LATEST POSTS

Sunday, March 23, 2014

SALAMU ZA PONGEZI KWA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE

Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM - 2014, Paul C. Makonda.

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI

Utangulizi:

Ndugu waandishi wa habari, mabibi na mabwana. Leo tena nimewaita kwa ajili ya kuzungumza mambo machache muhimu yahusuyo taifa letu Tanzania.
Yangu leo ni machache na muhimu ni kutoa salamu za pongezi za Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba murua aliyoitoa Juzi 21/03/2014 wakati akizindua bunge maalum la katiba.
Kama taasisi…
Katibu wa Hamasa na Chipukizi UVCCM - 2014, Paul C. Makonda.

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI

Utangulizi:
Ndugu waandishi wa habari, mabibi na mabwana. Leo tena nimewaita kwa ajili ya kuzungumza mambo machache muhimu yahusuyo taifa letu Tanzania.
Yangu leo ni machache na muhimu ni kutoa salamu za pongezi za Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba murua aliyoitoa Juzi 21/03/2014 wakati akizindua bunge maalum la katiba.
Kama taasisi muhimu katika taifa hili, tumechukua hatua hii madhubuti kulieleza taifa umuhimu wa ile hotuba, mantiki iliyopo katika ile hotuba, na kwa kuwa sisi tunawakilisha sauti za vijana zaidi ya milioni 25 wa taifa hili, na kwa kuwa athari nyingi za katiba hii tunayotengeneza zitawaathiri sana vijana kuanzia sasa na mustakabali wao.
Hatuwezi kukaa kimya ama tukaungana na wale wenye kulaumu pasipo kujua mantiki, maana mwisho wa siku vijana hawatawalaumu wale wanaowapotosha kwa sauti zao kali, bali watawalaumu wale walio na ufahamu na wakakaa kimya kama Martin Luther "King" alivyowahi kusema;
"In The End we will remember, Not the Voices of Our Enemies, but The Silence of Our Friends".
Sisi ni rafiki wa Taifa hili na watu wake, hatuwezi kukaa kimya huku tukiwaona wale wasitutakia mema wakiendelea kueneza sumu mbaya ya kutugawa katika makundi makundi.

Ndugu waandishi, Tanzania ina watu
milioni 49 (kwa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 na makadirio yake ya mwaka 2013). Kwa kuwa bunge hili maalum limechukua mfumo wa uwakilishi wa watu wote kwa makundi yao (
yaani fair representation), kwa bunge lenye wajumbe 619, maana yake ni kuwa, kwa wastani kila Mbunge anawakilisha Watanzania 79,000. Sasa hapa ndipo kwenye kazi na mantiki tunayoijenga; kwamba
i. Ikiwa Mbunge mmoja atasimama bungeni na kutekeleza wajibu wake ipasavyo, basi sauti za watanzania 79,000 zitakuwa zimewakilishwa vema, na akifanya tofauti yake halikadhalika haohao watanzania kwa hasara yao.
ii. Fikiria kwa mfano Mbunge akasimama dakika tano akatumia muda huo kutukana badala ya kujenga hoja kwa manufaa ya taifa, maana yake ni kuwa hawa watanzania elfu 79 wamepoteza dakika 79000x5=4,345,000 ambayo ni sawa masaa 72,461 ama siku 3,071 ambayo kimahesabu ni karibu miaka kumi. Hebu fikiria huyu ni Mbunge wako yaani kwa kitendo cha dakika tano amekufanya umepoteza miaka 10 kwa kutukana mfululizo.
iii. Ikiwa Mbunge atatumia hizo dakika tano, badala ya kujenga hoja zenye maslahi ya taifa na badala yake ajenge hoja ya ama chama chake cha siasa ama kundi lililompeleka, ama kwa kushawishiwa na mwingine ambaye anataka kutimiza matakwa yake, basi Raia ambaye anawakilishwa na huyu mtu, ni sawa na kwamba ameishi miaka kumi katika uso wa dunia hii bila malengo.
Ndugu waandishi, hesabu hizo hapo kwa udhahania wake zina maana tu kama wabunge wote wa bunge hili watathamini nafasi zao kama ni tunu kwa ustawi wa taifa na si ustawi wa ama wao binafsi ama taasisi zao, ama vyama vyao vya siasa ama madhehebu ama kitu kingine chochote.
Yale ambayo mheshimiwa Rais amewaasa wabunge na wanachi kwa ujumla ni kuhakikisha kuwa wanajiridhisha na mwenendo mzima kutoka mwanzo wa mchakato hadi tutakapofika mwisho wa mchakato huu na kupata katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Umuhimu wa hotuba ya rais kwa upande wetu UVCCM tumechukua mambo mawili muhimu 1. Rais Kutupitisha katika Historia muhimu ya taifa letu kuhusu Katiba, Muungano, Masuala mengine ya Muungano na Michakato ya maamuzi ya masuala yahusuyo utawala wa taifa letu; na 2. Umuhimu wa kutumia historia ya kila jambo wakati wa kufanya maamuzi yahusuyo jambo hilo;
1. Kutupitisha katika Historia ya Taifa
Kwanza tuseme wazi, vijana wa CCM tumeridhika pasi na shaka kwa mtindo ambao Rais aliutumia kuwaeleza wabunge na watanzania kwa kina ufanisi na kwa lugha inayoeleweka kirahisi historia ya michakato mbalimbali tuliyopitia kama katiba, tangu mwaka wa uhuru wa iliyokuwa Tanganyika (Tanzania Bara) na Zanzibar.
Mabadiliko makubwa ya katiba ya nchi hizi mbili ya mwaka 1965 na yale ya mwaka 1977. Marekebisho mengi ya katiba yamefanyika kati ya mwaka 1977 na 2013/14. Marekebisho yote yalihusu utashi wa serikali zote mbili (ya jamhuri na ile ya Zanzibar) katika azma ya kufikia mafanikio ya kujenga taifa lililo na heshima, lenye kuheshimu misingi ya utawala wa kidemokrasia, sheria na haki.
Historia hujenga ama hubomoa taifa. Hakuna ujenzi wa taifa bila kujua historia ya taifa husika. Kuijua historia yetu si tu kwamba inatupa nafasi ya kujisikia na kujivuna watanzanaia, bali inatupa naafasi ya kuwa na fikra pevu zaidi, juu ya hatua gani tuchukue kuendelea kuijenga Tanzania yetu katika mshikamano, umoja na udugu ikiwa kazi kubwa waliyoweza kuifanya waasisi wetu.
Leo hii kitendo cha baadhi ya watu kuwabeza waasisi wetu, ni kubeza historia yetu, na kitendo cha kulibeza taifa letu. Sababu bila juhudi zao na kutokuwa kwao wabinafsi, leo tunaishi kama familia moja. Anayedharaua historia yetu, na asiyetaka kujifunza kutoka kwa waliotutangulia, huyo ni mtumwa.
Katika idadi ya watu milioni 49, tuliopo, asilimia 44.8% (ambao ni karibu milion 22 ni watoto chini ya miaka 15 na asilimia 62.3% (ambao takribani watu milion 31) wana umri chini ya miaka 25. Ukienda mbele kidogo kwenye takwimu, utakuta kwamba asilimia 92.3% ya watanzania wanaishi kwa utegemezi, yaani maana yake takribani watu milioni 45 wa taifa hili ni wategemezi si wazalishaji na kwamba wazalishaji ni milioni nne tu.
Na hii inatokana, kwanza na ile asilimia 44.8% ya watoto na kwa kiwango kikubwa asilimia 64% ya vijana walio chini ya miaka 25 kwa maana kwa taifa letu, kijana wa miaka 25 bado si mzalishaji maana ama bado anawategemea wazazi wake, ama bado yupo shule. Takwimu hizi pia zaonyesha, wastani wa umri wa watanzania ni miaka 17, umri wa juu wa Mtanzania kutegemea kuishi umekadiriwa kuwa ni miaka 60. Tanzania na takwimu kama hizi, lazima wajifunze na kuelewa kwa undani mambo yahusuyo taifa.
Kuijua Historia ya nchi yako, kuwa na ufahamu wa takwimu muhimu zihusuzo uchumi na idadi ya watu na makazi, inakupa mwanga bora wa kutengeneza sera, kanuni na sheria zitakazolinda mustakabali wa taifa lako na ustawi wake.
Fikiria kwa mfano karibu nusu ya watanzania wana umri wa chini ya miaka 15, halafu wastani wa umri wa watanzania ni miaka 17, wakati huo huo sheria za nchi zinasema wale wanaoweza kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi ni wenye umri kuanzia miaka 18, je unafanya nini kutengeneza sera zitakazobeba masuala haya kwa pamoja.
Badala ya kutumia nguvu kutaka kulazimisha mambo fulani ambayo watu kama viongozi wanayataka, ni vema tukaijua historia, tukajua mahitaji muhimu kwa sasa na wakati ujao ndipo tutaweza kufikia kutengeneza taifa lenye uchumi endelevu unaostawi na kuwa mfano kwa Afrika na duni kwa ujumla.
Sisi UVCCM tumeamua kulisemea hili kwa uwazi na kwa sauti pana ili kuujuza umma wa watanzania kwamba wawapuuze wale wote wanaotaka kuwaondoa katika mchakato huu muhimu na kuwapeleka kule wasikotaka. Tunatambua nia njema ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi na dhamira ya dhati kuhakikisha tunapata katiba Mpya.
Na sote tunatambua kuwa kama serikali isingekuwa na nia njema, basi Tume maalum ya Katiba isingeundwa, au ingeundwa lakini isingejihusisha na ukusanyaji wa maoni nchi nzima. Na ikumbukwe, mchakato huu umepitia changamoto nyingi sana. Pamoja na changamoto hizozilizokuwa na kila sababu ya kukwamisha zoezi la mchakato wa katiba hii, Rais wetu kipenzi alisimama imara na kuhakikisha anatatua changamoto zote hizo ili kutimiza adhima na ndoto za watanzania kupata katiba mpya.
Tunathamini kwa asilimia 100% kazi iliyofanywa na tume chini ya Uenyekiti wa Jaji J.S. Warioba. Wapo ambao badala ya kujikita na maana halisi ya kazi hizi na hotuba za viongozi hawa, wao wanajihusisha na kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa lengo la kujikusanyia wafuasi pasipo kutazama kwa kina zaidi mahitaji ya watanzania ya sasa na kila changamoto ya muundo wa serikali kwa siku zijazo.
Na ndiyo maana Rais akiwa mkuu wa nchi ametoa taswira pana zaidi ya kule tulikotoka, tulipo na kule tuendako, na kuwataka wabunge wapime kila hoja na kila muunda wa serikali ili kuipatia Tanzania na Katiba inayotekelezeka. Cha ajabu, wapo walioanza kujipanga kuanza kuharibu dhana zima iliyoko katika dhamira ya viongozi wa taifa hili. Hizi ni hila mbaya ambazo hazikubaliki katika taifa la watu waliostaarabika Tanzania.
Kitendo cha Rais kutoa historia ndefu ya kule tulikoanzia na tulipo kuhsiana na katiba, muungano, Afrika Mashariki, masuala ya muungano, Mahusiano ya Zanzibar na Tanzania bara, kwanza inatoa morali kwa vijana na watoto kutamani kujifunza zaidi, inatoa wajibu kwa wabunge kujisomea zaidi na kuja na uelewa mzuri wa masuala yote yahusuyo taifa. Ametoa wajibu kwa maneno ya wazi kabisa;
"Akili ya kuambiwa, Changanya na ya Kwako"
Sisi tunaweka changamoto hapa, Ili uweze kuchanganya na ya kwako, sharti uwe nayo. Na namna pekee ya kuwa nayo, ni kusoma rasimu ya katiba kwa bidii, sura kwa sura, sehemu kwa sehemu, ibara kwa ibara, msitari kwa msitari, neno kwa neno na nukta kwa nukta. Si kukaa na kusubiri tu nani aseme ili ama uzomee ama upige makofi.
Rais Kikwete kwa matukio mawili ameiweka nchi kwenye ramani ya ulimwengu kuwa ni taifa ambalo linafanya mambo yake kwa utaratibu wa kisheria unaokubalika kimantiki na kwa utaratibu ambao hauleti migogoro na pale kunapotokea migongano, kumekuwa na njia muafaka za kuimaliza. Alifanya hivyo kule Afrika kusini kwenye maziko ya mwanamapinduzi halisi wa Afrika Hayati Nelson Mandela Madiba na amefanya hivyo Juzi Dodoma. Huu ndio ukweli, kama kuna ambaye hataki aje na hoja si kuja na ubishi usio na maana.
2. Umuhimu wa kutumia Historia katika kufanya maamuzi
Watanzania wachache sana walijua mahusiano yaliyokuwepo kati ya masuala yahusuyo muungano na uwepo kabla wa jumuiya ya afrika Mashariki na baadaye uvunjifu wake mwaka 1977. Taifa kwa miaka yote limepitia kwanza historia ya masuala hayo kabla ya kufanya maamuzi.
Hata muundo wa Bunge maalum la katiba umezingatia hali halisi ya sasa, uhitaji mkubwa wa watanzania kutaka katiba, ongezeko la mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia na hata kutengeneza katiba inayohusisha angalau uwakilishi wa watanzania wote (fair representation).
Itoshe kukubaliana kwamba, endapo wabunge wa bunge maalum la katiba watajipa muda mwingi wa kujisomea tafiti mbalimbali, historia ya taifa hili na mataifa mengine mengi duniani yaliyofikia hatua kama tunayoiendea, tukasoma vizuri rasimu ya katiba pamoja na ripoti ya Tume ya Warioba pamoja na ripoti mbalimbali za zamani zilizopelekea marekebisho ya katiba ya mara kwa mara (toka mwaka 1977), basi ni imani ya sisi vijana kwamba, tutatoka na rasimu nzuri ya katiba, si tu kwa mantiki ya kuisoma na kuielewa, bali iliyo na sura ya kutekelezeka na endelevu kwa ustawi wa taifa la Tanzania.
Na ndipo dhana ya kurekebisha, kuongeza, kupunguza ama kuja na rasimu mpya inapokuwa na nguvu. Wabunge wakisoma vema wana mamlaka ya kufanya hayo si tu kukaa pale bungeni na kugonga meza ama kuzomea. Kabla ya kufanya lolote, wabunge wafikirie dakika watakazozitumia kwa niaba ya watanzania (kama tulivyofafanua hapo juu).
Watanzania wanasubiri rasimu ya tatu kutoka katika bunge hili. hawatajali kama watakubaliana na hii, watairekebisha au watatengeneza nyingine, mwsiho wa siku wanasubiri rasimu watakayoipigia kura ya ama kukubali ama kukataa. kwa waungwana watakubaliana na mchakato mzima mpaka hapa na wataendelea kusubiri hatua zinazofuata.
Mungu Ibariki TANZANIA

PAUL C. MAKONDA
Katibu Wa Hamasa Na Chipukizi UVCCM - 2014

0 comments: