RAIS Jakaya Kikwete amesema ni mkusanyiko wa upuuzi kudai kuwa
alishiriki kumwokoa mtoto wake, Ridhiwani, aliyedaiwa kukamatwa na dawa
za kulevya nje ya nchi.
Alisema urais ni taasisi kubwa nchini na hivyo hawezi kujiingiza
katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo baadhi yao wanamsukuma
ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.
“This is nonsense (huu ni ujinga), na ni mkusanyiko wa upuuzi, sina
muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna
hiyo,” alisema Kikwete wakati alipokuwa akizungumza na Watanzania
waishio Marekani alipokutana nao Agosti 2, mwaka huu mjini Washington
D.C.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa nchini
Marekani, alisema hayo wakati akijibu maswali kuhusu madai yaliyotolewa
Julai Mosi mwaka juzi, na Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
“Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa
kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na
watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda
yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya
Watanzania,” aliongeza.
Pia alipoulizwa kuhusu kutiliana saini mikataba 12 na uongozi wa
Jamhuri ya Watu wa China, ikiwa kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa
Ridhiwani, Rais Kikwete alikanusha vikali kwa kusema hawezi kufikia
suala kama hili kwani kufanya hivyo ni kuiweka nchi rehani.
“Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria kuiweka
rehani, haya ni maneno ya kipuuzi tu, yenye kutafuta kututoa kwenye
ajenda zetu nzuri, hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye
mambo ya maana ya kuleta mabadikio katika ustawi wa Watanzania,”
alisisitiza.
Mwaka jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa alipokuwa akihutubia
mkutano wa hadhara katika mji wa Sikonge mkoani Tabora, alisema kuwa
alipata taarifa ya uhakika kutoka China kuwa vijana wenye asili ya
Afrika walikamatwa katika uwanja wa ndege wa Hong Kong, wakiwa na dawa
za kulevya zenye thamani ya sh. bilioni 4.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa alisema mkuu wa kitengo cha dawa za
kulevya katika uwanja huo alitaja majina ya vijana hao, likiwemo jina la
kijana anayedaiwa kuwa wa kigogo katika Serikali ya Rais Kikwete.
Alisema anamtaka Rais Kikwete akanushe uvumi huo kwa kuwa habari
zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinaihusisha serikali yake.
0 comments:
Post a Comment