MIEZI minne tangu gazeti hili lifichue taarifa za Kampuni ya 
ukandarasi ya Visual Storm Co. Ltd kuwa imesajiliwa Bodi ya Wakandarasi 
(CRB) kwa kutumia nyaraka za kughushi, hatimaye kampuni hiyo imefutwa 
rasmi.
Msajili wa CRB, Boniface Muhegi, amethibitisha kufutwa kwa kampuni 
hiyo inayomilikiwa na Noel Severe (31), mtoto wa mkurugenzi wa zamani wa
 Wanyamapori, Emmanuel Severe.
Noel pia ni mkwe wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, akiwa amemuoa bintiye aitwaye Dk. Adda Lowassa.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano, Muhegi alisema kuwa baada ya 
kujiridhisha wameifuta kampuni na kwamba ikibainika kuendelea kufanya 
kazi mahali popote nchini, taarifa zifikishwe CRB ili hatua zichukuliwe.
Kwa mujibu wa tangazo la CRB kwa umma, Visual Storm ni ya 52 katika 
orodha ya makampuni 379 yaliyofutwa tangu Januari Mosi mwaka huu kwa 
mujibu wa kifungu cha 13 (1) (b) (c) na (d) na 15 (1) (c) cha sheria 
namba 17 ya 1997 kama ilivyorekebishwa kwa sheria namba 15 ya 2008.
CRB ni chombo cha serikali kilichoanzishwa kwa sheria ya Bunge Na. 17
 ya mwaka 1997 ili kusajili wakandarasi wote na kusimamia kazi zao kwa 
lengo la kuwalinda watumiaji wa huduma za wakandarasi nchini.
Awali gazeti hili katika uchunguzi wake lilijiridhisha pasipo shaka 
kwamba CRB imeisajili Visual Storm Co. Ltd kwa kutumia nyaraka za 
kughushi, na hivyo ikaendelea kutekeleza miradi yake ya ujenzi.
Katika kile kilichoonyesha kuwepo kwa nguvu ya viongozi nyuma ya 
pazia, Visual Storm ilipewa mkataba wa ukarabati wa tawi la Benki ya 
Biashara ya Dar es Salaam (DCB) mwaka 2011 ikiwa bado haijasajiliwa na 
CRB kwa mujibu wa sheria.
Visual Storm ilisajiliwa kwa Msajili wa Makampuni (Brella) mwaka 2009
 kwa No. 71362 na kisha CRB Februari 23, 2013 kwa No. B5/0674/2/12 
daraja la tano.
Kampuni hiyo kabla ya usajili CRB, iliingia mkataba na DCB Oktoba 3, 
2011 wa kujenga ukumbi wa mikutano katika tawi la Ukonga kwa gharama ya 
sh 56,676,580 kwa muda wa wiki tano.
Hadi kufikia Januari 9, 2013, kampuni hiyo ilikuwa imeshindwa 
kukamilisha kazi hiyo, hatua iliyomlazimu Mkurugenzi Mkuu wa DCB, Edmund
 Mkwawa, kuiandikia akiitaarifu kusudio la kutaka kuvunja mkataba huo.
Nakala ya barua hiyo pia ilipelekwa kwa msajili wa CRB, Boniface 
Muhegi, ambapo Februari 12, 2013, bodi hiyo kupitia kwa Kaimu Meneja wa 
Kanda ya Mashariki, D. J. Karugendo, ilijibu kwa kuiandikia Visual Storm
 na kuipa siku saba itoe maelezo ya kushindwa kutimiza mkataba huo.
Mkwawa alipotakiwa kufafanua ni kwanini benki yake iliingia mkataba 
na kampuni ambayo haikuwa imesajiliwa CRB, alisema kuwa suala hilo 
aulizwe Visual Storm.
“Tunawasubiri hao CRB tukutane mahakamani, lakini kwanini usiwaulize Visual Storm wakakupa majibu?” alisema.
Hadi tuhuma hizo zinafikishwa CRB mwaka jana, bodi hiyo ilidai 
kutokuwa na taarifa ya kasoro hiyo, japo kulikuwa na kumbukumbu za 
kuonyesha kuwa walipata barua ya malalamiko ya DCB.
Kwa hatua hiyo, msajili wa CRB, Muhengi alisema kampuni hiyo inapaswa
 kuadhibiwa kwa kutozwa faini pamoja na DCB kwa kutoa zabuni kwa kampuni
 ambayo haikuwa na usajili wa bodi yake.
Katika uchunguzi huo, ilibainika kuwa Visual ilikimbilia CRB 
kujisajili baada ya kushindwa kutimiza mkataba wa DCB kwa wakati, na 
hivyo kuhofia kukumbwa na rungu la adhabu baada ya benki hiyo kuanza 
kulalamika.
Hata hivyo, kampuni hiyo ilitumia nyaraka za kughushi hatua ambayo 
Muhegi alisema kuwa wamiliki wake watapaswa kuchukuliwa hatua za 
kisheria baada ya kufutiwa usajili.
Ili kampuni iweze kusajiliwa CRB, Muhegi anasema ni lazima itimize 
vigezo kadhaa kulingana na daraja husika ambapo wamiliki wanatakiwa kuwa
 na wataalamu, ofisi na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wa wataalamu, kampuni inapaswa kuwa na mkurugenzi wa 
ufundi ambaye amesajiliwa na Bodi ya Mainjinia (ERB) ambaye atakuwa 
ameajiriwa na kampuni husika na kuwa mmoja wa wanahisa.
Kampuni ya Visual Storm awali iliwasilisha vielelezo vya vyeti vya 
Loserian Sokonoi ambaye hata hivyo alitofautiana na Severe na kuamua 
kuondoka na kuajiriwa serikalini akiwa ni mhandisi wa wilaya mkoani 
