WIZARA ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, imebaini kuwepo mtandao wa wanaosafirisha
wasichana wenye umri mdogo kutoka nchini na kuwapeleka China kisha
kuwafanyisha vitendo vya ukahaba pasipo ridhaa yao.
Hayo yalisemwa
jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Wizara hiyo, Bernard Membe,
wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala
mbalimbali yanayohusu wizara yake.
Alisema mtandao huo
ukishasafirisha wasichana hao na kuwafikisha China, huwanyang'anya hati
zao za kusafiria na kujikuta wakishindwa kurejea nyumbani, hali
inayowalazimisha kujikuta wakitumbukia kwenye biashara hiyo.
Membe
alisema, taarifa ambazo wizara yake inazo ni kwamba, tayari mmoja wa
wasichana hao amefariki kwa kuuawa. Alisema mwezi uliopita walialikwa
kwenda nchini China, ambapo walibaini kuwepo kwa vitendo hivyo vya
kusafirisha wasichana kutoka Tanzania na kuwapeleka nchini humo ili
kuwafanyisha ukahaba.
"Inaelekea kuna Watanzania wanaokwenda nchini
China kwa kutumia nyaraka bandi, huku wengine wakitumia paspoti ya nchi
zingine wakati wao ni Watanzania ili kusafiri nje ya nchi kwa lengo la
kufanya biashara ambazo ni haramu," alisema Membe.
Alisema kutoka na
kukithiri kwa hali hiyo, Rais Jakaya Kikwete, atakuwa na ziara ya
kutembelea nchi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ataenda kujionea
hali halisi ya kuwepo kwa vitendo hivyo.
Kwa mujibu wa Waziri Membe,
zaidi ya Watanzania milioni 3 wanaishi nje ya nchi, lakini baadhi yao
wapo wanaofanya ukabaha, biashara za dawa za kulevya na ugaidi. "Kufanya
vitendo hivyo ni kuivunjia heshima nchi yetu," alisema na kuwataka
Watanzania wasirubuniwe kwenda nje ya nchi kwa kudhani kuwa maisha ya
huko ni rahisi.
Aliwataka wenye mitandao ya kuendesha madanguro ya
ukahaba nje kwa kutumia wasichana wa Kitanzania wajue kwamba kufanya
hivyo ni kosa la jinai. Aliwataka Watanzania wanaoishi huko waishi kwa
kufuata misingi ya nchi na taratibu husika ili kulinda heshima ya nchi.
0 comments:
Post a Comment