LATEST POSTS

Friday, March 28, 2014

Watumishi wanaofanya makosa sasa kuadhibiwa

SERIKALI imesema kuanzia sasa, watumishi wote wa umma waliobainika kufanya makosa mbalimbali katika maeneo ya kazi, wasihamishwe vituo kama ilivyokuwa ikifanyika siku za nyuma kabla ya kuchukuliwa hatua.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Saalam jana na Naibu Katibu Idara ya Utumishi wa Serikali za Mitaa, kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Bi. Rose Elipenda wakati akitoa tathmini ya uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za kinidhamu katika utumishi wa umma.
Alisema mamlaka za nidhamu katika utumishi wa umma, hawafanyi kazi yake ipasavyo katika kushughulikia suala zima la nidhamu kwa watumishi na mtumishi yoyote.
Alisema mtumishi aliyefanya makosa, haruhusiwi kuhamishwa kituo cha kazi hadi asomewe shauri lake ndipo ahamishwe ili kupunguza makosa yanayojitokeza mara kwa mara.
"Ili kupambana na makosa yanayoendelea kujitokeza kwa watumishi wa umma, tumejitahidi kufanya vikao na wadau ili kuwakumbusha wajibu wao wa kusimamia sheria, kanuni na nidhamu kwenye utumishi," alisema.
Bi. Elipenda alisema, mwaka 2010/13 walipokea mashauri ya watumishi 289 ya kuyapitia ambayo kati ya hayo, watumishi 42 walirudishwa kazini na 61 walirudishwa kwenye mamlaka ya nidhamu kwa ajili ya kujadiliwa tena.
Aliongeza kuwa mamlaka ya nidhamu zinapaswa kubadilika na kufanya kazi kwa ajili ya watumishi pamoja na itatoa ushirikiano wanaposhughulikia masuala ya nidhamu ya watumishi walio chini yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

0 comments: