MWANACHAMA mkongwe wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa chama hicho
mkoani Dar es Salaam, Bw. John Guninita, ameitaka CCM kupitia Idara ya
Maadili, kumdhibiti Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Bw.
Nape Nnauye.
Bw. Guninita aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari na kusisitiza kuwa, Bw. Nnauye ni
kiongozi asiyefaa katika nafasi aliyonayo na kutaka aondolewe katika
chama kwani amekuwa akifanya kazi za chama bila kujali mipaka yake.
Alisema hakuna kikao cha CCM kilichokaa na kutoa tamko la kuwepo 'Mawaziri Mizigo' wanaostahili kuchukuliwa hatua.
"Wamekwenda
kwenye mikutano ya hadhara na kutaja majina ya Mawaziri wanaodai kuwa
ni mizigo, mimi kama mwanachama mstaafu wa CCM, naamini waliotangazwa
kwenye mikutano hiyo hawakuwatendea haki," alisema Bw. Guninita.
Aliongeza
kuwa, Bw. Nnauye ni kiongozi anayeogopa demokrasia ya kuchaguliwa ndiyo
maana hata nafasi aliyonayo hakugombea ameipata 'kimjomba mjomba'.
Majibu ya Nape
Akijibu
tuhuma hizo, Bw. Nnauye alisema kitendo cha Bw. Guninita kudai amepewa
nafasi hiyo 'kimjomba mjomba' ni kuwatukana wajumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa (NEC), kutoka Wilaya zote nchini ambao walipitisha jina lake.
Bw.
Nnauye alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, mbali ya Bw. Guninita
kuwatukana wajumbe wa NEC pia amemtukana Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais
Jakaya Kikwete ambaye ndiye aliyependekeza jina lake na kulipeleka
kwenye kikao cha NEC ili liweze kupitishwa na wajumbe.
Alitolea
mfano wa Waziri Mkuu, anapoteuliwa na Rais jina lake hupelekwa bungeni
ili liweze kupitishwa na wabunge hivyo uteuzi wa nafasi yake nao
ulizingatia vigezo hivyo na kumshangaa Bw. Guninita kwa kutojua mifumo
ya utendaji kazi ndani ya chama hicho.
"Anasema nimepewa cheo
kiujomba ujomba... Rais ni Mkwere na mimi ni Mmakonde huo ujomba unatoka
wapi, hayo ni matusi makubwa kwa wajumbe wa NEC na Rais, namshangaa
huyu mzee ambaye anajiita mstaafu wakati alifukuzwa na wanachama.
"Watanzania
wanaijua vizuri historia ya Guninita kwani ndiye aliyehusika kuyauza
majimbo ya Ubungo na Kawe kwa wapinzani katika Uchaguzi Mkuu uliopita,"
alisema Bw. Nnauye.
Alisema Bw. Guninita alikurupuka kusoma taarifa
yake kwa vyombo vya habari kwani hakuna kipengele kilichoonesha amepinga
uteuzi wa Rais katika Baraza la Mawaziri.
"Guninita hana kazi ya
kufanya, alinyimwa kura na wana CCM ambao walimfukuza hivyo Watanzania
wampuuze na kumsamehe kwa kauli zake," alisema.
Akizungumzia rai iliyotolewa na makundi mbalimbali ya kijamii na vyama vya siasa kumtaka Bw. Nnauye na Katibu Mkuu wa CCM,
Bw.
Abdulrahman Kinana wajiuzulu nafasi zao baada ya Rais Kikwete
kuwarudisha baadhi ya Mawaziri waliolalamikiwa, alisema "Sisi ni watu
wazima, tumesikia maoni yao".
Pia Bw. Nnauye alitolea ufafanuzi
kauli ya Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa Mawaziri
Mizigo wanatokana na chama mzigo, alisema kiongozi huyo ameanza kuzeeka
vibaya.
"Huwezi kusema chama mzigo wakati watendaji ndiyo mizigo,
Lipumba anastahili kupewa cheti cha mgombea bora wa urais anayeshindwa
kila uchaguzi," alisema.
Aliongeza kuwa , C C M inamuandalia cheti
cha kumpongeza Prof. Lipumba kwa kuwa mgombea bora anayeshindwa tangu
mwaka 1995 hadi sasa hivyo Watanzania wamsamehe, waendelee kuiamini CCM
kwani ndicho chama chenye uwezo wa kuwapigania na kushughulikia kero
zao.
0 comments:
Post a Comment