandaa Randama ya Rasimu, Bango Kitita la Rasimu
pamoja na maelezo aliyoyatoa wakati wa kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge
la Katiba.
Lakini pia Jaji Warioba anasema kuwa hata kama
sheria ilitaja muda wa kuvunja Tume hiyo, bado Serikali ilikuwa na
wajibu wa kuhakikisha inavunjwa katika mazingira yanayokubalika kama
zilivyovunjwa tume zote zilizotangulia, kwani sheria hiyo haikuzuia
kufanya hivyo.
Sisi tunadhani kuwa kwa kuzingatia utamaduni
uliozoeleka, Tume ingevunjwa rasmi katika mazingira ya kistaarabu na
heshima kama tulivyoshuhudia ikizinduliwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete
katika viwanja vya Ikulu, Aprili 13, 2012.
Tunashindwa kuelewa kiini cha udhalilishaji huo
mkubwa kwa Tume hiyo, pamoja na Rais Kikwete kuimiminia sifa na pongezi
nyingi kwa kuweka utaifa mbele. Akipokea Rasimu hiyo Desemba 31, 2013
katika viwanja vya Ikulu, Rais Kikwete alisema Tume hiyo imefanya kazi
iliyotukuka na ya kihistoria na kuwataka wajumbe wa Bunge Maalumu waige
mfano wake pindi Bunge hilo litakapoanza kazi ya kujadili Rasimu na
hatimaye kuandika Katiba mpya. Sasa nini kimetokea kiasi cha Tume hiyo
kuonekana kama imefanya uhaini ni kitendawili ambacho hakijateguliwa.
Sisi tunadhani kwamba haikuwa sahihi kwa Serikali
kuwadhalilisha Jaji Warioba na makamishna wa Tume hiyo, hata kama
pengine haikufurahishwa na baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba waliyoiwasilisha.
Kwa kuzingatia kwamba Tume hiyo iliundwa na watu
ambao uzalendo wao hauwezi kutiliwa chembe ya shaka, Serikali ilipaswa
kuienzi kazi waliyofanya hata kama kwa shingo upande.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment