LATEST POSTS

Tuesday, April 1, 2014

Mtumbwi wazama, 7 wapotea

MTU mmoja amefariki dunia na wengine saba hawajulikani walipo baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia kuvuka Mto Rufiji, kupinduka na kuzama majini.
Tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku katika Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani baada ya mtumbwi huo kugonga kivuko kilichokuwa majini ambapo ajali hiyo ilichangiwa na mto huo kujaa maji.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani humo,
ACP Ulrich Matei, alisema jeshi hilo linamshikilia nahodha wa mtumbwi huo kwa uchunguzi zaidi.
Alisema ajali hiyo ilitokana na mto huo kujaa maji kupita kiasi pamoja na mtumbwi huo kubeba watu wengi kuliko uwezo wake jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.
Aliongeza kuwa, mtumbwi huo ulipakia watu 16 ambao kati ya hao, saba hawajulikani walipo wengi wao wakiwa watoto na ambapo hadi sasa, maiti ya mtu mmoja imepatikana.
"Nawaomba wakazi wa Mkoa wa Pwani katika kipindi hiki, wasitumie Barabara ya Msata- Bagamoyo kutokana na hali ya mvua inayoendelea kunyesha," alisema Kamanda Matei.
Alisema maji yamejaa kila sehemu ikiwemo baharini na kwenye mito hivyo ni vyema wananchi wakawa makini kutokana na hali hiyo ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Akihojiwa na Kituo cha Radio One, Mkuu wa Wilaya hiyo, Nurdin Babu, alisema jitihada za kuwatafuta watu wengine waliopotea zinaendelea kufanyika kwa kutumia boti.
"Tumewataka wananchi wasiuvuke mto huu kwenda mashambani kwa sababu umejaa maji, watu wengine ambao wamenusurika wameruhusiwa kurudi nyumbani," alisema.

0 comments: