LATEST POSTS

Thursday, March 27, 2014

TCME yamshukia Kigwangalla, aonywa

SHIRIKISHO la Wachimbaji na Watafutaji Madini na Nishati Tanzania (TCME), limelaani vikali maandamano ya wachimbaji wadogo yaliyoongozwa na Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamis Kigwangalla, kwani yalisababisha uvunjifu wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilo, Emmanuel Jengo, alisema, maandamano ya wachimbaji yaliyoongozwa na Dkt. Kigwangalla yameleta fedheha kubwa kwa sekta ya madini..
 Alisema wanaunga mkono uamuzi wa Serikali wa kufunga machimbo hayo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
"Tunalaani upotoshwaji wa kisiasa uliofanywa na Dkt. Kigwangalla, kuhusu umiliki wa weneo hilo , ni vyema ikaeleweka vizuri kwa viongozi wa siasa wa maeneo hayo na jamii kwa ujumla kwamba maandalizi ya shughuli za uchimbaji yanatokana na uwezekezaji mkubwa wa utafiti wa madini uliofanywa na kampuni ya resolute kati ya mwaka 2008 na 2009,"alisema Jengo.
Alisema jamii inatakiwa kuelewa kwamba eneo lililovamiwa na wachimbaji wadogo linamilikiwa na Kampuni ya Uchimbaji na utafiti wa Madini ya Resolute Tanzania ambao wana leseni halali ya kuchimba madini katika eneo hilo.
Aliongeza kuwa kitendo cha kiongozi kuhamasisha wachimbaji wadogo kuvunja sheria ni mfano mbaya sana kwa jamii na ni kitendo hatarishi kwa amani na utulivu katika maeneo mengine ya uchimbaji hapa nchini.
Pia alisema ni kosa kiongozi kufanya harakati zisizokubalika za kuwashawishi wananchi kujenga chuki dhidi ya wawekezaji, kitendo ambacho kinaweza kuchochea machafuko, uharibifu na kudhoofisha juhudi za dhati za serikali za kukuza uchumi kwa kuvutia uwekezaji na kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji.
Alisema ni vema kwa viongozi kutafuta taarifa za kweli kutoka kwa kampuni husika na idara nyingine za serikali kufikia ufumbuzi wenye busara kwa matatizo ya aina zote, kwani kama wana nia ya dhati kuwatetea na kuwaendeleza wachimbaji wadogo ni vyema wakashirikiana na Wizara ya Madini na Nishati kuomba eneo lingine kwa ajili yao.
Shirikisho linatoa rai kwa Serikali kusimamia sheria na kuendelea kutenga maeneo halali kwa ajili ya wachimbaji wadogo, pamoja na kuratibu shughuli za wachimbaji wadogo ili ziwe endelevu na kuchangia vema katika uchumi wa Taifa.
Pia alisema Serikali ina wajibu wa kulinda wawekezaji wa ndani na wa nje waliotumia fedha nyingi kufanya tafiti za ugunduzi unaofanywa na wachimbaji haramu kinyume na sheria kanuni na taratibu za nchi.

0 comments: