Mhe. John Mnyika
SIKU
moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kukubali pingamizi la
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuizuia Kamati Kuu (CC) ya
CHADEMA isimjadili hadi kesi yake ya msingi itakapokuwa imesikilizwa,
chama hicho kimemfungia rasmi kushirikiana na wabunge wenzake katika
shughuli za kisiasa.
Sambamba na hilo, chama hicho kimesema kuwa kuanzia sasa kinasahau
mjadala kuhusu Mbunge huyo wa Kigoma na badala yake kinajikita kuchapa
kazi kwa ajili ya malengo waliyojiwekea mwaka huu 2014.
Shughuli ambazo Zitto amefungiwa nazo ni pamoja na zile za nje na
ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, hususani zinazohusu kambi rasmi
ya upinzani bungeni, inayoongozwa na CHADEMA.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano Habari
na Uenezi, CHADEMA, John Mnyika, alisema uamuzi wa mahakama haujaelekeza
kwamba Zitto apewe ushirikiano na chama chake, hivyo uamuzi wa CC wa
kutoshirikiana naye uko pale pale.
Katika uamuzi wa CC uliosomwa na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa,
pamoja na kutangaza uamuzi wa kuwavua uanachama Samson Mwigamba na Dk.
Kitila Mkumbo, alisema: “Kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishitaki chama
kinyume na matakwa ya katiba ya chama na kanuni zake, na kwa vile
Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya chama visijadili wala kuamua suala
lolote linalohusu uanachama wa Zitto, viongozi wa ngazi zote za chama
wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo katika nchi
yetu na nje ya Tanzania, wasishiriki wala kusaidia kwa namna yoyote
mikutano yoyote ya nje au ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa
itakayofanywa na Zitto na mawakala wake kwa jina la CHADEMA.”
Mnyika alisema Kamati Kuu ilishapitisha azimio la kumtenga Zitto na
shughuli za siasa na kuwataka wanachama wao kote nchini, wasitoe
ushirikiano kwa kazi au shughuli yoyote itakayofanywa na mbunge huyo.
“Uamuzi huo upo pale pale, na mahakama haijaelekeza kwamba apewe
ushirikiano,” alisema Mnyika wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia
ya simu.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, aliwataka wafuasi wa CHADEMA
kutambua kuwa kilichoamriwa na mahakama ni pingamizi la awali tu kwani
kesi ya msingi bado haijaanza kusikilizwa.
“Unajua kilichoamriwa ni pingamizi la awali. Huko ni sawa na
kushangilia bao wakati mpira ndio kwanza umeanza na unaendelea. Mfano
mzuri ni kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Simba na Yanga. Yanga walishangilia
mabao matatu ya kipindi cha kwanza wakijua wameshinda, walipoingia
kipindi cha pili unajua kilichotokea… Kwa hiyo kesi ya msingi bado, na
hatuoni sababu ya kushangilia kwa sasa,” alisema.
Mnyika aliwataka wanachama wao kutambua kuwa CHADEMA iko imara na
inaendelea na kazi zake kama kawaida, huku ikiwa na ajenda muhimu na
mikakati mizito kwa ajili ya mwaka 2014.
Alizitaja baadhi ya ajenda ambazo wananchi wataanza kuzifanyia kazi
kuwa ni pamoja na suala la katiba ambapo chama hicho kimepitisha
maazimio sita mazito ya kuyafanyia kazi kuelekea mchakato wa katiba mpya
na maandalizi ya mpango kazi wa mwaka 2014.
“Kamati Kuu iliyopita, mbali ya kushughulikia suala la wanachama wetu
wasaliti, pia ilikuwa na mambo mengi ya kujadili. Kuna maazimio sita ya
mchakato wa katiba mpya ambayo tutawaeleza, kuna suala la kupanda kwa
bei ya umeme na maazimio yake. Watanzania wasubiri waone CHADEMA
imeazimia nini katika suala la kupanda kwa gharama za umeme ambapo
wameanza kuumizwa na ongezeko hilo,” alisema Mnyika.
Kwa msimamo huo wa kumfungia rasmi Zitto kushiriki shughuli za chama,
ni wazi kuwa unazidi kumuweka njia panda Zitto ambaye sasa atabaki
kuwa mwanachama kwa nguvu ya mahakama hadi hapo itakapoamriwa
vinginevyo.
Sasa Zitto ataungana na wabunge wenzake wawili, David Kafulila wa
Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) na Hamad Rashid Mohammed wa Wawi (CUF)
ambao pia ubunge wao upo kwa nguvu ya mahakama.
Zitto alifungua kesi Mahakama Kuu siku moja kabla ya CC kuanza vikao
vyake ambavyo vilikuwa vijadili utetezi wa tuhuma zake za kuendesha
mkakati wa siri wa kusaliti chama, akiomba mahakama izuie suala la
uanachama wake lisijadiliwe hadi kesi yake isikilizwe.
Akitoa uamuzi wa awali, Jaji John Utamwa, alisema kuwa mahakama
imeridhia ombi la Zitto kuwa CHADEMA au chombo chochote kisijadili
uanachama wake hadi kesi ya msingi itakapomalizika.
Katika kesi ya msingi, Zitto anaiomba mahakama ikizuie chama hicho
kumchukulia hatua, ambapo kesi hiyo inatarajiwa kutajwa Februari 13,
mwaka huu.
Zitto aliwasilisha maombi dhidi ya Baraza la Wadhamini la CHADEMA
pamoja na Katibu Mkuu wa chama, Dk. Slaa, akiiomba mahakama itoe zuio la
muda kwa Kamati Kuu kutojadili uanachama wake.
Katika kesi hiyo, Zitto ameiomba mahakama iizuie Kamati Kuu kujadili
uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa na Baraza Kuu la chama
na kuomba mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe nakala za taarifa za vikao
vilivyomvua uongozi ili akate rufaa.
Katika hatua nyingine, Janeth Josiah anaripoti kuwa
CHADEMA imemtaka Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova, kuacha propaganda za kisiasa na badala yake
awakamate na kuwachukulia hatua za kisheria, waliohusika kumteka,
kumtesa na kumuumiza mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Temeke,
Josephat Yona.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CHADEMA, Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Henry Kilewo, alisema kama Kamanda Kova
amechoka kuwa mtumishi ndani ya jeshi hilo na kufanya siasa, atoke
hadharani na kujitangaza.
“Tunamtaka Kamanda Kova atoke hadharani atangaze kuwa anatumikia
chama gani cha siasa ili tukutane kwenye majukwaa ya siasa na siyo
kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama,” alisema Kilewo.
Alisema polisi inapaswa kuyachukulia kwa uzito mkubwa na unaostahili
matukio ya namna hii ambayo yanaanza kuota mzizi kwenye jamii.
Kilewo alisema mwaka 2012/2013 yalitokea matukio yenye sura ya aina
hiyo ya kutekwa na kuteswa kwa watu mbalimbali, wakiwamo wanaharakati,
wanahabari na wanasiasa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa.
Alitoa mfano kuwa Jeshi la Polisi walimkamata kijana Evodius
Justinian na wenzake, waliwatesa vikali na kuwarubuni katika jitihada
za kuwashinikiza wakiri kuwa viongozi wa CHADEMA ndio waliowatuma
kutekeleza matukio ya uhalifu.
Alisema bado Watanzania wanataka kujua taarifa na hatua zilizochuliwa
kisheria katika matukio ya kutekwa na kuteswa kwa Dk. Steven Ulimboka
na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.
Hata hivyo, alisema CHADEMA ipo mstari wa mbele kutetea haki za
binadamu, kupinga ukatili, uhuni na vitendo kama hivyo na hakiwezi
kumtuma mtu yeyote kufanya utekaji, utesaji au udhalilishaji.
Kwa mujibu wa Kova, uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa tukio la
kutekwa kwa kiongozi huyo wa CHADEMA, lina uhusiano na ugomvi
unaoendelea ndani ya chama hicho, hivyo ameunda tume ya wataalamu
kuchunguza.
Yona alikutwa usiku wa juzi akiwa katika hali mbaya ya kujeruhiwa huko Ununio wilayani Kinondoni.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment