LATEST POSTS

Friday, March 28, 2014

SIRI YA CCM KUNG'ANG'ANIA SERIKALI MBILI KIKATIBA

katuni 83f0e
Katika maisha ya kawaida, binadamu ana msimamo wake na hata uamuzi asiopenda ubadilike.
Katika medani ya siasa nchini msimamo wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) kuhusu Muungano na muundo unafahamika. Ni muundo wa kutaka Serikali mbili ambao chama hicho unakipigania kwa udi na uvumba.(Hudugu Ng'amilo)
Hata hivyo, msimamo huo ni kinyume na mapendekezo au matakwa ya wengi kama ilivyoainishwa kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume hiyo iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba ilikusanya maoni ya wananchi na ilipendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Hivi karibuni akifungua Bunge Maalumu la Katiba, Rais Jakaya Kikwete akaunga mkono msimamo wa chama chake, jambo lililoibua mjadala unaoendelea hadi sasa.
Hoja ya Serikali mbili
Kwanini CCM wanataka Serikali mbili na siyo tatu au moja kama ilivyo maoni ya wananchi walio wengi kwa mujibu wa maelezo ya Tume ya Warioba? Makala haya yanachambua hoja hiyo.
Profesa Bakar Mohammed ni Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anayesema msimamo wa CCM wa kudai Serikali mbili unatokana na hofu ya uhafidhina wa kuogopa mabadiliko.
Anasema viongozi wengi wa CCM wanasumbuliwa na hofu na woga wa mabadiliko na kwamba wanakuwa wagumu kuyakubali yanapotaka kutokea.
"Kama mtu unaangalia madaraka zaidi, lazima kunakuwa na woga, na hii ni hulka ya binadamu kuwa na woga wa kuacha kile ulichokizoea... Lakini ukiangalia masilahi ya nchi na kuacha yale yanayokusukuma kusingekuwa na wasiwasi huu unaoonekana sasa," anasema.
Anasema CCM inachofanya ni kuhakikisha haking'oki madarakani, huku viongozi wake wakiamini kuwa wana sifa za kuongoza na siyo wengineo.
Profesa Bakari anailinganisha hofu ya sasa ya CCM na ile waliyokuwa nayo viongozi wa chama hicho miaka ya 1990 zilipoanza vuguvugu za mabadiliko ya siasa za vyama vingi. Anasema CCM kiliendesha propaganda kuwa mfumo wa vyama vingi haukuwa na tija na ungeleta vita.
Hofu hiyo anasema ndiyo inayokifanya chama hicho kikongwe kuhofia kung'olewa madarakani.
"Woga huo bado upo, wanaogopa pengine mfumo ukiwa wa Serikali tatu uwezekano wa wao kubaki madarakani utakuwa mdogo," anafafanua.
Anaongeza kusema kuwa hofu ya CCM siyo kwa ajili ya masilahi ya nchi, badala yake inaonekana chama kinaangalia masilahi yake.
Ingekuwa vyema anasema kwa CCM kueleza madhara yanayoweza kulikumba taifa ikiwa muundo wa Serikali tatu utapita.
"Wanatoa hoja kuwa mfumo wa Serikali tatu unaweza kusambaratisha nchi, lakini hakuna uhakika kama mfumo huu uliopo nchi hauwezi kusambaratika," anasema.
Hofu ya kuyumba na kuanguka
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk. Benson Bana anasema siri ya CCM kung'ang'ania Serikali mbili inatokana na hofu ya kuyumba na kuanguka.
Anasema CCM kimekuwa madarakani na mfumo huo kwa miaka 50 na kwamba hofu yao ni kuwa ukiondoa Serikali mbili kinaweza kuyumba na kuachia madaraka.
Anasema misingi ya wanasiasa ni madaraka, na kwamba ukishayapata, huwezi kuyaachia kirahisi.
"Misingi ya wanasiasa ni madaraka... Kuyalinda, kuyahifadhi na kuyatumia madaraka yale kwa namna yoyote...Huwezi kuyaachia madaraka kirahisi. Utafanya ujanja, utatumia mbinu chafu ili tu kuhakikisha unabaki madarakani, na hiki ndicho wanachofanya CCM," anasema.
Dk. Bana anasema CCM kingeeleweka na kingekuwa na mwonekano mzuri zaidi endapo wangepigania kuwapo kwa Serikali moja.
"Wangekuwa wanataka muungano imara, endelevu na uliokomaa wangeelekeza katika Serikali moja...Lakini hawataki kwa sababu wanajua moja inaweza ikawanyima uongozi," anasema.Dk. Bana anasema ni vyema wananchi wakaelimishwa huu muungano una faida gani na wanafunzi shuleni katika elimu ya uraia waelezwe faida zake.
"Ingekuwa wazi tungejua nani anafaidika na nini, mikopo misaada, nani anachangia nini...Je zile sababu za waasisi za kuungana bado zipo sasa miaka 50 ya Muungano, ule woga kuwa Zanzibar itamezwa bado upo leo?" Anahoji.
Anaongeza kuwa ni vyema kwa watawala kutazama mazingira ya sasa ya siasa zetu kwa kile anachoeleza kuwa hata Katiba ikipita ikakubali kuwapo wa Serikali mbili, bado wananchi watahoji mantiki ya muundo huo.
Msomi mwingine wa siasa, Dk. Alexander Makuliko anasema hofu ya CCM ni kuwa ndio iliyouasisi Muungano wa Serikali mbili, hivyo isingependa hali hiyo ibadilike.
Anaendelea kusema kuwa CCM imezoea mfumo huu na kuwa ikiukosa itaathirika, kwakuwa ni sera yake na imekuwa ikiitekeleza, lakini msimamo wa wananchi ndiyo kitu cha msingi kuzingatiwa. Hoja zijengwe na zisikilizwe, ubabe hautakiwi, busara inahitajika zaidi.
Anasema pamoja na suala la Serikali mbili kuwa ni pimajoto ya uhai wa CCM, hata hivyo hoja zinazotolewa katika kutetea msimamo wao ni nzuri tu na zinazoeleweka vyema.
"Sioni kama wanang'ang'ania, lakini ukweli ni kuwa kila chama kina sera yake, na CCM kimeweka sera yake katika suala la Muungano wao wanasema ni Serikali mbili, na siyo tatu...kwamba tatu zitaongeza gharama na mengineyo, ni sababu za msingi kabisa," anasema.
Anaongeza kuwa hoja zinazotolewa na chama tawala ni kubwa na siyo za kupuuzwa, lakini vilevile kero zinazotajwa kuhusu mfumo wa Muungano uliopo nazo zipo na zinaweza kutatuliwa katika mfumo uliopo.
"Unajua hivi vyama kila kimoja kinataka kuvutia kwake, hata bila rasimu ya Warioba...Ninashauri walete hoja, kisha watu wazipime hizo hoja, kwanini serikali mbili, na wale wa tatu tayari wameleta hoja na ushahidi, watu waachwe wapime," anasema na kuongeza:
''Jambo la msingi kuzingatiwa ni kuwa mawazo ya wananchi wengi yataonekana wakati wa kura za maoni. Angalizo ni kuhakikisha kuwa kura hiyo isije ikachakachuliwa.''
CHANZO MWANANCHI

0 comments: