DIWANI wa Kata ya
Mswaha-Darajani, Tarafa ya Mombo, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga (CCM),
Aweso Kipaku (34), amejiuzulu nafasi hiyo akipinga hatua ya Mkuu wa
Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo, kumuweka ndani.
Akizungumza na
mwandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Kipaku alisema Bw. Gambo aliagiza
awekwe ndani Januari 24 mwaka huu, saa 11 jioni na kupata dhamana saa
nne usiku.
Alisema polisi walimkamata, kumpeleka Kituo cha Korogwe
lakini Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani, alikwenda
kumuwekea dhamana na kufanikiwa kutoka.
Mbali ya Kipaku, wengine
waliokamatwa na kuwekwa ndani ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha
Mswaha-Darajani, Bw. Abbas Siafu na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha
Mswaha-Darajani, Bw. Said Kijiwa.
Chanzo cha kukamatwa kwao ni
tuhuma zilizotolewa dhidi yao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya
wakidaiwa kuchochea mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye Kijiji cha
Mswaha-Darajani.
"Juzi tuliitwa kwa Mkuu wa Wilaya na viongozi
wenzangu, baada ya kumalizika Kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu
wa Wilaya (Gambo) alimuamrisha OC-CID anichukue na kuniweka ndani hadi
nilipopata dhamana usiku.
"Najiuliza mimi kiongozi wa wananchi
nadhalilishwa kwa kufungwa pingu, kukaa chini tena nikisukumwa, je,
wananchi wangu wapo salama kiasi gani... nimeamua kujiuzulu nafasi ya
udiwani kwa vile nimedhalilishwa sana," alisema.
Kipaku alisema
tayari ametoa taarifa ya kujiuzulu kwake kwa Katibu wa CCM mkoani humo,
Gustav Muba jana ambapo zaidi ya wanachama 300 wa chama hicho
wanaomuunga mkono wamerudisha kadi.
Aliongeza kuwa, sababu
iliyomfanya awekwe ndani ni kitendo cha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa
Kijiji uliofanyika Januari 21 mwaka huu na kudaiwa anachochea mgogoro wa
wakulima na wafugaji.
"Wakulima wanataka wafugaji waondoke wakidai
mifugo yao inakula mazao...Gambo aliahidi angekwenda kusimamia kazi ya
kuwaondoa wafugaji kwenye eneo husika lakini hakufanya hivyo mara tatu,
leo hii anasema sisi viongozi wa kata ndiyo tufanye kazi hiyo kana
kwamba tuna Jeshi la Polisi," alisisitiza.
Alisema Januari 22 mwaka
huu, watu wasiojulikana walikwenda kuchoma moto mazizi ya wafugaji
lakini chanzo si viongozi wa kata ni viongozi wa Wilaya na Mkoa ambao
wamechelewa kuchukua hatua za kumaliza mgogoro husika.
Juhudi za
Majira kumpata Bw. Gambo kuzungumzia sakata hilo zilishindikana ambapo
juzi alipigiwa simu lakini ilipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,
Alhajj Majid Mwanga akidai wapo Tanga kwenye kikao na kuhoji mnataka
kuzungumza na Mkuu wa Wilaya kwa suala lipi.
Jana simu yake ilikuwa
ikiita bila kupokelewa ambapo Katibu wa CCM mkoani humo, Muba alikiri
kupokea taarifa ya kujiuzulu diwani huyo lakini hakuwa tayari kuzungumza
lolote akidai bado hawajajadili uamuzi wake kama wamkubalie au
wamkatalie.
"Nimepewa taarifa hiyo lakini tunasubiri barua rasmi,
sisi kama chama lazima tumjadili na turidhike na kile kilichofanya
ajiuzulu, kama hakina mashiko tunajadiliana na kumuomba aendelee kuwa
diwani," alisema Muba.
0 comments:
Post a Comment