LATEST POSTS

Tuesday, April 1, 2014

Majangili sita mbaroni na SMG

MAJANGILI sita wamekamatwa katika Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida wakiwa na silaha ya kivita aina ya SMG, meno 53 ya tembo yenye kilo 169.7 na magazini tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu, watu hao walikamatwa juzi katika Kijiji cha Kiombo Wilayani Singida.
Alisema meno yaliyokamatwa ni sawa na tembo 26 ambao wameuawa na majangili katika Hifadhi za Rungwa na Kizigo
Aliongeza kuwa, pamoja na changamoto kubwa iliyopo dhidi ya ujangili, Serikali imeazimia kuwasaka, kuwakamata majangili na washirika wao popote walipo usiku na mchana.
"Msako unaendelea ili kuwasaka wauaji wa tembo hawa hivyo nawaomba wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu, zitoeni kwa Jeshi la Polisi, vyombo vya usalama na askari wanyamapori.
Alimpongeza Mkurugenzi wa Wanyamapori na kikosi chake cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kati Manyoni na kikosi kazi maalumu kwa kujituma zaidi na kufanikisha kukamatwa majangili hao, meno ya tembo na silaha.

0 comments: