AFRIKA Mashariki kuna mwigizaji mmoja tu. Ni msichana mweusi tii. Binti huyu ameachahistoria kule Hollywood jijini Los Angeles, Marekani alfajiri ya kuamkia Jumatatu wiki hii.
Ilikuwa kwenye tuzo kubwa za filamu za Hollywood ziitwazo Oscar 2014.
Huyu ni Lupita Amondi Nyong’o. Ni mwigizaji na prodyuza wa video za muziki. Lupita ni raia wa nchi jirani tu hapo ya Kenya.
Alishinda katika kipengele cha Muigizaji Bora Msaidizi wa Kike (Best Supporting Actress) 2014 kupitia filamu kubwa duniani iliyoingia sokoni mwaka 2013 iitwayo 12 Years a Slave.
Lupita ni Mluo, moja ya makabila ya Kenya. Anazijua vizuri mila na desturi za kabila lake. Amezaliwa kwa mama Doroth na baba Peter Nyong’o kule Mexico Machi, 1983.
Unajiuliza kama amezaliwa Mexico imekuwaje nikasema ni Mkenya? Tulia. Wakati anazaliwa baba yake alikuwa na familia nchini humo kimasomo lakini baadaye walirejea Kenya wakati bado Lupita akiwa kichanga.
Baba yake ni mwanasiasa. Aliwahi kuwa Waziri wa Afya hapo nchini Kenya na pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisumu.
Lupita ana umri wa miaka 31 tu lakini tayari amefanya makubwa na dunia sasa imemtambua.
Lupita ambaye ndiye habari ya mjini, ni mtoto wa pili katika familia ya watoto wanne.
Anazungumza Kiswahili safi, Kijaluo, Kiingereza ‘yai’ na Kihispaniola. Kuhusu shule yupo vizuri. Ameshafika chuo kikuu.
Akiwa na umri wa miaka 14, Lupita aliigiza kwa mara ya kwanza katika sinema iliyoitwaRomeo and Juliet. Prodaksheni yake ilifanyika Nairobi, Kenya chini ya Kampuni ya Phoenix Players.
Akiwa na Phoenix Players, alicheza michezo ya On The Razzle, There Goes The Bride na nyingine kibao.
Baadaye Lupita alikwenda Marekani kimasomo katika Chuo cha Hampshire Collegeakisomea shahada ya Uigizaji na Sanaa.
Alifanya kazi za uzalishaji nyuma ya kamera kwa kipindi kirefu. Hakuwa na papara. Alikuwa na ndoto. Alijua ipo siku atafika juu. Ndiyo falsafa ya maisha. Lupita anathibitisha kuwa usikate tamaa ipo siku ndoto yako itatimia.
Katika sinema alizosimamia uzalishaji na zikafanya vizuri ni pamoja na Fernando Meirelles’s The Constant Gardener, Mira Nair’s The Namesake, na Salvatore Stabile’s Where God Left His Shoes.
Mwaka 2008, Lupita alirudi nyumbani kwao Kenya. Alianza kuigiza kwenye michezo ya runingani kama Shuga uliohusu vita dhidi ya HIV/AIDS.
Mwaka 2009, alitengeza bonge moja la ‘dokyumentari’ iitwayo In My Genes iliyolenga kuanika maisha kibaguzi ya watu wenye ulimavu wa ngozi (Albino) nchini humo.
Pia aliongoza utengenezaji wa video ya ngoma ya The Little Things You Do ya Wahu aliyomshirikisha Bobi Wine iliyochaguliwa kugombea Video Bora ya MTV kwa mwaka 2009.
Lupita ameshiriki sinema nyingi za Hollywood lakini hii ya 12 Years a Slave ndiyo imethibitisha ni mkali.
Kumbuka katika Tuzo za Oscar ameshindanishwa na magwiji wa sinema wa Hollywood kama Jennifer Lawrence wa sinema nyingine kubwa duniani ya American Hustler.
Turudi kwenye usiku wa tuzo za juzi. Kilichonifurahisha kwa staa huyu aliingia ukumbini akiwa na furaha kubwa. Alionekana mwenye kujiamini mno.
Sidhani kama furaha ile ilitokana na kukumbatiana na Pharrel Willams au Angelina Joliena Brad Pitt.
Au unadhani furaha ile ilitokana na kukumbatiana na akina Lady Gaga? Hapana. Ni kujiamini kuwa si rangi nyeupe tu kama akina Nicki Minaj tu ndiyo wanaweza. Hata binti mdogo kutoka nchi ya Afrika Mashariki anaweza. Ndivyo ilivyokuwa.
Baada ya Lupita kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo alinyanyuka na akatamka kwa sauti ya juu, ‘Yeeesss’. Maana yake alijiamini kuwa anaweza kuwaburuza mastaa wa Hollywood.
Angalia alivyokumbatiwa na akina Leonardo DiCaprio. Pia Will Smith na mkewe Jade Smith. Utadhani ni mzaliwa wa New York au Miami kule Marekani. Kumbe ni raia wa Kisumu, Kenya.
Lupita amepita. Hakuna mwigizaji makini ambaye hajalisikia jina la Lupita hapa Bongo.
Kuna wale ambao walishindwa kuzuia hisia zao na kujikuta wakiandika kwenye kurasa zao ni kwa jinsi gani Lupita aliwasisimua na kutaka kufuata nyayo zake.
Asante akina Elizabeth Michael ‘Lulu’, Jokate Mwegelo mliokubali kufuata nyayo zake ili nanyi mfike Hollywood.
Ni wakati wa akina Wema Sepetu, Steven Jacob na wengine wengi wa Bongo Movies kuanza kusaka fursa kama ilivyokuwa kwa Lupita. Ishu hapa ni kujiamini kwamba nanyi mnaweza. Kuna mifano mingi ya watu weusi kuwa kwa sasa ndiyo ‘wana-ran’ dunia. Asante Lupita kwa kuitangaza Afrika Mashariki duniani.
0 comments:
Post a Comment