Rais Jakaya Kikwete akihutubia alipokuwa akifungua mkutano wa 19 wa
mwaka wa Tafiti za sera na Maendeleo (Repoa) uliofanyika katika Hoteli
ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete amechaguliwa kuwa kiongozi
mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo barani Afrika kwa mwaka
2013.
Heshima hiyo kwa Rais Kikwete imetolewa na jarida
la kimataifa la African Leadership Magazine Group na tuzo yake
ilitarajiwa kutolewa jana jioni katika sherehe iliyopangwa kufanyika
kwenye Hoteli ya St.Regis, Washington D.C, Marekani.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema kuwa tuzo hiyo ilitarajiwa kupokewa
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kwa
niaba ya Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tuzo hiyo hutolewa kwa
viongozi wa Afrika ambao hutoa mchango mkubwa wa kiuchumi na kijamii
kila mwaka kwa watu wao, kama ilivyokuwa kwa Rais Kikwete kutokana na
mwelekeo wake wenye mafanikio kwa masuala ya utawala bora.
Taarifa hiyo ilisema kuwa jarida hilo limetambua
utawala bora chini ya uongozi wa Rais Kikwete ambao limesema umeifanya
Tanzania kuwa nchi ya kupigiwa mfano na kituo cha uhakika cha uwezeshaji
kutokana na mageuzi yaliyofanywa katika sera na mifumo ya uchumi.
Ilisema kuwa, Rais Kikwete alikuwa chaguo la
kwanza la wasomaji wa jarida hilo ambao walipiga kura kupitia njia
mbalimbali za mawasiliano za jarida hilo.
“Kuhusu maoni ya wasomaji wetu juu ya kiongozi
yupi wa Afrika ambaye ni hodari zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na
maendeleo, matokeo ya majibu ya swali hilo yamedhihirisha bila shaka
yoyote kuhusu nafasi ya Rais Kikwete katika uongozi wa nchi yake,”
taarifa ya Ikulu imelinukuu jarida hilo na kuongeza: “Ushahidi uko kila
mahali, ameweza kusimamia uchumi ambao umekuwa kwa wastani wa asilimia
saba kwa miaka yote ya uongozi wake.”
Sherehe hizo za kukabidhi tuzo zilitarajiwa
kutumiwa na jarida hilo kutangaza mafanikio ya Tanzania chini ya uongozi
wa Rais Kikwete kwa jumuia ya kimataifa, taasisi za kibiashara na kwa
wanadiplomasia.
0 comments:
Post a Comment