Shinyanga.
Baadaye kampuni hiyo iliwasilisha CRB cheti cha Kent Kissima na 
kumtambulisha kama mkurugenzi wa ufundi ilhali ni mwajiriwa wa serikali 
akifanya kazi kama meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) makao makuu.
Katika majibu yao ya awali, CRB walisema mkurugenzi wa ufundi wa 
kampuni hiyo ni Sokonoi na baadaye wakasema ni Kissima ambaye kwa sasa 
amehamishwa makao makuu (Tanroads) na kupelekwa kuwa meneja wa Mkoa wa 
Simiyu.
“Tumekwenda huko TRA (Mamlaka ya Mapato) tumekuta kadi za vifaa 
walizowasilisha huko sio vya kwao, kinachofuata sasa ni kuifuta na 
kuanza utaratibu wa kuwasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na 
Rushwa (Takukuru) na vyombo vingine vya kisheria,” alisema.
Alipotafutwa Sokonoi kuthibitisha kama ndiye bado mkurugenzi wa 
ufundi wa kampuni hiyo, alijibu: “Huyo jamaa tulifanya naye kazi, lakini
 wakati tukiwa kwenye mchakato wa usajili alionekana kunizika fedha 
zangu nikajiondoa.
“Mimi kwa sasa niko Shinyanga nimeajiriwa serikalini na 
nilikwishawaandikia CRB kuwaarifu kuwa vyeti vyangu visitumike popote 
kwenye taasisi yao kwa namna yoyote, maana sifanyi kazi huko tena.”
Naye Kissima kwa maelezo yake mbele ya viongozi wa Tanroads na Wizara
 ya Ujenzi, alikana kuwapa Visual Storm vyeti vyake ili vitumike 
kumtambulisha kama mtaalamu wao wa ufundi.
Gazeti hili linayo nakala ya mkataba kati ya Visual Storm na Kampuni ya Fabec/Home base (T) Ltd.
Mkataba huo ulitumiwa na Visual kuwalaghai CRB wakati wa kukaguliwa 
vifaa vyao vya ujenzi, ili kuonyesha kwamba wameikodishia Fabec 
iliyokuwa na kazi ya ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Mpanda wakati huo.
Msemaji wa Fabec, aliyejitambulisha kwa jina moja la Ziota, 
alipotafutwa alilieleza gazeti hili kuwa kampuni yao haijawahi kuwa na 
mkataba wa aina hiyo na Visual.
“Kampuni hiyo wala sijawahi kuisikia, inamilikiwa na nani?” alihoji 
Ziota na kufafanua kuwa hata kama wangekuwa wamekodishwa vifaa hivyo, 
CRB walitakiwa kutembelea mradi wao kujiridhisha kama vipo kweli.
Baada ya kusajiliwa CRB, Kampuni ya Visual Storm imeendelea 
kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ile ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya 
Jamii (NSSF) bila kuisajili kwenye bodi kama sheria inavyosema wala 
kufuata taratibu za kupata vibali vya ujenzi.
Utetezi wa Severe 
Mkurugenzi Mkuu wa Visual Storm, Severe, alikiri na kuonyesha 
mshangao akihoji nani alivujisha suala hilo kwenye vyombo vya habari.
Alidai kuwa ameshangaa kuona nyaraka sahihi alizompatia mshirika wake
 kwa ajili ya kushugulikia usajili, zilibadilishwa na kupachikwa zile za
 kughushi.
“Kaka yaani nashangaa kwanini jambo hili linakuwa hivi, mimi hivi 
vifaa unavyonionyesha hapa kampuni yetu haina na sijui hawa walivitoa 
wapi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu utata wa mkurugenzi wao wa ufundi, Severe alimtaja
 Sokonoi kuwa ndiye waliyewasilisha jina lake CRB. Lakini alipobanwa 
aeleze inakuwaje mhusika anafanya kazi serikalini, alisema walikuwa 
kwenye mkakati wa kumbadilisha.
Alipoelezwa kuwa CRB wanamtambua Kissima kama mkugenzi wa ufundi wa 
kampuni hiyo, Severe alidai kutomtambua mtu huyo, huku akionyesha 
kushangaa alichomekwaje na kuwa mmoja wa wanahisa.
Severe katika kujitetea alimtwisha lawama mtu aliyemtaja kwa jina la 
Ruben, ambaye alidai kuwa alikuwa mshirika wake kwamba ndiye alivujisha 
siri hiyo kwa sababu wakati wa usajili CRB alihusishwa kwa ukaribu.
Tanzania Daima lilimtafuta Emmanuel Ruben, ambaye alikiri 
kushirikiana na Severe katika usajili wa kampuni hiyo CRB, lakini 
akasema kuwa baadaye walihitilafiana katika mgawanyo wa rasilimali na 
hivyo akajitoa na kuanzisha kampuni yake.
“Mimi pale CRB nina power of attorney (nguvu ya kisheria) kwa Kampuni
 ya Visual Storm kwa vile tulikuwa pamoja, lakini kwa sasa niko 
kivyangu, sasa hayo ya kwamba nimeleta siri hiyo kwenu ndiyo nasikia 
kwako,” alisema Ruben.
Uchunguzi wa habari hii umefadhiliwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).
Chanzo: Tanzania Daima 
 
 






 
 
0 comments:
Post a Comment