Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamemvamia na
kumjeruhi kwa risasi, mfanyabiashara maarufu wa simu jijini Mbeya,
Obadia Mtawa (41).
Vitendo hivyo vimefuatiwa na kumpora mamilioni ya fedha, simu na gari la kutembelea.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni, muda mfupi baada
ya Mtawa kurejea nyumbani kwake katika Mtaa wa Isyesye, akitokea katika
shughuli zake katika eneo la Ilomba.
Alikuwa na gari lake lililokuwa na kasha lenye fedha na simu za aina mbalimbali.
Akizungumzia mkasa huo akiwa katika wodi ya Mifupa
katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Mtawa alisema akiwa njiani kurejea
nyumbani aliona pikipiki mbili zilizokuwa nyuma yake, zikiwa zimewashwa
taa.
Alisema pikipiki hizo zilikuwa na watu waliokuwa wamepakizana.
Alisema baada ya kushuka kwenye gari lake
akijiandaa kuingia ndani, alisikia sauti za watu wapatao wanne
wakimwambia kuwa yuko chini ya ulinzi na kwamba mmoja wao aliipiga panga
lake kwenye gari lake.
“Niliposhuka kwenye gari wakaingia ndani na kusema
nipo chini ya ulinzi na baadaye wakapiga risasi ambazo moja ilinipiga
mguuni kisha wakaniuliza fedha ziko wapi,” alinena.
Alisema aliwajibu kuwa fedha zilikuwa kwenye gari
na kuwataka wazichukue. “Wakachukua funguo za gari na kisha wakaingia
kwenye gari na kuoondoka nalo likiwa na fedha na simu,” alisema.
Alisema kiasi cha fedha kilichochukuliwa hakijui
lakini zilikuwa za mauzo ya siku nzima ya juzi na kwamba kwa wastani
maduka yake yanakusanya Sh50 milioni.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba polisi walikuwa
wakiwasaka watu hao.
Msangi alisema juhudi za wananchi na polisi
zilifanikiwa kuliona gari la Mtawa katika maeneo ya Uyole na kwamba hadi
jana hakuna mtu aliyekamatwa.
Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kuna watu waliokuwa wakimfuatilia Mtawa kwa muda mrefu.
Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kuna watu waliokuwa wakimfuatilia Mtawa kwa muda mrefu.
0 comments:
Post a Comment