Nzega. Licha ya Serikali kupiga vita kujichukulia sheria
mikononi, unyanyasaji na mauaji ya wanawake, baadhi ya wananchi wa
Kijiji cha Uchama wilayani Nzega mkoani Tabora wamemuua mwanamke mmoja
na mtoto wake wa kike kwa sababu zisizofahamika.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa
Polisi mkoani Tabora, Peter Ouma alisema tukio hilo limetokea Januari 17
mwaka huu katika kijiji hicho.
Kamanda Ouma aliwataja mama na mtoto waliouawa
kinyama na watu wasiofahamika kuwa ni Amina Kabingu(45) na mwanaye Shija
Mtaki(12) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi
Uchama.
Alisema kuwa Amina Kabingu na mtoto wake shija
walikuwa wakisafisha majaruba ya kulimia mpunga katika mashamba yao
majira ya jioni, ndipo watu wasio fahamika waliwavamia na kuanza
kuwashambulia kwa vitu vyenye ncha kali kusababisha kupoteza maisha yao.
Diwani wa kata hiyo, Karoli Masanja alilitaka
jeshi la jadi la Sungusungu kuwasaka wauaji hao kwa kushirikiana na
Polisi ili kuwabaini wahalifu hao waliofanya ukatili.
Karoli alisema serikali ichukue hatua kali
kudhibiti mauaji hayo ikiwa ni pamoja na vyombo vya dola kuzingatia
wajibu wake wa kutenda haki kwa jamii husika.
Toka Januari 1 mwaka huu hadi Januri 18 mwaka huu
wanawake watatu wameuawa kinyama huku mmoja akipigwa na kubakwa ikiwa ni
pamoja na kuvunjwa baadhi ya viungo vya mwili wake.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment