Mpaka sasa panaweza kuwapo makundi
mbalimbali yanayofikiri kwa mitazamo tofauti. Kuna wasiotaka kuamini
mpaka leo hii mafanikio waliyofikia, wanajiuliza maswali pasipo kupata
majibu.
Hata hivyo kuna wale ambao ni mashabiki wafuatiaji
wa Bongo fleva hapa nchini ambao wanaweza kujibu vyema endapo
wataulizwa swali la kupima bora wa msanii huyu wa kike anayeonekana kuwa
na sifa zote za kuvalishwa heshima ya Malkia wa Bongo fleva.
Judith Wambura maarufu pia kwa jina la Komando,
Binti machozi au Anaconda ndiye anayezungumziwa leo hasa kutokana na
mafanikio yake katika tasnia ya muziki hata kudumu kwa muda mrefu kwenye
ushindani wa soko la muziki huo.
Starehe imefanya uchunguzi na tathmini kuangalia,
kulinganisha na kujiridhisha kwamba Lady Jay Dee anaweza kuwa ndiye
Malkia wa Bongo Fleva akilinganishwa na wasanii wengine wote wa kike
nchini katika muziki huo.
Tathimini ya Starehe imezingatia vigezo katika
maeneo mbalimbali kupitia heshima yake kimuziki, kudumu kwake muda
mrefu(ukongwe) na tuzo nyingi alizowahi kutunukiwa. Pia Lady Jay Dee
kuwa msanii ndiye aliyeshirikishwa zaidi na wasanii wengine, kuwa na
mafanikio ya kipato kikubwa na kufanya shoo kubwa za ndani na kimataifa.
Sifa na vigezo hivyo vinaweza kukuachia swali hili; hivi Jay Dee hafai
kutawazwa rasmi kuwa Malkia wa Bongo Fleva kwa sasa?. Hapana shaka jibu
zuri unalo wewe mpenzi wa muziki na msomaji.
Tuzo alizochukua
Jay Dee anatajwa kuwa msanii mwenye tuzo nyingi
kuliko wasanii wengine wa kike kwani hadi sasa amenyakua tuzo mbalimbali
ndani na nje ya nchi zinazofikia 26. Mwaka mwaka 2000/01 alifanikiwa
kupata tuzo ya mwanamziki bora wa kike katika Tuzo za M-NET, kabla ya
kutunukiwa tuzo tatu za Video Bora za Channel O maarufu kama ‘Channel O
Music Video Awards’.
Tuzo hizo ni pamoja na ile ya Video Bora Afrika
Mashariki kupitia albamu yake ya Machozi (mwaka 2003), na mwaka
uliofuata wa 2005 pia wimbo huo ulishinda Tuzo ya Video Bora ambapo pia
alipata Tuzo ya Video Bora ya Kushirkishwa kwa video iliyoitwa Makini
Wanadamu, iliyochezwa na msanii Titi wa nchini Uganda mwaka huo huo wa
2005.
Jaydee alipata pia tuzo ya Wimbo Bora wa Distance(mwaka 2004 hii ilikuwa ya BBC))
Mbali na tuzo hizo kuna nyingine tano
alizofanikiwa kutunukiwa nchini Uganda moja ikitambulika kama ‘Pearl of
Africa Music Awards’ ambapo Jay dee aliibuka Mwanamziki Bora wa Kike kwa
mwaka 2006, 2007, 2008, 2010 na 2011.
Katika upande wa tuzo za Kilimanjaro hapa nchini,
Jay Dee ametunukiwa tuzo 10 katika kipindi cha miaka 12 iliyopita.
Baadhi ya tuzo ni pamoja na Tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike na Video ya
mwaka(2002, 2009, 2010, 2011, 2012 na 2013.
Nyingine ni pamoja na Tuzo ya Albamu Bora kwa
mwaka 2004, Mwimbaji Bora wa Kushirikishwa(2008), Wimbo Bora Afrika
Mashariki(2011), akishirikishwa na mwanamuziki Kidumu kutoka nchini
Burundi. Hadi sasa hakuna msanii wa kike nchini aliyefikia idadi hiyo ya
tuzo.
Wasanii aliofanya nao ‘kolabo’
Kuna wanamuziki nyota wa nyumbani akiwemo Mr II,
AY, Profesa Jay na wengine kadhaa waliofanikiwa kushirikishwa katika
nyimbo nyingi kuliko wasanii wengine.
Hata hivyo, Jay Dee ni kuwa mmoja kati ya wasanii
watatu wanaoongoza kushirikishwa katika nyimbo za wasanii mbalimbali za
wasanii wa ndani na nje. Baadhi ya nyimbo alizoshirikishwa kimataifa ni
pamoja na wimbo Nitafanya wa msanii Kidumu wa Burundi, Sirimba wa Ngoni
kutoka Uganda, Njalo na Wadubadubaza za Mina Nawe wa Afrika Kusini,
Mimi ni mimi wa Oliver Mtukudzi wa Zimbabwe na Africa wa Salif Keita wa
nchini Mali.
Kwa upande wa Bongo Jay dee ameshirikishwa katika
zaidi ya nyimbo 50 na wasanii tofauti ambapo baadhi zikiwa Bongo Dar es
Salaam wa Profesa Jay na Machoni Kama Watu wa AY
Nyingine ni Mambo ya Fedha wa msanii Joseph
mbilinyi (Mr Sugu), ambaye sasa ni mbunge, Mambo bado wa Chege, Nimpate
Wapi wa Rich Longomba na Sikiliza wa marehemu Ngwair.
Hapo pia ni wazi kwamba hakuna msanii mwingine wa kike ambaye amefanikiwa kushirikishwa kama Lady Jay Dee.
Matamasha makubwa aliyofanya
Akizungumza na Starehe, meneja wa msanii huyo
Gadna G Habash, anataja onyesho la kwanza na kubwa alilowahi kufanya Jay
Dee kuwa ni pamoja na fainali za kumtafuta mshindi katika mashindano ya
ubunifu ‘Kora All Africa Designers Competition’ ya mwaka 2001.
“Yalifanyika Sun City, Afrika Kusini, kulikuwa na
wasanii wakubwa aliyoshiriki nao kama vile Shaggy wa Marekani na Oliva
Mutukuzi wa Zimbabwe, ikiwa ni tamasha lake kubwa la kwanza kushiriki,”
anasema na kuongeza:
Tamasha lingine ni uzinduzi wa Tuzo za Kora
lililofanyika nchini Benin mwaka 2007, ambapo pia alifanikiwa kukutana
na wasanii wengine wakubwa kama vile P Squire.
Wenzake wanamzungumziaje?
Mbali na tathmini hiyo, mwanamuziki wa kike kutoka
Kundi la Wakilisha, Sara Kiasi maarufu kwa jina la Shaa anakiri kwamba
Jay Dee anastahili sifa zote za kuitwa Malkia kutokana na jinsi
alivyomfahamu. “JAY Dee alinishtua na kuniongezea ujasiri wa kuamini
hata mimi ninaweza kufika mbali baada ya kuona video yake ya Machozi
katika Kituo cha Channel O’, wakati huo nikiwa shule ya msingi,” anasema
Shaa na kuongeza:
“Lakini mpaka sasa anaonekana kufanya vizuri zaidi tofauti na
wasanii wengine wa kike alioanza nao, kwa hivyo nasema; ‘Mnyonge
mnyongeni lakini haki yake mpeni. Sista Jay Dee anastahili heshima hiyo.
Historia yake kimuziki
Binti huyu wa mzee Mbibo kutoka kijiji cha
Manyamanyama, wilaya ya Bunda, mkoani Mara, alianza muziki akiwa na
umri wa miaka saba kupitia huduma za uimbaji wa kwaya katika Kanisa la
Kisabato mkoani humo, kabla ya kumaliza elimu yake ya msingi katika
miaka 1990.
Jay Dee alijiunga na huduma hiyo bila kujua kwamba leo angeweza kuwa mmoja kati ya nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini.
Juhudi zake kimuziki zilichangia kumjengea heshima
katika medani hiyo tangu mwaka wa 2000 na hadi sasa amefanikiwa kuwa na
kapu lenye albamu tano ambazo ni Machozi aliyoitoa mwaka 2000, Binti
(2003), Moto (2005), Shukrani (2007), Best of Jaydee(2011) na Nothing
But The Truth(2013). Rekodi hiyo ya kuwa na albamu tano pia haijafikiwa
na msanii mwingine yoyote wa kike nchini.
Mafanikio yake
Albamu ya Machozi ilifanikiwa kumweka katika
thamani ya kuwa msanii wa kwanza wa Bongo Fleva ikitajwa kutumia gharama
kubwa kuiandaa katika historia ya muziki wa kizazi kipya nchini kwa
wakati huo. Jay Dee kwa sasa anamiliki studio yake ijulikanayo kama Jag
Records.
Pamoja na mengi aliyofanikiwa katika maisha
kupitia muziki, kipimo chake kwa sasa kimezua gumzo katika ukurasa wa
wasanii wenye utajiri mkubwa baada ya kununua usafiri mpya wa gari la
kifahari aina ya Range Rover Evoque..
0 comments:
Post a Comment