LATEST POSTS

Friday, January 24, 2014

Zitto ruksa kukata rufaa Chadema



Kutokana na uamuzi huo, Zitto sasa ataweza kukata rufaa ya kupinga kuvuliwa madaraka kwenye Baraza Kuu la chama hicho. 

Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umempelekea Zitto Kabwe taarifa ya kikao cha Kamati Kuu kilichomvua madaraka yake ndani ya chama hicho ili aweze kukata rufaa.
Habari za kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kuwa Kamati Kuu ya chama hicho ilifikia uamuzi huo wakati wa vikao vyake vilivyofanyika kati ya Januari 3 na 4, mwaka huu.
Kutokana na uamuzi huo, Zitto sasa ataweza kukata rufaa ya kupinga kuvuliwa madaraka kwenye Baraza Kuu la chama hicho.
Taarifa zinaeleza kuwa kamati hiyo ilimwagiza Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kumpatia mwenendo wa kikao Zitto ili aweze kukata rufaa.
Dk Slaa alithibitisha jana kuwa chama hicho tayari kimetuma muhtasari wa kikao hicho kwa Zitto, ambaye alikuwa anauhitaji hadi kufikia hatua ya kufungua mashtaka mahakamani.
Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando alisema wamepokea barua hiyo na walikuwa wanajiandaa kukata rufaa.
“Ni kweli tumepokea taarifa ile na tulikuwa tuna fursa ya kuchagua kukata rufaa au la, lakini tumeisoma na tumeona tukate rufaa,” aliongeza Msando.
Alisema hatua hiyo, bado haitasimamisha kesi inayoendelea mahakamani, bali walalamikiwa sasa wana fursa ya kuitisha kikao cha Baraza Kuu na kupima kama wana haja ya kuendelea na kesi.
Gazeti hili limeshuhudia barua hiyo iliyotumwa kwa Zitto, Januari 20, 2014 ikiwa na namba ya kumbukumbu namba C/HQ/ADM/KK/08/40.
Katika barua hiyo, Zitto aliarifiwa kuwa Kamati Kuu ya Chadema katika kikao chake cha Januari 3 na 4, 2014 kiliandaa taarifa kamili ya mwenendo wa shauri lake.
“Kwa kuwa Kamati Kuu ilikuwa ikitambua umuhimu wa yeye kupewa nakala za mwenendo huo wa uamuzi wa kikao hicho, ilimwagiza Katibu Mkuu wa Chadema kumpatia Zitto nakala za mwenendo wa kikao.
Barua hiyo inaeleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya taarifa ya Zitto iliyoeleza nia yake ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati Kuu, wa kumvua nyadhifa zake.
Zitto alivuliwa nyadhifa zake na Kamati Kuu ya chama hicho, Novemba 21, mwaka jana kwa kosa la kushiriki katika kupanga njama za kuhujumu chama hicho.
Alivuliwa madaraka pamoja na makada wengine, aliyekuwa  Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, ambao walituhumiwa kuhusika na kuandaa waaraka uliokuwa na lengo la kuvuruga uongozi wa chama hicho.
Wote watatu walipewa siku 14 za kujieleza ili wasitimuliwe kutoka kwenye chama hicho, lakini Zitto aliamua kukata rufaa kwenye Baraza Kuu wakati wenzake hawakukata rufaa na matokeo yake wakavuliwa uongozi Januari 6, mwaka huu.
Zitto alifungua shauri Mahakama Kuu akiitaka kuushinikiza uongozi wa chama hicho kumpa taarifa ya kikao kilichomvua madaraka ili akate rufaa kwenye Baraza Kuu.
Pingamizi Mahakama Kuu
Katika hatua nyingine, Chadema wamewasilisha pingamizi la awali lenye sababu sita kwenye Mahakama Kuu wakiiomba iitupilie mbali kesi iliyofunguliwa na Zitto.
Zitto katika kesi yake anaiomba mahakama izuie chama hicho na wakala wake, na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote wala kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi hapo rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama hicho kupinga kuvuliwa nyadhifa, itakaposikilizwa.
Pia anaiomba Mahakama Kuu imwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie mwenendo na taarifa za kikao cha Kamati za kumvua nyadhifa zake zote ndani ya chama na iwazuie walalamikiwa kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake kama Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Mawakili wa Chadema, Tundu Lissu, Peter Kibatala na John Mallya wamewasilisha pingamizi zao za awali kwa njia ya maandishi juzi Mahakama Kuu wakiiomba iitupilie mbali kesi hiyo kwa sababu haina msingi na gharama zilipwe na Zitto walitoa sababu sita.
Katika sababu ya kwanza, mawakili hao wanadai kuwa shauri hilo halina msingi kwa vile halikuwahi kusikilizwa kwenye mahakama ya chini.
Sababu ya pili wanaiomba mahakama iitupilie mbali kwa vile imewasilishwa kwenye masijala kuu ya Mahakama Kuu badala ya ile ya wilaya.
Wanadai katika sababu ya tatu kuwa kesi hiyo haina msingi kwa kuwa mlalamikaji hajaomba maoni ya Mahakama Kuu kuhusiana na suala lake la uanachama wa Chadema.
Nne, wanadai kuwa anaendesha mashauri mawili ya kukata rufaa ili kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema kwa wakati mmoja, jambo ambalo ni matumizi mabaya ya mahakama.
Tano,  wanaiomba mahakama itupilie mbali kesi hiyo kwa madai kuwa haina msingi kwa vile Mahakama Kuu siyo mahali pake pa kulishughulikia shauri hilo kwa sababu mlalamikaji hajatumia ipasavyo ngazi za chama.
Sita, wanadai kuwa mahakama haina mamlaka ya kutoa uamuzi wa maombi ya Zitto aliyoyaweka katika kesi yake kwa sababu itakuwa inaingilia mamlaka ya vyama.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa Februari 13, mwaka huu mbele ya Jaji John Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Slaa amweka kando Zitto
Katika hatua nyingine, Dk Slaa amesema kuwa hatua ya chama hicho kumwadhibu Zitto inalenga kudumisha nidhamu ndani ya chama hicho.
Akihutubia mkutano wa hadhara huko Rungwe jana, Dk Slaa alisema chama hicho kinapaswa kutilia mkazo suala hili kwa kuwa kinajiandaa kuchukua dola.
“Haya mambo yanatokea hata nyumbani kwetu, lazima kuna wakati inatokea mtu mnatofautiana lakini suala la nidhamu ni muhimu,” alisema Dk Slaa, ambaye alieleza alilazimika kuzungumzia suala hilo baada ya kunong’onezwa na mtu mmoja.

0 comments: