LATEST POSTS

Thursday, March 6, 2014

'AMCHINJA' MTOTO WAKE KWA KUCHOKA KUMTIBIA


MTOTO wa miaka 12 anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Majengo wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, (jina tunalo) amenusurika kifo baada ya baba yake mzazi kujaribu kumchinja kwa madai ya kuchoshwa na gharama za kumtibu maradhi yanayomsumbua. 

Tukio hilo limetokea juzi saa 11 alfajiri katika Kijiji cha Majengo wilayani Kahama, ambapo mkazi wa kijiji hicho (jina linahifadhiwa) mwenye miaka 37 alimkamata mtoto huyo na kumchinja kwa kisu shingoni kwa lengo la kutaka kumuua.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kusudio hilo halikuweza kufanikiwa, ingawa mtoto huyo alipata majeraha sehemu ya koromeo. Mtoto huyo aliokotwa na wasamaria wema alikotupwa na baba yake akiamini ameshatimiza azma yake ya kuua.
Baada ya hapo baba yake huyo akiwa anaamini tayari ameua alijipeleka mwenyewe polisi kwa lengo la kujisalimisha.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Serikali Wilaya ya Kahama, Dkt. Joseph Fwoma, alithibitisha kufikishwa kwa mtoto huyo katika hospitali hiyo na wasamaria wema waliomuokota, huku akiwa anavuja damu nyingi shingoni kutokana na jaribio hilo la kuchinjwa.
Dkt. Fwoma alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo madaktari walimfanyia upasuaji wa haraka na kumshona sehemu ya koromeo iliyokuwa na jeraha kubwa, kisha kuongezewa damu.
Alisema hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri. Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto huyo ambaye walishatengana na mumewe kwa kipindi kirefu, (jina tunalo) alisema alishtushwa na taarifa za kuchinjwa kwa mtoto wake ambaye alikuwa akiishi naye kwa kipindi kirefu kabla ya kuchukuliwa na baba yake siku moja kabla ya tukio hilo.
“Leo asubuhi (jana) nimepigiwa simu na kuelezwa taarifa za kuchinjwa kwa mwanangu, nilishtuka sana, sikuamini kwamba juzi alimchukua kwa ajili ya kwenda kumuua, mara nyingi huwa akimchukua kwa lengo la kumtafutia matibabu," alisema na kuongeza;
“Kila alipokuwa akimchukua alikuwa akimrudisha, katika siku za hivi karibuni alikuwa akilalamika mara kwa mara akidai amechoshwa na gharama za kumtibu."
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Hata hivyo alisema inahisiwa baba wa mtoto huyo anasumbuliwa na matatizo ya akili.

0 comments: