LATEST POSTS

Sunday, September 14, 2014

Chadema kumpata mwenyekiti leo

  Freeman Mbowe.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo kinafanya uchaguzi mkuu wa kumpata mwenyekiti na makamu wenyeviti wake watakaokiongoza chama hicho kwa miaka mitano ijayo huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa mwanasiasa mkongwe wa nchini Kenya, Raila Odinga.
Mchuano katika nafasi ya uenyekiti ilitarajiwa kuwa kati ya mwenyekiti anayemaliza muda wake, Freeman Mbowe na aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Tabora wa chama hicho, Kansa Mbarouk ambaye jana alitangaza kujitoa katika kinyang’anyiro.
Hivyo kujitoa kwa Mbarouk kuna maanisha kwamba nafasi hiyo imebakisha wagombea watatu watakaochuana kuwania kiti hicho ambao ni Daniel Luvanga na Gambaranyera Mongateo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa akizungumzia maandalizi ya Mkutano Mkuu wa chama hicho alisema kila kitu kinakwenda sawa ikiwa ni pamoja na vikao vya Kamati Kuu na Baraza Kuu ili kuandaa ajenda na kupitia majina ya walioomba kuteuliwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Gazeti hili lilikuwapo katika ukumbi wa Mlimani City jijini hapa na kushuhudia wajumbe wakiendelea kujiandikisha huku Kamati Kuu ikiendelea na mkutano wake kisha Baraza Kuu ikiwa ni kuweka kila kitu katika hali ya ufanisi.
Katika uchaguzi huo kundi ambalo linatarajiwa kuwa na ushindani ni la kuwania ujumbe wa kamati kuu ambapo hadi jana waliokuwa wameomba kuteuliwa kuwania kuingia katika chombo hicho kikubwa cha uamuzi walikuwa ni 58 kati ya nafasi hizo sita za Tanzania Bara na mbili Zanzibar, huku wajumbe wake watachaguliwa kwa uwiano sawa wa kijinsia.
Mbarouk akitangaza kujitoa katika kinyang’anyiro hicho alisema hawezi kuwa miongoni mwa wanachama wanaoikiuka na kuivunja katiba ya chama.
“Viongozi wetu wamekiuka katika ya chama, nilimwekea pingamizi Mbowe kutokana na kutokuwa na sifa za kugombea kwani ameongoza kwa miaka kumi jambo ambalo halimlazimu kuendelea tena,” alisema Mbarouk na kuongeza:
“Hatua nitakazochukua nitakwenda kwa msajili kuomba ufafanuzi wa kifungu cha 6.3.2 C kuhusu ukomo wa uongozi”.
na hapo ndipo tutaona jinsi uongozi utakaopatikana utakuwa hautambuliki.”
Mbarouk alisema Chadema ni chama makini, kinachojiandaa kushika dalo hivyo viongozi wake wanatakiwa kuheshimu misingi ya katiba ya chama na si kutumia ubabe na ndiyo sababu iliyomfanya kujitoa.
Katiba barua yake kwenda kwa Katibu Mkuu, Dk Slaa ambaye alikiri kuipokea jana saa5.20 asubuhi Mbarouk alihitimisha kwa kusema “Kwa mazingira haya sioni uwezekano wa kutendewa haki kwani mazingira ya uchaguzi huru na haki hayapo.”

Aliongeza: “Nitaendelea kuwa mwanachama wa Chadema na wala sifikirii kukihama kama watu wanavyodai, nimeshiriki katika harakati mbalimbali kukijenga chama hivyo nitakipigania muda wote na pindi nikiona mambo hayaendi sawa nitasema bila woga.”
Uchaguzi katika Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee umekamilika juzi kwa Halima Mdee kuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Paschal Pabrobas mwenyekiti Baraza la Vijana (Bavicha) na Hashim Juma Issa akiibuka mwenyekiti wa Baraza la Wazee.

0 comments: