FALSAFA ya Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ya kuongoza Bunge hilo kwa kasi
na viwango, jana iliingia doa; na kulazimika kuahirisha Bunge hilo
baada ya kiti chake kutuhumiwa kuyumba katika kutetea kanuni
zilizopitishwa na Bunge hilo wiki tatu zilizopita.
Hali hiyo
ilijitokeza bungeni mjini Dodoma jana muda mfupi baada ya Bunge hilo
kuanza, ambapo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alianza
kuchangia kwa kutuhumu kiti cha Mwenyekiti wa Bunge hilo kutetereka na
kushindwa kusimamia kanuni.
Alisema ndani ya Bunge hilo viporo vya
kanuni vilivyokuwa vimebaki bila kutolewa maamuzi vilihusu kanuni ya 37
na 38 zinazohusu utaratibu wa upigaji kura, lakini inashangaza kuona
wamepewa jedwali lingine lenye mabadiliko ya kanuni kinyume cha
utaratibu.
"Mheshimiwa Mwenyekiti hapa tumeletewa jedwali lenye
marekebisho ya kanuni maalumu ambazo tayari zilipitishwa na Bunge
Maalumu na kuridhiwa," alisema Lissu.
Alitaja kanuni ambazo tayari
zilikuwa zimeridhiwa na Bunge hilo, lakini zilipelekwa zikiwa kwenye
jedwali hilo kwa ajili ya kufanyiwa mabadiliko kuwa ni kanuni ya 14 (1),
32, 33,35 na 51 (1) D.
Alitaja kanuni nyingine kuwa ni 63 (1), 64
(1) ambayo ilipitishwa na azimio la Bunge na ile ya 85 (4). Lissu
alisema mabadiliko hayo ya kanuni yamesainiwa na Katibu wa Kamati ya
Uongozi ya Bunge badala ya mwenyekiti.
Alisema kuwasilishwa kwa
jedwali hilo la mabadiliko ya kanuni ni kinyume cha kanuni ya 87 (2)
ambayo inaeleza utaratibu na mapendekezo ya marekebisho ya kanuni.
"Sasa
kanuni hazina hata wiki tatu mnaanza kuzichakachua... hiki mnachotaka
kukiingiza hapa kisiingizwe mpaka yatakapoletwa mapendekezo ya kanuni ya
37 na 38," alisema Lissu na kuongeza kuwa; "Kamati ya uongozi haina
mamlaka na mambo ya kanuni."
Lissu alienda mbali zaidi na kusisitiza
kuwa; "Hii ni takataka isiingizwe ndani ya Bunge hili, huu ni ubatili."
Akikazia zaidi msimamo wake, Lissu alisisitiza; "Hatuwezi kuruhusu
uchafu wa namna hii, hii ni takataka."
Lissu wakati akitoa hoja zake
alikuwa akishangiliwa na baadhi ya wabunge na wengine kuzomea. Baada ya
Lissu kumaliza kuwasilisha hoja hiyo ya kupinga jedwali hilo la
marekebisho ya kanuni, ndipo alipofuata zamu ya Mwenyekiti wa Bunge,
Sitta ambapo alisema;
"Hizi ni tuhuma nzito kwa mwenyekiti wa Bunge
(Sitta) na zinaelekezwa kwake wakati hicho kinachoongelewa hajakiona."
Alisema maelekezo yalitoka kwa Kamati ya Uongozi kwenda kwenye Kamati ya
Kanuni ni halali.
Sitta, alielezea kushangazwa kabisa na hali
iliyokuwa inatokea bungeni. Wakati hali ya mvutano ikiendelea, huku
kukiwa na hali ya kutoelewana na wabunge wengine kuzungumza bila kupewa
nafasi na kiti, Sitta alikuwa alitumia busara kuwatuliza wabunge hao
bila ya mafanikio.
Baadaye Sitta, alitoa nafasi kwa Mwanasheria wa
Serikali y a Mapinduzi Zanzibar, Abubakari Hamis, ambaye alianza
akishangazwa na msingi wa kutaka kufanyika kwa mabadiliko hayo ya kanuni
katika Bunge hilo.
Alisema kifungu cha 87 (2) cha kanuni
walizozipitisha kinaeleza utaratibu wa kubadili kanuni, hivyo mtu hawezi
kujifunga na kufanya mabadiliko bila kufuata utaratibu.
"Hatukubali
kanuni kubadilishwa badilishwa kinyemela, chochote ambacho kitaenda
kinyume cha taratibu hatutakubali, fuata kanuni, ukishafuata kanuni
tutaheshimu lakini kinyume hatutakubali," alisema.
Baada ya hapo
Sitta, alimpa nafasi Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, Jaji
Frederick Werema, ambaye kabla ya kuanza kutoa hoja zake alikumbana na
zomeazomea kiasi cha yeye kukiri kuwa hajazoea kuzomewa.
Alisema
analoliona yeye ni kuwahisha hoja bila kusoma kanuni vizuri na
kuzielewa. Alisema kanuni ya 87 fasihi ya kwanza inaeleza vizuri jinsi
ya kuzifanyia marekebisho kanuni hizo.
Mbunge wa Bunge hilo, Ismail
Jussa Ladhu, alisema inashangaza kuona kanuni ambazo hazijaanza kutumika
kasoro zake zinaanza kuonekana. "Kasoro yake yameonekana wapi?"
Alihoji?
Baada ya kumaliza kusikiliza hoja za wabunge, Sitta alisema
migogoro ya kanuni huamuliwa na Kamati ya Kanuni za Bunge. Alisema yote
yaliyosemwa yawe mazuri au mabaya anayapeleka kwenye kamati ya kanuni
za Bunge yawe mazuri au mabaya.
Hatimaye mwenyekiti aliahirisha Bunge hadi leo jioni.
0 comments:
Post a Comment