Zaidi ya magari 1,000 yamekwama kwenye Barabara Kuu ya Mwanza -
Dar es Salaam katika Kijiji cha Ngonho, Kata ya Miguwa, wilayani Nzega,
kutokana utekaji wa malori uliofanywa juzi usiku.
Baadhi ya madereva walisema walikutwa na mkasa huo
juzi saa nne usiku wakati magari yao yalipotekwa na watu wanaosadikiwa
ni majambazi na kuwanyang’anya mali na kisha kuwatendea ukatili wa
kuwajeruhi sehemu mbalimbali za miili yao ikiwa ni pamoja na kuwakata
masikio na kuwatoboa macho.
Kutokana na tukio hilo, waligoma kuondoa magari
yao na kusababisha mabasi ya abiria na malori ya mizigo kukwama wakati
abiria wapatao 3,000 wakitaabika kwa kukosa chakula na maji.
Madereva hao waligoma kuondoa magari yao baada ya
kukasirishwa na kitendo cha polisi wa Nzega kushindwa kuwasaidia wakati
walipotekwa.
Madereva hao wameapa kutoondoa magari hayo hadi
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe au
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa watakapofika kwenye eneo hilo ili
kusikiliza kilio chao.
Unyama wa watekaji
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya
Nzega, Emmanuel Mihayo alisema watu walijeruhiwa vibaya kwenye utekaji
huo kwa kukatwa masikio na kutobolewa macho.
Dk Mihayo aliwataja majeruhi hao kuwa ni raia wa
Burundi, Herelina Eddy, ambaye alitobolewa macho na hali yake ilikuwa
mbaya na alikuwa kwenye maandalizi ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya
Nkinga kwa matibabu zaidi.
Alisema majeruhi wengine wawili wanaendelea vizuri
na matibabu katika hospitali hiyo. Majeruhi hao ni Abraham Ismail na
Omary Adrian, ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam.
Alisema Adrian alikatwa sikio na shavu pamoja na mkono wa kushoto wakati Ismail alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
Polisi watuhumiwa
Mmoja wa madereva waliotekwa, ambaye aliomba jina
lake kuhifadhiwa alisema kuwa polisi wa Nzega waliombwa kutoa msaada
lakini walikataa.
Dereva huyo alisimulia kuwa mmoja wa madereva alifanikiwa
kutoroka wakati walipotekwa na kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha
Polisi cha Wilaya ya Nzega lakini askari waliokuwepo kituoni hawakutoa
ushirikino.
“Polisi hao walitoa visingizio, wakidai kwamba
gari lao halina mafuta na walikataa kutumia lori la dereva huyo kwenda
kwenye eneo la tukio,” alisimulia dereva.
Baada ya kunyimwa msaada, dereva huyo alilazimika kurudi kwa wenzake ndio akajikuta akitekwa tena.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Peter Ouma,
ambaye alifika kwenye eneo la tukio, aliahidi angewachukulia hatua kali
polisi hao.
“Nawaahidi ndugu zangu, hawa waliosababisha hali
hii wote nawachukulia hatua kali za kinidhamu mara mmoja na taarifa hizi
mtazisikia kwenye vyombo vya habari,” aliahidi Kamanda Ouma, huku
akiwaomba madereva wa malori na magari ya abiria waendelee na safari
zao.
Hata hivyo, madereva hao waligoma kuendelea na
safari na badala yake walisisitiza kuwa wanataka askari waliokuwa doria
wachukuliwe hatua za kinidhamu.
“Tunalishangaa Jeshi la Polisi, wameshindwa
kutusaidia na matukio kama haya yamezidi hapa Nzega tunataka Waziri Mkuu
na Waziri wa Mambo ya Ndani wachukue hatua... hatuondoki mpaka
kieleweke,’’ alisema dereva mwingine, ambaye pia aligoma kutaja jina
lake.
Madereva hao walisema vitendo vya utekaji magari
katika Wilaya ya Nzega, vimekuwa vikitokea mara kwa mara na kuhatarisha
maisha ya watu, magari na mali zao.
“Hivi mbona tukiendesha magari haya na kwenda nchi
za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hatupati
matatizo haya ya kutekwa,” alihoji dereva mwingine.
Mateso kwa abiria
Kutwa nzima jana, mabasi na magari madogo
yalikwama katika eneo hilo na kusababisha foleni kubwa, hivyo
kusababisha adha kwa wasafiri, hasa wanawake na watoto.
Kutokana na hali hiyo, wachuuzi wa bidhaa
mbalimbali walitumia fursa hiyo kujineemesha kwa kuuza vitu kwa bei ya
juu, ambapo chupa ya maji ya kunywa nusu lita iliuzwa Sh1,000 badala ya
Sh500 wakati ile ya lita moja Sh2,000 badala ya Sh1,000.
Aina zote za soda ziliuzwa Sh2,000 badala ya kati ya Sh600 hadi
1,000 wakati sahani moja ya chakula kwa mamalishe iliuzwa kati ya
Sh3,000 na Sh5,000.
Mmoja wa abiria alionekana akilalamika na kutoa
maneno makali ya kuwashutumu madereva kwa kuwasababisha adha hiyo pamoja
na Serikali kushindwa kuwasaidia.
“Sisi tunataabika, hatuna msaada. Watoto wetu
wanateseka, wengi wetu tumeishiwa, hatuna fedha,” alilalamika Mariamu
Majara, abiria aliyekuwa akisafiria kwenye basi la Kajumulo lililotoka
Mwanza kwenda Dar es Salaam.
Taarifa ambazo zililifikia gazeti hili jioni zilisema, mgomo huo ulimalizika na mabasi kuanza kuondoka saa 1:30 usiku.
0 comments:
Post a Comment