LATEST POSTS

Tuesday, February 11, 2014

Vigogo sita CCM waitwa Kamati ya Maadili


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza kwenye mkutano na  waandishi wa habari uliofanyika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, jana. Picha na Bashir Nkoromo 

Dar es Salaam. Vigogo sita ambao wanatajwa kuwa wanajiwinda kwa ajili ya kuwania urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao, wameitwa mbele ya Kamati ya Ndogo ya Maadili ya chama hicho, kwa ajili ya kuhojiwa kwa tuhuma za kukiuka maadili.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili jana zinawataja vigogo hao kuwa ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
“Wote wamepelekewa barua za wito wa kufika mbele ya Kamati ya Maadili inayoongozwa na Mzee Mangula (Philip, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara), ambayo itakutana mjini Dodoma, Februari 14 (kesho kutwa) ,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka Ofisi Ndogo ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam na kuongeza:
“Barua hizo zimesainiwa na Mzee Kinana (Abdulrahman, Katibu Mkuu wa CCM) mwenyewe na tayari zimeanza kusambazwa leo (jana) mchana.”
Kamati hiyo ndogo ya maadili, inaundwa na Mangula, Kinana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Maua Daftari na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye jana alithibitisha kuwapo kwa Kikao cha Kamati ya Maadili Februari 14 pamoja na kuitwa kwa baadhi ya wanachama kwa ajili ya kuhojiwa.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina yao wala idadi ya walioitwa... “Wewe fahamu tu kwamba kikao hicho kitafanyika tarehe hiyo uliyoitaja, lakini masuala ya majina na idadi ya walioitwa yatajulikana kwenye kikao, mimi sina kwa sasa,” alisema Nnauye.
Katika siku za karibuni kumekuwa na vita ya maneno baina ya makada wa chama hicho, wakituhumiana kutangaza mapema kugombea urais kabla ya ruhusa rasmi ya chama.
Kauli za walioitwa
Jana, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya walioitwa na wengi wao walisema hawakuwa wamepokea barua za wito huo.
Sumaye kwa upande wake alisema: “Kwa sasa niko Mwanza na sijapata barua yoyote ya kuitwa katika kikao chochote cha chama.”

Lowassa alipigiwa simu mara kadhaa na kusema kuwa yuko kwenye kikao apigiwe baadaye. Alipigiwa mara sita na kusema alikuwa bado kwenye kikao.
Membe kwa upande wake alisema: “Kwangu si mara ya kwanza kuitwa Kamati ya Maadili, ifahamike kwamba unaweza kuitwa kutoa ushahidi, maelezo au ufafanuzi wa jambo lolote unalokuwa umeitiwa.”
Wassira pia alisema hakuwa amepata barua hiyo ya wito... “Mimi ndiyo nimeshuka kutoka Bunda, sina hiyo barua ya kuitwa kwenye Kamati ya Maadili. Mwaliko nilionao ni wa kikao cha Kamati Kuu kesho (leo) ambao mimi ni mjumbe,” alisema Wassira.
Kwa upande wake, Makamba naye alisema alikuwa hajapata wito huo, wakati Ngeleja hakukanusha au kuthibitisha kupokea barua hiyo kwa maelezo kwamba yeye siyo msemaji wa CCM, hivyo asingeweza kuzungumzia suala la kuitwa kwake.
“Kwa kweli wewe fahamu tu kwamba mimi siyo msemaji wa chama. Chama chetu kina utaratibu wa wasemaji wake, waulize hao maana watakuwa na taarifa sahihi,” alisema Ngeleja.
Katika hatua nyingine, Nnauye alisema Kamati Kuu (CC) ya CCM, inakutana Dar es Salaam leo, huku Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ikitarajiwa kukutana Jumamosi na Jumapili wiki hii mjini Dodoma.
Vikao hivyo pamoja na mambo mengine vinatarajiwa kujadili ushiriki wa wajumbe wake katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo limepangwa kuanza Februari 18, mwaka huu mjini Dodoma.

0 comments: