LATEST POSTS

Saturday, January 25, 2014

Amng’ata meno mtoto baada ya kumfanyia ukatili mkewe

 
Picha ikimwonyesha mtoto Zakaria (1) na jeraha lake lililotokana na kung’atwa na baba yake. 
 
Serengeti. Wakati alipoolewa kuwa mke wa pili kwa mahari ya ng’ombe wanane, Katarina Mturi (22) alisindikizwa kwa ngoma na tamaduni za Kabila la Kikurya, wala hakuamini kama kuna siku ataichukia ndoa hiyo.
Inawezekana hakuamini hivyo kwa kuwa mume wake Matata Makali (siyo jina halisi), ambaye alionekana mwenye upendo na kujali, pengine ni kwa sababu ya mapenzi mapya ya binti mdogo.
Katarina alikuwa ameolewa mara ya pili akitoka kwa mume wake wa kwanza aliyedai hakuwa na hata chembe ya upendo ndipo kwa kushauriana, familia yake ilimrudishia mahari mwanaume huyo na ndoa kuvunjika.
Mwanamke huyo anasema kuwa alikaa nyumbani kwao kwa muda, ndipo akajitokeza Matata(45), akiamini kuwa sasa amepata mume mwema.
Hata hivyo, hali ilikuwa kinyume, kwani leo Katarina ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Chinato, kijijini Bisarara, Kata ya Sedeco katika Wilaya ya Serengeti iliyopo Mkoa wa Mara, amekuwa miongoni mwa wanawake wanaosimulia ukatili wa kijinsia katika ndoa. Kutokana na yaliyomkuta, anaona kuwa ndoa siyo tena hitaji lake muhimu maishani.
Kwa nini?
Pamoja na mateso, kipigo alichokuwa akipata, alijitahidi kuvumilia familia yake ikimtia moyo na kumweleza kuwa ndoa ndivyo zilivyo.
Lakini Katarina anasema hatosahau tukio la saa 2:30 usiku, Januari 8 mwaka huu, ambapo mumewe huyo mpya alimfanyia ukatili bila kuwa na chembe ya huruma.
Katarina anaeleza kwamba hofu yake sasa ni ukatili kumwachia ulemavu.
“Katika hali ambayo mpaka leo sijaielewa, nilikuwa ndani na wanangu wawili, mkubwa na huyu mdogo mume wangu aliingia ndani akaniamuru niswage ng’ombe usiku huo kwenda ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa malisho. Nilikakataa, kwa sababu ilikuwa ni usiku. Nilimweleza kuwa kisheria haikubaliki kuchungia mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa, tena  kuna wanyama wakali na mimi ni mwanamke nitafanyaje?,” anasimulia.
Katarina anaongeza akionyesha maeneo aliyoumizwa: “Maneno hayo yakamkasirisha na kilichotokea ndiyo kama unavyoona.”
Kilichomtokea
Anasema kuwa mume wake alichukua fimbo na kuanza kumpiga mithili ya mbwa mwizi, bila kuchagua sehemu ya kupiga na kumuumiza maeneo mbalimbali ya mwili ikiwamo mguu, ambao sasa uko hatarini kuoza.

“Akanipiga mpaka mwenyewe akachoka; sikuwa na uwezo wa kukimbia kwani damu zilinitoka mno na mtoto alikuwa akilia baada ya kuona ninavyopigwa. Lakini mwanaume huyo hakuwa hata na chembe ya huruma. Nikitafakari  kosa langu sijui, nadhani alikuwa amepanga kwa muda mrefu kutekeleza lengo hilo,”anaeleza.
Baba amalizia hasira kwa mtoto
Katarina anasimulia kuwa baada ya kipigo hicho alichopata yeye, Matata alimrukia mtoto wake na kumng’ata meno mgongoni, akidai alimpandisha hasira baada ya kulia alipomwona mama yake (yeye Katarina) anapigwa.
“Bila chembe ya huruma aliamua kumrukia mtoto wa mwaka mmoja na kumng’ata mgongoni mpaka akamtoa nyama.  Licha ya mtoto kulia kutokana na maumivu makali aliyopata, Matata hakujali, hata mimi kudhani kuwa mwisho wetu na mwanangu ndiyo umefika,”anasimulia Katarina.
Agoma kuwapeleka hospitali
Licha ya majeraha waliyopata usiku huo wa Januari 8, siku iliyofuata ya Januari 9 Matata aliamka na kuendelea na shughuli zake, bila kujali, wala kuwa na dalili za kuwapeleka hospitali mkewe na mwanawe ingawa aliona kuwa mkewe hakuweza kutembea kutokana na jeraha na maumivu aliyokuwa nayo.
Mama abeba jukumu
Meremo Mturi (43), mama mzazi wa Katarina anasema kuwa akiwa nyumbani kwake katika shughuli zake za kawaida, ghafla alimwona binti yake (Katarina) na mjukuu wake wakisindikwa hadi nyumbani kwake hapo.
“Nilipowaona nilistuka nikajua kuna jambo lisilo la kawaida wametendewa, ndipo Katarina akanisimulia nami nikashuhudia hali halisi, niliogopa sana,”anasema.
Hospitali
Mareno anasimulia kuwa kuona hali hiyo alilazimika kuwapeleka Hospitali Teule ya Nyerere baada ya kupitia polisi na kupata hati maalumu ya Pf 3.

Hata hivyo anasema kuwa kwa walikaa hospitali zaidi ya siku 7 wakitibiwa, lakini mume wa Katarina (Matata), hakuweza kujitokeza, wala kutoa fedha kwa ajili ya matibabu.
Wakosa fedha za matibabu
Walisitisha tiba za hospitali kutokana na kukosa fedha, ambapo sasa wanafikiria kugeukia tiba ya miti shamba kutokana na ukweli kwamba hali ya majeraha yao siyo nzuri na ikiwa hakutafanyika jitihada za ziada huenda mguu Katarina ukaoza.
Hospitali watahadharisha
Mmoja wa wauguzi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa siyo msemaji wa hospitali hiyo aliliambia gazeti hili kwamba hali ya kidonda cha Katarina, hata mtoto wake siyo nzuri na wanaweza kupata ugonjwa wa tetenasi, huku akiomba ndugu na wasamaria wema kuwasaidia waweze kupata tiba hospitalini.
Diwani
Richard Nyikera Diwani wa Kata ya Sedeco anakiri matukio ya ukatili kukithiri eneo lake, akieleza kwamba elimu zaidi inahitajika kukomesha matukio hayo.
Akizungumzia tukio la mwanamke huyo na mwanawe kujeruhiwa, Nyikera anasema kuwa awali kulitokea ugomvi kati ya Katarina na mke mwenzake.
“Huyo mke mdogo alitoroka na kwenda Nyamongo kwa mjomba wake kwa madai ya kupigwa na mke mwenzake, lakini mke mkubwa naye alilalamika kupigwa na mume wake wakisaidiana na mke mdogo, sasa .kilichotokea hapo sijui,” anasema.
Mtendaji wa kijiji
Wakati diwani wa kata hiyo akieleza hayo, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Thomas Kurura anadai kutokuwa na taarifa ya tukio hilo kijijini kwake.
Mwenyekiti wa kitongoji 
Hata hivyo, mwenyekiti wa kitongoji hicho Nyandema Mashora, anakiri kutokea  tukio hilo akieleza kuwa haijulikani alipo mtuhumiwa wa tukio hilo akidai kuwa (Matata), alionekana akikodi pikipiki huku akieleza anakwenda kujisalimisha polisi.
“Polisi wamefika hapa bila mafanikio, tukimwona tutatoa taarifa ili akamatwe kwa kuwa kila mmoja anajua unyama alioutenda,” anasema.
Dawati la jinsia
WP Sajenti Sijali Nyambuche wa Dawati la Jinsia wilayani humo anasema kuwa licha ya juhudi za Kamanda wa Polisi Wilaya kutoa gari ili kumsaka Matata, lakini hawajamkamata  kwa kuwa ametoroka eneo hilo.
“Tunakosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa vijiji, wanashiriki
kuwaficha wahalifu na kusababisha kesi zilizoko kwenye dawati letu kukosa mwelekeo mzuri. Tumefika kijijini hawakutoa ushirikiano, tukamchukua mke wake wa kwanza atusaidie, lakini jamii na viongozi wangekuwa wanasaidia, ukatili ungepungua,”anasema.
Matukio ya ukatili
Mratibu wa dawati hilo anakiri kuongeza kwa matukio ya ukatili wilayani humo, akieleza kwamba ukatili huo sasa uko katika sura tatu.
Anazitaja sura hizo kuwa ni ukatili kwa wanawake, watoto na wanawake kuwafanyia ukatili wanaume, ambao hata hivyo huona aibu kujitokeza tofauti na walivyo wanawake.
“Pamoja na mkakati wetu kwa kushirikiana na mashirika yasiyo yakiserikali kutoa elimu kwa jamii, bado hali ni mbaya, kila wiki lazima mpokee matukio ya ukatili, naomba jamii kwa pamoja tushirikiane ili kujenga taifa lenye ustawi,”anasema.
Kutokana na kukithiri kwa ukatili kwa wanaume sasa dawati hilolinaundwa na askari mchanganyiko wakiwemo wanaume tofauti na awali.
Wanaharakati waomba
Donald Mewama kutoka Shirika la Wasaidizi wa Kisheria na Haki za Binadamu (Washehabise) anasema kuwa kukithiri kwa ukatili wa kijinsia siyo dalili njema ya utawala bora kwa kuwa haki hazitendeki ndani na nje ya familia.
“Mwaka huu kutafanyika ukeketaji ni ukatili wanaofanyiwa watoto wa kike, Serikali na vyombo vyake vinatakiwa kuanza mapema mikakati ya kudhibiti  hali  hiyo,”anasema akitahadharisha.
 Chanzo: Mwananchi

0 comments: