MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wakazi na watumiaji wa bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, kuchukua tahadhari stahiki kukabiliana na maafa yanayoweza kusababishwa na mvua ambazo zinaweza kunyesha kati ya jana na leo, katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA kwenye vyombo vya habari juzi, vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24 vinatarajiwa.
Maeneo yanayotajwa kuathirika na hali hiyo ni ukanda wote wa Pwani (Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).
"Hali hii inatokana na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa Mashariki mwa Bahari ya Hindi sambamba na kusogea kwa haraka kwa mfumo wa mvua za msimu (ITCZ), hivyo kuongeza kiwango cha unyevunyevu kutoka baharini kuelekea maeneo yaliyotajwa," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo wakazi na watumiaji wa bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, zinashauriwa kuchukua tahadhari stahiki.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa mvua zinazoendelea na zinazotarajiwa kunyesha zinaashiria kuanza mapema kwa mvua za masika katika baadhi ya maeneo ya pwani ya Kaskazini ikiwemo Dar es Salaam.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa inaendelea kufuatilia hali hiyo na itatoa mrejeo kila itakapobidi.
0 comments:
Post a Comment