ALIYEKUWA Hakimu wa Wilaya ya Urambo, Oscar Bulugu, aliyekuwa
akikabiliwa na mashitaka matatu ya kuomba na kupokea rushwa,
amehukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja na nusu au kutumikia
kifungo cha miaka mitatu jela.
Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa
Shinyanga, Massele Chaba, baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa
mashitaka.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa mbili, Hakimu Chaba, alisema
kuwa analazimishwa na matakwa ya sheria kutoa adhabu hiyo kwa
mshitakiwa aliyetiwa hatiani, na ikiwa hajaridhika anaruhusiwa kukata
rufaa.
Bulugu, alifikishwa mahakamani hapo mwaka jana na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa, akikabiliwa na mashitaka matatu, moja la kuomba
rushwa na mengine mawili ya kupokea rushwa.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mabula Mapalala ulidai kuwa
mtuhumiwa alitenda makosa hayo kati ya Machi 15 na 22 mwaka jana akiwa
ni hakimu mkazi wa Wilaya ya Urambo.
Ilidaiwa kuwa Machi 15 mtuhumiwa akiwa ni hakimu wa Mahakama ya
Wilaya ya Urambo, alimshawishi Lucas Raymond Changala ampe sh milioni
tano ili ampe dhamana ndugu yake aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya wizi
wa fedha za benki ya NMB.
Mapalala alidai katika shitaka la pili, Machi mtuhumiwa alipokea sh
milioni moja kutoka kwa Changala kama malipo ya awali ili ampe dhamana
Phillipo Raymond aliyekuwa mtumishi wa benki ya NMB anayetuhumiwa
kuiba zaidi ya sh. milioni 100.
Katika shitaka la tatu, mwanasheria huyo wa Takukuru alidai kuwa
Machi 21 mtuhumiwa huyo alipokea tena sh. milioni moja ikiwa ni
muendelezo wa malipo aliyoomba ili ampe dhamana mtumishi huyo wa NMB.
Upande wa mashitaka uliiomba mahakama impatie adhabu kali mtuhumiwa
ili iwe fundisho kwakuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya
rushwa hasa vinavyofanywa na watumishi wa umma.
Akijitetea, Bulugu aliiomba mahakama isimpatie adhabu kubwa kwa vile
ni kosa la kwanza na anategemewa na zaidi ya watu 10 ikiwemo wazazi
wake.
Baada ya utetezi huo, hakimu aliyesikiliza shauri hilo, alimhukumu
kulipa faini ya shilingi laki tano kwa kila kosa au kutumikia kifungo
cha miaka mitatu kwa kila kosa na adhabu hiyo ya kifungo itakwenda
pamoja.
0 comments:
Post a Comment