Mbeya.Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alipata wakati mgumu juzi jioni baada ya
kuzomewa na wananchi waliokerwa na kitendo chake cha kubadilika na
kumruhusu mwekezaji kuendelea kumiliki eneo la ardhi katika Shamba la
Kapunga, Wilaya ya Mbarali, Mbeya.
Ilibidi Mkuu wa Wilaya hiyo, Gulam Hussein Kifu
aingilie kati kuwatuliza wananchi hao waliokuwa wakipiga kelele na kutoa
maneno makali kwa waziri huyo.
Profesa Tibaijuka alikwenda huko kwa nia ya
kusuluhisha mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya wananchi wa Kapunga
na mwekezaji wa Kampuni ya Kapunga Rice Project. Awali, shamba hilo
lilikuwa mali ya Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco).
Wananchi hao walikasirishwa na hatua yake ya
kuamua kuwa eneo hilo ni halali kwa mwekezaji huyo tofauti na msimamo
wake wa awali wa kutaka ardhi hiyo irudishwe kwa wananchi.
Profesa Tibaijuka alibadili mawazo yake baada ya kufanya mazungumzo na mwekezaji huyo ndani ya gari akiwa na Mkuu wa Wilaya.
Msimamo awali
Profesa Tibaijuka alifika Kijiji cha Kapunga saa
6.45 mchana na kuanza kikao cha ndani na viongozi wa kijiji kwenye ofisi
yao hadi saa 8.14 mchana. Alielezwa alielezwa kwamba mgogoro huo
unatokana na kitendo vya mwekezaji huyo kutaka kupora ardhi yote ya
kijiji chenye wakazi wapatao 4,400.
Mwenyekiti wa Kijiji, John Nyoni alisema mwaka
1995, wanakijiji walitoa hekta 5,500 za ardhi kwa Nafco ambazo ziko
kwenye mradi maalumu wa kuendelea kilimo cha mpunga, lakini
wanachoshangaa ni kuona aliyerithi eneo hilo (mwekezaji) anadai hekta
nyingine 1,870 kutoka kwenye mashamba ya wananchi pamoja na kijiji
chote.
Nyoni alidai kuwa katika harakati hizo, mwekezaji
huyo alipokonya shule, zahanati ya kijiji na sasa anataka kuwaondoa
wananchi wote. Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Tibaijuka alisema
alifika hapo kutoa jawabu la suluhisho na kwamba atakachotoa ni cha
mwisho wala hakutakuwa na mgogoro mwingine tena.
“Serikali imetambua chanzo cha makosa ni Nafco
kusajili na kupata hati moja kwa eneo lote likiwamo la kijiji pamoja,
hivyo mwekezaji huyo alikabidhiwa hati hiyo ikionyesha eneo la hekta
7,370 badala ya hekta 5,500,’’ alisema Profesa Tibaijuka.
Aliwahakikishia viongozi wa kijiji hicho chenye
vitongoji saba kwamba alifika hapo ili kumtaka mwekezaji akabidhi hati
hiyo serikalini ili ofisi yake ikaibadilishe na kwamba kama atakataa
atamwandikia Rais Jakaya Kikwete kumtaka aifute hati yote.
Baada ya kikao hicho, Waziri akiwa na msafara wake pamoja na
baadhi ya viongozi wa kijiji walikwenda kwenye eneo la mwekezaji na
kumkuta Mkurugenzi Mtendaji, Justin Vermaak ambaye alisema anawashangaa
wananchi wanaokaa eneo hilo ambalo ni lake kisheria.
Vermaak alisema hati aliyonayo inaonyesha kuwa
eneo lote ni lake, lakini wananchi wanakataa na matokeo yake
wanasababisha vurugu.
Akizungumza baada ya kupata taarifa hiyo, Profesa
alimweleza mwekezaji huyo kwamba kimsingi wananchi wa Kapunga waliipatia
Nafco hekta 5,500 ambazo ndizo anazotakiwa kumiliki mwekezaji. Alisema
Nafco walifanya makosa katika usajili wa hati kwa kuchanganya eneo la
mashamba ya wananchi na eneo la kijiji chote.
“Hivyo tunakuomba usalimishe hati hiyo ili
tukaiandike upya kwa kuzingatia eneo la hekta 5,500 na eneo jingine la
hekta 1,870 kuwaachia wananchi,’’ alisema.
Mwekezaji huyo alikubaliana na uamuzi huo wa
Waziri lakini akazua dai jipya la fidia... “Fidia ya nini? Kwanza
miundombinu yote uliikuta na nadhani watu wa kukulipa ni wale
waliokuuzia,” Profesa Tibaijuka alimjibu.
Kuona hivyo, mwekezaji huyo akaibua hoja nyingine
mpya ya kutaka ardhi nyingine lakini Profesa Tibaijuka alipinga hoja
hiyo na kumsisitizia kuwa awasilishe hati.
Baada ya kuona Profesa Tibaijuka anazidi kuwa
mkali, mwekezaji huyo akamwomba waziri: “Basi tutaongea kwenye gari.
Tupande pamoja wakati wa kuzunguka kwenye mashamba yangu.”
Waziri huyo naye alikubali kupanda gari hilo na
walianza safari ya kulitembelea shamba hilo huku akiwa amepanda gari la
mwekezaji huyo.
Katika gari hilo, mwekezaji alikuwa akiendesha
wakati waziri akiwa mbele na nyuma yake alikaa Mkuu wa Wilaya, Kiffu na
msaidizi wa mwekezaji aliyetajwa kwa jina moja la Jacob.
Abadili msimamo
Baada ya safari hiyo, waandishi walimwomba waziri
atoe kauli ya Serikali kuhusu mgogoro huo ndipo aliposema kwamba baada
ya kuzunguka ameona mwekezaji hana matatizo na amegundua kuwa chanzo cha
mgogoro ni Serikali.
“Hivyo, Serikali itaendelea kuzungumza na
mwekezaji na wananchi ili kumaliza mgogoro. Mwekezaji ni mzuri lakini
wapo wananchi wakorofi ambao wanadiriki hata kwenda kuzuia maji yasije
kwa mwekezaji na wanakijiji pia wana makosa,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alipoulizwa imekuwaje amebadili msimamo wake wa awali wa kumtaka
mwekezaji asalimishe hati, Profesa Tibaijuka alicheka kisha kueleza
kuwa amemwelewa mwekezaji. Alipoulizwa ikiwa mwekezaji huyo atakabidhi
hati kama alivyomwagiza, Tibaijuka alijibu; “Aaaah, hilo siyo la msingi.
La muhimu ni kwamba mambo yanakwenda vizuri na majibu kamili yatatolewa
hivi karibuni.”
Kuzomewa
Profesa Tibaijuka na msafara walianza mkutano wa
hadhara na wanakijiji saa 11.45 jioni na kuwahutubia wananchi kwa
kuwaeleza mwekezaji hakuwa na makosa, bali Nafco ndiyo wa kulaumiwa.
Kauli hiyo ilifuatiwa na zomea zomea huku baadhi ya wananchi wakisema: “Ondoka, umekuja kutembea huku, hujaja kutusaidia.”
Wananchi walikuwa wakisema hayo kwa sauti kubwa
wengine wamshutumu mwekezaji huyo kuwa hana ushirikiano. Wamedai pia
kwamba ujio wake umesababisha mateso kwa kuwa baadhi ya nyumba zao
zimechomwa moto na wengine mazao yao kunyunyuziwa sumu katika kipindi
hiki cha mgogoro. Wakati wengine wakilalamika na kusema kila mmoja lake,
wapo waliokuwa wakinyoosha mikono wakitaka kupewa nafasi kutoa
madukuduku yao mbele ya waziri huyo.
Hali hiyo kukosekana uelewano baina ya waziri na wananchi hao ilimfanya Mkuu wa Wilaya kuingilia kati na kuwaomba wananchi hao watulie
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment