CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepasua ngome ya
mbunge wake, Zitto Kabwe na kuzidi kujiimarisha kisiasa katika jimbo la
Kigoma Kaskazini.
Timu ya viongozi wa CHADEMA wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama
hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed, Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema
na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano, John Mnyika iliwasili jana na
kuitikisa Kigoma kwa mikutano ya M4C Operesheni Pamoja Daima.
Hamasa ya wananchi wa Kigoma hususan katika Kata ya Mikongolo iliyoko
katika jimbo la Kigoma Kaskazini, ilijionyesha wazi baada ya timu hiyo
kupokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakiimba nyimbo za kukisifu
chama hicho huku wakilazimika kutembea umbali wa kilometa 3 kwenda eneo
la mkutano kutokea mahali ilipotua helkopta.
Kutokana na umati wa wananchi kuwa mkubwa, watumiaji wengine wa
barabara wakiwemo waliokuwa wakiendesha magari, walilazimika kusimama
pembeni mwa barabara kupisha msafara huo wa viongozi, huku nderemo,
vifijo pamoja na ishara za salamu za chama hicho, zikitawala.
Wakihutubia katika maeneo mbalimbali ya mkoani hapa wakianzia
wilayani Uvinza (Nguruka), Kigoma Kaskazini (Mikongolo na Kagunga) na
Kigoma mjini, viongozi hao wameendelea kuzungumzia ajenda za operesheni
hiyo ambayo ni pamoja na masuala ya mchakato wa katiba mpya, umuhimu wa
Watanzania kudai kuboreshwa kwa daftari la wapiga kura, matumizi ya
rasilimali za nchi kwa faida ya wananchi na hali ya ugumu wa maisha
ambayo wamekuwa wakiihusisha na uongozi mbovu unaosimamia sera
zilizoshindwa.
Akizungumza katika mikutano iliyofanyika jana katika maeneo
mbalimbali ya Kigoma wakianzia wilayani Uvinza (Nguruka), Kigoma
Kaskazini (Mikongolo na Kagunga) na Kigoma mjini, Makamu Mwenyekiti
Mohamed alisema kuwa lengo la operesheni hiyo ya CHADEMA awamu hii ni
kuwatembelea wananchi nchi nzima ili kujadiliana nao masuala hayo muhimu
kwa taifa.
Mbali ya kuwashukuru wananchi na hususan wanachama wa CHADEMA mkoani
Kigoma kwa kuendelea kusimama na kukipenda chama chao, Makamu Mwenyekiti
huyo alisema kuwa wameamua kuwa sauti ya Watanzania wanyonge katika
masuala yanayohusu mustakabali wao, hivyo hawataruhusu mtu yeyote, awe
mwanachama au kiongozi, kukiyumbisha chama kwa maslahi binafsi.
“Chama chenu kimetambua kuwepo kwa hila na njama za kutaka
kukisambaratisha. Kuna watu waliingia kwenye chama hiki kwa ajili ya
malengo ya kukisambaratisha, bahati nzuri kwetu na bahati mbaya kwao ni
kwamba mbinu hizo zimefeli kwa sababu zimebainika,” alisema Mohamed huku
akionekana kuungwa mkono na watu wa Mkongolo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu, Lema, aliwaasa Watanzania kuwa
ili nchi yao ikombolewe kuondokana na watu aliodai ni wakoloni weusi
wanaofanya kazi kwa mwavuli wa CCM, kunahitajika chama kimoja chenye
nguvu ambacho kitasimama imara kwa ushirikiano na wananchi wenyewe.
Lema pia alitumia fursa ya mikutano ya jana kukemea propaganda za
udini ambazo zimekuwa zikienezwa mkoani humo na nchi nzima kwa ujumla
zikitumiwa na baadhi ya wanasiasa wanaofilisika na kuishiwa hoja kama
ngao ya kujikinga kila wanapotuhumiwa usaliti na kukosa uadilifu katika
masuala ya uongozi.
“Ndugu zangu wana wa Kigoma naomba msishiriki katika dhambi ya udini
inayopandwa na baadhi ya watu wachache wasioitakia mema nchi yetu. Hii
dhambi haitatibika kamwe, kaeni mbali na uovu huu. Wanaoupanda wana
malengo yao…achaneni nao. Tujadilini mambo ya msingi yanayotukabili sote
kama Watanzania,” alisema Lema.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano, Mnyika, alisisitiza
kwamba chama hicho kitaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kinidhamu
kwa wanachama wake hususan kwa viongozi ambao watabainika kwenda kinyume
na taratibu za chama hicho.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment