LATEST POSTS

Friday, January 31, 2014

Mwanamke achinjwa, kichwa chawekwa kwenye sufuria

JESHI la Polisi mkoni Rukwa linawashikilia watu wanne kwa tuhuma ya mauaji ya mwanamke mmoja aliyeuawa na kichwa chake kuwekwa kwenye sufuria ya kupikia ugali na kutelekezwa kwenye uwanja wa kuchezea mpira.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema jana kuwa tukio la kuuawa kwa mwanamke huyo, Ritha Malechela (35), lilitokea mwanzoni mwa wiki hii huko katika Kijiji cha Kisa wilayani Sumbawanga mkoani humu.
Mwaruanda alisema kuwa awali mama huyo alikuwa anaishi na mpenzi, Josephat Chinga (32) baada ya kutoroka kwa mume wake ambaye hakutajwa jina lake, ghafla nako alitoweka katika mazingira ya kutatanisha, ndipo mwanzoni mwa wiki hii walikuta kichwa chake kimewekwa kwenye kiwanja kimoja cha mpira kijiji hapo.
Mwaruanda aliongeza kuwa, kichwa hicho kilikutwa kikiwa ndani ya sufuria na pembeni yake kukiwa na barua inayosadikiwa kuandikwa na mmoja wa watuhumiwa waliomuua mama huyo ambaye anadaiwa kuandika barua hiyo baada ya kushindwa kulipwa ujira wake alioahidiwa kulipwa baada ya kumua mwanamke huyo.
Alisema kuwa, barua hiyo ilikuwa imeandikwa majina ya waliohusika na mauaji hayo baada ya kushirikiana na anayedaiwa kuwa mpenzi wa marehemu huyo kwa lengo la kupata viganja vyake vya mikono ambavyo inasemekana kuwa vilikuwa na alama ya 'M' ambavyo aliondoka navyo kwa madai ya kwenda kutengeneza dawa ili apate utajiri.
Inadaiwa kuwa, baada ya mauaji hayo kiwiliwili cha mama huyo kilitupwa ndani ya Ziwa Rukwa na kichwa kufukiwa chini huku taarifa zikidai kuwa, mpenzi wake aliahidi kulipa Sh 400,000 kwa kila mmoja aliyeshiriki mauaji hayo ndipo wauaji hao walipoamua kuvujisha siri hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, waliohusika na mauaji hayo ambao wamekamatwa katika tukio hilo Joseph Milumba (31), Geofrey Ndenje(27) na mwanamke aitwaye Grace Sindani (40) anayedaiwa kuwa alihusika kwenye njama hiyo kwa kumshawishi marehemu huyo kuondoka kwa mpenzi wake ili waweze kufanikisha mauaji hayo.

Chanzo: Majira

0 comments: