Wanawake wanachukuliwa kama ni watu wa kubaki katika ndoa kutii amri za mume hata kama amri hizo siyo za haki, heshima au zinavunja utu wa mwanadamu.
Kwa mfano, gwiji la fasahi ya Kiswahili, marehemu
Sheikh Shabaan Robert katika kitabu chake “Maisha yangu na baada ya
miaka hamsini” katika ukurasa wa kumi anatoa wasia kwa bintiye kwa
kumwambia;
“Fanya kila hali, la mume kulikubali, ila lisilo
halali, kukataa si hatia” Hapa anampa ujasiri mwanawe wa kike kutokubali
mambo ya ovyo kutoka kwa mume, ana mjengea uwezo wa kuwa mwanamke na
mama shupavu katika maisha ya ndoa yake na kuweza kukabiliana na
familia.
Matukio ya kutendewa isivyo wanawake siyo mageni,
wanawake wamekuwa wakipata vipigo, kuteswa na wengine kufikia hata
kujeruhiwa hapa Zanzibar.
Wanawake Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi ngumu,
wana mzigo wa kuhudumia familia, wanafanya biashara, wanafanya kazi
ofisini huku wakisubiriwa kupika, kuchota maji, wanabeba mimba na
kujifungua na wakati mwingine hata hayo matunzo ya mama mjamzito
hayapati hasa wanawake wa vijijini.
Katika sehemu za mashamba Unguja na Pemba,
wanawake wanalima, wanapanda, wanapalilia, wanachuma karafuu huku
wengine wakianguka na wasipofikisha vyakula vinavyotakiwa, anapata
matusi na hatimaye kuambulia kipigo.
Katika utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa
Mjini Magharibi Unguja, kati ya Novemba hadi Desemba mwaka jana,
Zanzibar kuna matukio kadhaa ya wanawake kupata vipigo kutoka kwa waume
zao.
Ijapokuwa TAMWA katika utafiti huo wanasema kwamba
hulka ya kuwapiga wanawake siyo matukio maarufu sana, ukweli ni kwamba
wanawake wengi wa Zanzibar ni wasiri mno, hata akipigwa au kuteswa hawi
wazi kutangaza.
Mathalan mmoja ya wanawake aliyehojiwa Mtaa wa
Kwamtipura, analalamikia hulka ya mumewe ya kumpiga mara kwa mara hasa
pale anapodai huduma muhimu kama chakula na ikiwa akimweleza upungufu
basi inakuwa nongwa na sababu ya kuanza kupokea vipigo!
Mwanamke huyu hivi karibuni alipokea kipigo pale
aliposema kiwango cha chakula alichoachiwa ni kidogo na hakiwezi
kumtosha, ndipo mume wake alianza kumfokea kwa maneno machafu na kuanza
kumpiga jambo ambalo lilimfanya mwanamke huyo kukimbilia kwa Sheha
Machano Khamis kwenda kujisalimisha.
Wanawake wanaopata vipigo kwa hakika ni wengi,
lakini wamekuwa wakitofautiana kutokana na sehemu hadi sehemu. Wapo
wanaopigwa kwa madai ya kudai haki za msingi za mke ikiwamo kupatiwa
huduma za mahitaji ya chakula, mavazi na hata kufanya kazi.
Miongoni mwa sababu za kushamiri kwa vitendo vya
kupigwa wanawake na waume zao ni pamoja na wivu wa mapenzi, ulevi,
kugombania watoto na mali na kuporomoka kwa maadili katika jamii.
Akizungumzia hilo, Sheha wa Kwamtipura, Machano Khamis anasema
mara nyingi chanzo cha kipigo ni wanaume ambao wanawapiga wake zao
wanapolalamikia haki zao.
Lakini anakitaja chanzo chengine ni ulevi, na hili
limejitokeza sana katika Shehia yake ambapo amekuwa akilalamikiwa mara
nyingi na wanawake kupigwa kwa sababu ya ulevi wa waume zao
Maelezo hayo yanasadikiwa pia na Makadhi wa
Mahakama za Kadhi wilaya, Afisa wanawake na watoto wilaya na hata Polisi
ambao wote kwa nyakati tofauti wanaeleza sababu cha wanawake kupigwa
katika ndoa na hata wale wasiokuwa katika ndoa.
Sababu kubwa inayozifanya kesi hizi zisiripotiwe
ni wanawake kuona aibu, na upigaji huo kuchukuliwa kama adabu ya kawaida
tu anayopewa mwanamke kwa sababu ya kukosea.
Pia wanawake licha ya kuwa wanaumizwa vibaya
lakini wanakataa kutoa taarifa kwa kuogopa kuvunjika kwa ndoa zao. Hapa
hatupaswi kuwatupia lawama wanawake kwani ni mfumo ndio uliowafikisha
hapo walipo wanawake kuonekana kuwa hawana sauti katika jamii.
Katika utafiti huo wa TAMWA, ripoti inasema kwamba
katika kipindi cha kuanzia mwezi Juni mwaka 2011 hadi Machi mwaka 2012
kuna kuna matukio matano ya wanawake kupigwa na waume zao na kuripotiwa
Polisi lakini wanawake waliofikwa na mkasa huo wapo wengi isipokuwa
hawafiki katika vyombo vya kisheria.
Mbali ya hao wanaokwenda vituo vya Polisi na
baadhi ya wakati kesi hizo kumalizwa kienyeji, wengine wanakwenda katika
Mahakama ya Kadhi kudai talaka baada ya kuchoshwa na vipigo.
Kuna kesi 10 zimeorodheshwa katika mahakama hizo
ambapo walalamikaji(wanawake) wanataka kuvunja ndoa wakiepusha miili yao
kugeuzwa ngoma na waume zao.
Wakizungumzia kadhia wanayopata wanawake hapa
Zanzibar kwa mtazamo wa kidini, viongozi wa dini tafauti wanasema kwamba
dini haijatoa ruhusa kwa wanaume kumpiga mkewe bali wanaume wanapaswa
kuishi na wake zao kwa mapenzi na huruma kwani wao ndio walinzi na
walezi wa familia.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar(SUZA), Dk. Sheikh Issa Ziddy r anasema “Uislamu haujaruhusu kwa
hali yoyote udhalilishaji ingawa suala la kumpiga mwanamke limetajwa
katika Quraan na mafunzo ya Mtume kuna hadithi zinazokataza mtu kumdhuru
mwenzake”
Anasema kuna masharti yamewekwa kabla ya mume
kufikia hatua ya kumwadabisha mkewa, lakini kabla ya kufikia hatua ya
kumpiga kipigo kisichodhuru mume anatakiwa kutimiza mambo matano ambayo
ni kuwa mume haruhusiwi kumpiga mkewe kwa kosa lolote hadi kosa hilo
liwe kubwa na uzito wa pekee.
Pia kabla ya hatua ya kumpiga anapaswa kwanza
kumpa nasaha mkewe kwa kosa alilotenda na sharti la pili ni kumpa
mawaidha amma yeye mwenyewe au atafute mtu aje kumpa mawaidha.
Sharti la tatu ni kumkumbusha mara kwa mara huku sharti la nne
kumhama malazi yaani kumuacha akalala peke yake, sharti la tano kwenda
kushitaki kwa wazee au katika vyombo vya sheria ikiwemo kwa Kadhi na
viongozi wa dini na la sita ndio kumpiga, lakini kipigo ambacho
hakitomdhuru huku sharti la kumpiga mwanamke hutakiwi kumpiga ukiwa na
hasira.
“Ukishawekewa masharti kama hayo matano sharti la
mwisho ikiwa mke hasikii ndio umeruhusiwa kumpiga lakini unatakiwa
usimpige ukamuumiza wala usimpige ukiwa na hasira lakini hapo hapo
unaambiwa hupaswi kumdhuru mwengine basi ndio baadhi ya wanazuoni husema
kupiga haijaruhusiwa kwa mantiki hiyo” aliongeza Sheikh Ziddy.
Hakuna mwanamke ambae amehojiwa akasema kuwa
mumewa kabla ya kufikia kumpiga amefuata maagizo hayo ya dini kwa upande
wa waumini wa kiislamu zaidi ya kujiona wao ndio wenye uwezo wa kufanya
watakalo kwa kumpiga mwanamke kwa nguvu na kumuumiza vibaya.
Kwa upande wa dini ya Kikristo, Father Emmanuel
Masoud wa Kanisa la Anglikan anasema kuwa hakuna andiko linalofundisha
kwamba mwanamme ampige mke wake bali wanaume wanahimizwa kuwapenda na
kuwatunza wake zao kama wanavyojipenda wao wenyewe na kumpa mke heshima
ili maombi yao yakubalike kwa Mola.
Father Masoud anasema tatizo la kupiga wanawake
ndani ya wakristo lipo kutokana na mapokeo ya kimila hasa mfumo dume na
mfumo jike, kuna baadhi ya makabila kama mume hampigi mkewe anaonekana
hampendi au anaambiwa ametawaliwa na mkewe.
Father Masoud anasema wakristo wanaungozwa na
kitabu kitakatifu cha Biblia na wamekatazwa kuwapiga wanawake na
wamesisitizwa kuishi nao kwa wema ili waombi yao yakubaliwe.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, moja ya mambo
ambayo yanawaumiza wanawake karibu kote duniani ni ukiukwaji wa haki za
binadamu wanazofanyiwa na matokeo ya hayo ni maumivu ya kimwili na
kisaikolojia wanayopata wanawake.
Wanawake wanateseka katika vita, katika matukio ya
kigaidi, wengine wanakufa kwa njaa, kwa kukosa maji na huduma nyengine.
Inakisiwa kuwa asilimia 80 ya wakimbizi wote ni wanawake waliokimbia
machafuko ya kisiasa, vita na matukio mengine.
Huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC)
Mapigano yameacha athari kubwa kwa jamii, wakina mama na watoto ndio
wanaopatwa na majanga kama hayo yanayosabishwa na vita wengi wao hivi
sasa wanaishi katika maisha ya dhiki wakiwa wakimbizi.
Zanzibar haikuwa nyuma katika masuala ya
kuathirika kwa wanawake na matukio ya machafuko ya kisiasa. Mwaka 2001
wanawake kadhaa walifanyiwa vitendo vya kikatili, wengine walikimbia
nchi kwenda Shimoni Mombasa Kenya kunusuru maisha yao.
Ni Wanawake hao hao wanaowapa vipigo hapa Zanzibar
ndio wanaokuwa mstari wa mbele katika kuwachagua viongozi mbalimbali wa
kisiasa, kwenye mikutano ya vyama vya kisiasa ni wanawake ndio
wanaojaza uwanja.
Wanawake wa Zanzibar walijitolea mali na maisha
yao kuunga mkono, juhudi za kisiasa na kijamii, wengi wao ama
hawajulikani kabisa au wamewekwa kwenye kapu la sahau kwa makusudi au
kwa bahati mbaya iwapo viongozi wakishaingia madarakani.
Chanzo: Mwananchi
Hawakuwa wanaume tu waliosimama mstari wa mbele katika mapambano
ya kudai uhuru, bali kulikuwa na wanawake shupavu, hodari na mahiri
ambao walikuwa sehemu ya kuanzishwa kwa vuguvugu la madai ya kisiasa,
lakini mambo yanapokuwa mazuri wanawake wanaelezwa kazi yao ni jikoni!
Wengi wetu tunafahamu kwamba historia ya mapambano
ya wanawake inakwenda mbali zaidi, wakati wa kutafuta uhuru ni wanawake
waliojitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya vyama vya ukombozi, wengine
wakasimama kwenye majukwaa kupaza sauti za ukombozi wakiwashinda wanaume
woga.
Katika matukio mengi ya kisiasa husikii kabisa
kutajwa kwa mchango wa wanawake katika harakati za mapambano ya kudai
uhuru. Hili linafanywa kwa makusudi kwani ni aina ya wanaume wanaowapiga
wanawake ndio hao hao wengine wanajitumbukiza katika masuala ya kisiasa
na kuhodhi madaraka.
Jambo la muhimu kwa kila mwana jamii ni
kuhakikisha haki, maslahi na wajibu wa kila mmoja unatimizwa na
kuheshimiwa. Elimu zaidi inahitajika kwa ngazi zote kuona kwamba
wanawake waishi katika dunia ya amani na yenye kuwaheshimu Zanzibar na
kwengineko.
0 comments:
Post a Comment