LATEST POSTS

Tuesday, February 11, 2014

Mkurugenzi Erolink atoroka nchini

 MKURUGENZI wa Kampuni ya uwakala wa ajira ya Erolink Tanzania Limited ametoroka nchini baada ya serikali kubaini kuwa  ameikosesha kodi ya zaidi ya sh bilioni tatu kwa miaka mitatu.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa  mkurugenzi huyo ajulikanaye kwa jina la Elvis Rogers Kamanyile, aliondoka nchini na familia yake  kuhofia  hatua za kisheria ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa kosa la kukwepa kodi.
Aidha, chanzo chetu kilidokeza kuwa  mkurugenzi huyo aliondoka nchini kwa madai ya kwenda kutibiwa ingawa madai hayo yanasemekana kutokuwa na ukweli ndani yake. Habari zilizopatikana zilidokeza kuwa  hivi sasa kampuni hiyo ya Erolink ipo katika mchakato wa kubadili jina  ili kuepuka kesi  ya madai ya kukwepa kodi inayokuja mbele yake, huku baadhi ya viongozi serikalini (majina yanahifadhiwa) wakiwa mstari wa mbele kufanikisha  zoezi hilo.
“Hivi sasa Erolink ipo katika mchakato wa  kubadili jina ili kupoteza ushahidi lakini pia kama hiyo haitoshi  zoezi hilo  linasimamiwa na baadhi ya viongozi wazito serikalini, kutokana na baba wa mkurugenzi huyo aliwahi  kuwa mkurugenzi wa moja ya benki kubwa hapa nchini ili kuhakikisha sakata hilo linazimika kwa sheria kutofuata mkondo wake,” kilisisitiza chanzo hicho.
Hofu ya mkurugenzi huyo inakuja baada ya agizo la Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alilolitoa wiki mbili zlizopita la kupiga marufuku utaratibu wa mawakala kuajiri wafanyakazi wanaowatafutia.
Badala yake aliwataka  mawakala husika wakiwamo Erolink kuwahamisha wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwao na mawakala wengine  kwenda  kampuni husika  moja kwa moja na kuwa waajiri halali katika kipindi cha mwezi mmoja.
Kwa mujibu wa Waziri Kabaka, kuhusiana na uchunguzi uliofanywa kwa kampuni 13  ulibaini kuwepo kwa ujanja  unaotumiwa  na mawakala wanane kutofuata na kuzingatia sheria na taratibu ambapo mwisho wake hukwepa kodi na kujipatia faida  kwa kutotoa  haki za msingi kwa wafanyakazi kama inavyofanywa na Erolink.
Mbali ya hayo, uchunguzi pia ulibaini  kutokuwapo kwa tahadhari kwa wafanyakazi  wanaoajiriwa  kwa utaratibu huo ikiwemo kukosa haki za kijamii kama likizo ya uzazi, matibabu na  sheria  za mifuko ya hifadhi ya jamii.
Waziri Kabaka alibainisha kuwa uwepo wa kampuni za mawakala wanaoajiri watu unaleta mfumo wa kibaguzi katika mishahara  kwa kazi za aina moja, kukosa fursa ya kujiendeleza  kielimu na mafunzo, kukosekana kwa uasalama  na uhakika wa ajira huku wafanyakazi wakilipwa mishahara ya kima cha chini  kinyume cha sekta  wanayofanya kazi.
Hata hivyo kampuni nyingi za uwakala hapa nchini ikiwamo Erolink zinakiuka  sheria  ya ajira na uhusiano kazini namba 6/2004 inayomtaka mwajiri kuchukua  hatua stahiki kwa kuhakikisha wafanyakazi bila kujali jinsia  zao wanalipwa mshahara  linganifu kwa kazi zenye uzito na thamani sawa.
Pamoja na katazo hilo Tanzania Daima limebaini kuwapo kwa wafanyakazi wa kigeni   wanaohusishwa katika utaratibu wa kukodishwa ambao Waziri Kabaka aliwataka kuhakikisha wanaomba vibali huku akisisitiza kwamba waajiriwe na kampuni zinazowakodisha. 
Chanzo:  Tanzania Daima

0 comments: