HATIMAYE Mtoto, Hamisi Hashimu Liguya (13) mkazi wa Yombo jijini Dar
amerejea nchini kutoka India alikopelekwa kwa matibabu akiwa na
tabasamu akiamini kwamba, Mungu amemtendea miujiza, Risasi Mchanganyiko
lina habari kamili.
Hamisi aliyekuwa akisumbuliwa na uvimbe mkubwa wa mguu wa kushoto
kiasi cha kushindwa kutembea na kuishia kutambaa amerejea akiwa na
matumaini ya kutimiza ndoto zake.
Mtoto huyo alipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Ganga, Tamil Nadu,
India ametua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNI) jijini
Dar mwishoni mwa wiki iliyopita akiambatana na baba yake mzazi, Hashim
Liguya.
Daktari wa hospitalia hiyo, Raja Sabapathy kwa niaba ya madaktari
wenzake amemwandikia mmoja wa waandishi wetu barua pepe akifurahia
kitendo cha Hamisi kutembea ingawaje kwa msaada wa magongo.
“Uwezekano wa Hamisi kupona ulikuwa mdogo, lakini Mungu ametenda
miujiza, baada ya kuukata mguu wake na kumtengenezea wa bandia,
tulifurahi kuona ameuumudu vyema mguu huo,” aliandika Dk. Sabapathy.
Daktari huyo aliongeza kuwa, Hamisi
amekuwa na furaha baada ya kumuondolea uvimbe wa kilo tano katika mguu
wake na kusisitiza kuwa mtoto huyo anahitaji mazoezi ya kila siku ili
kuuzoea mguu wake wa bandia.
Mara baada ya kutua uwanja wa ndege, Hamisi alisema kuwa
ameyafurahia matibabu aliyoyapata India, kwani hakutegemea kama angeweza
kwenda na kurudi akiwa anatembea na kuwa na matumaini mapya.
“ Nimefurahi sana, naamini sasa nitaweza kutimiza ndoto zangu kwa
kuwa, naweza kutembea,” alisema Hamisi huku akiwashukuru Watanzania kwa
misaada waliyopitia kupitia Global Publishers na Mtangazaji Hoyce Temu.
Baba mzazi wa mtoto huyo alitoa shukrani zake za dhati kwa Watanzania
wote waliojitolea kumchangia mtoto wake na kusema kuwa hana cha
kuwalipa zaidi ya kuwaombea dua na kuwataka waendelee na moyo huohuo kwa
watu wengine.
“ Furaha yangu imezidi kikomo, sikuwa na matumaini ya kumuona
mwanangu akitembea tena, nawashukuru Watanzania kwa wema wao,” alisema
baba huyo.
Watanzania waliitikia wito wa kumchangia fedha Hamisi baada ya
kuhamasishwa na Kampuni ya Global Publishers wachapishaji wa Magazeti
Pendwa Tanzania na Mtangazaji wa Kipindi cha Mimi na Tanzania, Hoyce
Temu.
Pia, hamasa nyingine zilitoka kwa Kikundi cha Mkono kwa Mkono ambacho kilionesha jitihada za kumsaidia Hamisi.
Hamisi aliondoka Tanzania, Februari 28, mwaka huu kwenda India kwa ajili ya matibabu hayo akiwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao kitaalam unajulikana kwa jina la plexiform neurofibromatusis.
Hamisi aliondoka Tanzania, Februari 28, mwaka huu kwenda India kwa ajili ya matibabu hayo akiwa anasumbuliwa na ugonjwa ambao kitaalam unajulikana kwa jina la plexiform neurofibromatusis.
0 comments:
Post a Comment