UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora na
wananchi wa kata mbalimbali wilayani humo wamesisitiza kupinga mpango
wa wilaya hiyo kutaka kuhamishiwa Mkoa mpya wa Katavi
Wamesema mpango huo wa kutaka kuwahamishia wananchi wa wilaya hiyo
katika mkoa mwingine wa Katavi hauna tija katika suala zima la
mustakabali wa maendeleo yao na taifa kwa ujumla, hivyo hawapo tayari
kuhamia Katavi.
Wakizungumza hivi karibuni katika ziara ya kikazi ya Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Kaliua, Mhe. John Kadutu, wananchi wengi wakiwemo viongozi wa
chama tawala (CCM) walisema mpango huo utarudisha nyuma maendeleo ya
wananchi.
“Sisi hatutahama kutoka Tabora kwenda Katavi. Haiwezekani serikali
itutoe karibu na makao makuu ya Mkoa wetu wa Tabora halafu watupeleke
Katavi, umbali wa zaidi ya kilometa 70. Tunasema hatuondoki Tabora
ng’o,” alisema mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Musa Samuel,
kauli ambayo iliungwa mkono na wananchi wengi wa kata 16 kati ya kata
18 za wilaya hiyo.
Akisisitiza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kaliua, John Kadutu,
alisema halmashauri yake haipo tayari kuondoka Mkoa wa Tabora na
kuhamia Mkoa mpya wa Katavi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Ibrahim Kifoka,
ambaye pia ni Diwani wa Silambo, alieleza kusikitishwa na mpango huo
na kusema wananchi wake hawakubaliani na mpango huo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment