WAKATI
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiko njia panda baada ya Mwenyekiti wake,
Rais Jakaya Kikwete, kuwarejesha mawaziri ‘mizigo’ waliopendekezwa na
chama chake wang’olewe, makundi ya urais yameanza kupigana vikumbo
kuwania nafasi tatu za ujumbe wa sekretarieti.
Nafasi hizo nyeti ndani ya chama hicho tawala, ziko wazi baada ya
Rais Kikwete kufanya mabadiliko ya mawaziri na kuwaondoa wajumbe watatu
wa sekretarieti na kuwaingiza kwenye Baraza la Mawaziri.
Nafasi za ujumbe wa sekretarieti, zinapiganiwa kwa udi na uvumba,
kwani ndio wanaosukuma ajenda kwenda Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu
(NEC) na hatimaye Mkutano Mkuu.
Pia wajumbe wa sekretarieti wanapata fursa ya kuwa wajumbe wa Kamati Kuu na NEC taifa.
Wajumbe walioondolewa kwenye sekretarieti ni pamoja na Naibu Katibu
Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba, ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Fedha,
Wizara ya Fedha na Uchumi (Sera).
Wengine ni Asha-Rose Migiro, ambaye kwa mabadiliko hayo anakuwa
Waziri wa Katiba na Sheria na Jenista Mhagama, Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, akichukua mikoba ya Philip Mulugo, aliyetupiwa
virago.
Chini ya utaratibu mpya wa CCM, wajumbe wa sekretarieti wanaoteuliwa
kuwa mawaziri wanalazimika kuachia nafasi zao za chama ili wawe na muda
zaidi wa kuitumikia serikali.
Kutokana na nafasi hizo kuwa wazi, habari zinasema vikumbo vya kujaza
nafasi hizo vimeanza, huku makundi ya urais yakijipanga kuhakikisha
wanapenyeza watu wao.
Kwa kawaida, nafasi hizo hujazwa baada ya Mwenyekiti wa CCM taifa,
Rais Kikwete kuteua majina ya makada anaotaka waingie kwenye
sekretarieti na kisha majina hayo huthibitishwa na Kamati Kuu (CC) na
kupigiwa kura na wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.
Licha ya mamlaka ya uteuzi kuwa chini ya Rais Kikwete kama ilivyo kwa
mawaziri, vigogo na makada waliokaribu na rais wameanza kuhaha kutumia
mbinu mbalimbali kuhakikisha majina ya watu wao yanateuliwa.
Pamoja na nafasi ya Migiro na Mhagama, nafasi ya Mwingulu, ya Naibu Katibu Mkuu Bara, ndiyo inayotolewa macho zaidi.
Duru za siasa ndani ya CCM zinataja majina mawili, mosi la aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na Nape Nnauye, ambaye
kwa sasa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi taifa.
“Kuna uwezekano mkubwa kati ya mawaziri wanne waliong’olewa bungeni,
wawili wanaweza kuingia kwenye sekretarieti. Nchimbi ana nafasi ya
kuziba nafasi ya Nchemba kuwa naibu katibu mkuu,” alisema mtoa habari
wetu.
Kwa mujibu wa habari hizo, mwingine anayetajwa huenda akateuliwa
kuziba nafasi ya Waziri Migiro ni Balozi Khamis Kagasheki ambaye kabla
ya mabadiliko ya mawaziri, alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Duru za siasa ndani ya CCM z
inamtaja Balozi Kagasheki kufiti kwenye
nafasi ya Migiro kutokana na uzoefu wake wa siasa za nje alipokuwa
Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali.
Hivi karibuni, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
kwa kuwateua wajumbe watatu wa sekretarieti ya CCM kuwa mawaziri na
kufanya kuwapo sura kumi mpya.
Pia aliwarejesha mawaziri ‘mizigo’ ambao hivi karibuni walipendekezwa
na Kamati Kuu (CC) ya CCM kwamba wang’olewe kwa utendaji wao mbovu.
Chimbuko la mawaziri ‘mizigo’ lilitokana na ziara ya Katibu Mkuu,
Abdulhaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi taifa, Nape Nnauye
katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambapo waliwataja baadhi ya waziri
kuwa ni mizigo.
Mawaziri waliotajwa kuwa ‘mizigo’ ni pamoja na Waziri wa Kilimo na
Chakula, Christopher Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.
Shukuru Kawambwa, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Waziri wa Maji, Profesa
Jumanne Maghembe.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment