LATEST POSTS

Wednesday, April 2, 2014

Mtoto aokoa maisha ya mama yake

MTOTO mwenye umri wa miaka miwili nchini Uingereza, Riley Ward amepokea sifa kedekede kwa kuokoa maisha ya mama yake kwa kupiga nambari ya simu 999 kwa kile kilichoelezwa kuwa mama yake alikuwa amezimia.

Kwa mujibu wa BBC, wahudumu wa afya katika kituo cha kupokea simu za dharura nchini Uingereza walisema kuwa walipokea simu ya mtoto mdogo aliyewaambia kuwa ''Mama amelala''.

Wahudumu hao walifanikiwa kwenda nyumbani kwa mtoto huyo katika mtaa Leicestershire na kumpa huduma ya kwanza mama wa mtoto huyo na kisha kumpeleka hospitalini moja kwa moja.

Walimfanyia upasuaji wa dharura baada ya kupatikana na damu iliyokuwa imeganda kichwani huku akivuja damu nyingine kutoka katika kizazi chake.

Mtoto huyo Riley Ward amezawadiwa kutokana na kitendo chake cha ujasiri na wahudumu hao waliosema kuwa huyo ndiye mtoto mchanga kabisa kuwahi kupiga simu kituoni humo.

Mama yake, Dana Henry, alimtaja mwanawe kama shujaa wake kutokana na tukio hilo, Dana (27) alishtushwa sana na kitendo cha mtoto wake aliyekuwa na uwezo wa kupiga simu.

Pia alisema kuwa ameweza kuwafundisha watoto wake wadogo namna ya kupiga simu ya dharura ikiwa yeye na mumewe hawahisi vizuri.

0 comments: