LATEST POSTS

Tuesday, April 1, 2014

Wachina waliokata rufaa na kuachiwa, washtakiwa tena

RAIA wawili wa China ambao walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuachiwa huru baada ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa nchini na kushinda, jana walirudishwa tena kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao walisomewa mashtaka matatu likiwemo la kuvua samaki katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Hindi, eneo la Tanzania bila kuwa na kibali.
Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni nahodha wa meli ya Tawaliq 1, Hsu Chin Tai na wakala wa meli hiyo, Zhao Hanguing.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Waliarwande Lema, wakili Mwangamila, alidai shtaka la kwanza linawahusu washtakiwa wote.
Alisema inadaiwa kati ya Januari 10, 2009 na Machi 10 mwaka huo, washtakiwa walikutwa wakivua samaki katika ukanda huo bila kuwa na kibali.
Shtaka la pili linamhusu mshtakiwa wa pili, Hanguing ambaye inadaiwa kati ya Januari 10, 2009 na Machi 8 mwaka huo, aliharibu mazingira kwa kutupa uchafu kwenye maji katika ukanda huo.
Katika shtaka la tatu, pia linamuhusu Hanguing ikidaiwa kati ya Machi 8 na 11, 2009, alimsaidia mshtakiwa wa kwanza kufanya shughuli za uvuvi Tanzania bila kibali, kukwepa kosa na adhabu.
Februari 23,2012 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliwahukumu washtakiwa hao kifungo cha miaka 30 jela au kulipa faini ya sh. bilioni 22 ambapo washtakiwa hao walikata rufaa Mahakama ya Rufaa na kuachiwa huru mwishoni mwa wiki.
Washtakiwa hao walishinda rufaa hiyo baada ya Jopo la Majaji watatu akiwemo, Salum Masati na Semistocles Kaijage kusema kuwa, Mahakama imebaini kesi hiyo ilifunguliwa bila kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). Kesi hiyo imepangwa kuitwa tena Aprili 14 mwaka huu

0 comments: