Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba, amesema anashangazwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la
Katiba, Samuel Sitta kung’ang’ania kuendelea na Bunge hilo licha ya Rais
Jakaya Kikwete kuridhia lifikie kikomo Oktoba 4 mwaka huu.
Hivi karibuni, Rais Kikwete alikutana na viongozi
wa vyama vya siasa vilivyo chini ya Kituo cha Demokrasia (TCD) na
kukubaliana kusitisha mchakato wa Katiba hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa
2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu wiki hii
jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba alisema ameshangazwa na uongozi wa
Bunge Maalumu la Katiba kuendelea na vikao wakati uwezekano wa
kukamilisha mchakato haupo.
“Hivi kuna haraka gani ya kuwa na rasimu katika
Bunge hili? Mimi nilivyoelewa makubaliano ya Rais na TCD ni kama
walikuwa wanasema kwa ustaarabu hebu twende polepole. Nimeambiwa kuwa
Rais alitoa muda mpaka Oktoba 4, lakini uongozi wa Bunge ukapanga mpaka
mwisho wa Oktoba,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Mimi nafikiri makubaliano kati ya Rais na
viongozi wa vyama ni kukataa kuongeza muda. Hiyo kwangu ni lugha ya
kistaarabu kwa Bunge kwamba hamwezi kumaliza kazi hii kwa kipindi hiki,”
alisema Jaji Warioba.
Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Sitta kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa kuhusu
Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume yake, badala ya kujihami.
“Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini
nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate maoni ya watu ya kila aina.
Kuna wale ambao watakusifu na wengine watakusema vibaya. Nilisemwa mengi
sana. Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu
mmoja mmoja,” alisema na kuongeza:
“Sitta asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri kuwa hana kasoro.”
Aliongeza: “Nashangaa sana mambo yanavyoendelea
kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii tena. Ni wakati fulani mtu
anaweza kunipigia simu, hebu angalia wanavyosema....”
Alisema hatua ya uongozi wa Bunge kung’ang’ania kuendelea na mchakato ni kupingana na Rais Kikwete.
“Lakini mimi inanishangaza ilikuwaje Rais anatoa
nyongeza ya hadi Oktoba 4, uongozi wa Bunge unaongeza hadi mwisho wa
mwezi? Rais anasema hivi na Bunge linasema hivi. Mimi naomba uongozi wa
Bunge utafakari tena,” alisema na kuongeza:
“Kinachofanywa na uongozi wa Bunge la Katiba hakina shinikizo la CCM , bali ni uamuzi ambao unatokana na matakwa yao.
“Kama ni makubaliano ya viongozi wa vyama vya siasa na CCM
walikuwapo, sasa kama chama kimeona hatuwezi kupata Katiba bora kwa nini
tena uendelee?”
“Sheria ilisema Bunge lile litapewa siku 70,
lisipomaliza litapewa nyingine 20, wakafanya tafsiri zao, kwani hizo
siku 90 hazijaisha? Walipofikia wakati wakasema sasa tunakutana na Bunge
la Bajeti tuahirishe, wakaahirisha. Kama mara ya kwanza liliwafanya
wasitishe, nini kinawazuia kwa sasa?”
Alisema mbali ya tamko hilo, uongozi wa Bunge hilo
umetangaza kuendelea na mchakato wakisema kuwa rasimu itakuwa tayari
mwisho wa mwezi huu.
“Nasikia wanaendelea, nasikia wanasema rasimu
itakuwa tayari mwisho wa mwezi huu. Hivi katika hali hii wanaweza?”
alihoji Jaji Warioba huku akionyesha sura ya mshangao.
Warioba ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu katika
serikali ya awamu ya pili ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alisema
ahadi iliyotolewa na Sitta ya kupatikana kwa rasimu ndani ya Septemba
haitekelezeki.
“Sina tatizo na kuahirisha Bunge Maalumu la
Katiba, kwa kuwa waliona haiwezekani kupata Katiba kabla ya uchaguzi,
lakini sioni uwezekano wa kumaliza kazi zote kwa wakati huu,” alisema na
kuongeza:
“Sioni kama wana muda wa kamati kuandika rasimu
mpya ya kupigia kura, kwa sababu suala siyo kupiga kura tu, kuna mambo
ambayo lazima kuwe na maridhiano na itachukua muda.”
Akitoa mfano wa suala la Muungano, Warioba alisema
ni kati ya mambo yanayohitaji maridhiano badala ya kuishia kwenye
kupiga kura tu.
“Kwa mfano suala la muungano halitakwisha hivihivi
bila maridhiano. Kuna mengine, nimesikia wanajadili Mahakama ya Kadhi,
limejitokeza sana. Litakapofika kwenye uamuzi, lazima kuwe na
maridhiano. Wasipokuwa na maridhiano inawezekana wakaleta rasimu ambayo
haina Mahakama ya Kadhi. Je, wale wanaoitaka wakikataa una uhakika wa
kupata theluthi mbili? Wale wanaopinga wakikubali utapata theluthi
mbili?” alihoji.
Kupiga kura
Akizungumzia kauli ya Sitta ya kuwasiliana na
balozi za nje ili kuhakikisha wajumbe waliosafiri huko wapige kura
hukohuko, Warioba alisema kupiga kura peke yake hakutoshi kutoa uhalali
wa Katiba bali maridhiano ndiyo msingi.
Aliongeza: “Mimi sielewi uongozi wa Bunge unafanya
nini! Kwa sababu ukipitisha kitu kwa siri, hata kabla ya kufika kwenye
kura ya maoni kikakataliwa na wananchi. Ni vizuri kutulia na
kushauriana, wasiwe na haraka.”
Amewashauri viongozi wa Bunge hilo kutafakari upya uamuzi wa kuendelea na vikao wakati Rais ameonyesha nia ya kuvisitisha.
Misimamo ya vyama imeharibu
Akieleza sababu za Bunge hilo kuyumba, Jaji
Warioba alisema licha ya Tume yake kuwapa viongozi wa vyama vya siasa na
wajumbe wengine nyaraka 10, lakini wameingiza misimamo ya vyama vyao:
“Mchakato ulipoanza kwa wale ambao tulikabidhiwa
kazi hii, tuliamini tunaelekea kupata Katiba bora itakayotokana na maoni
ya wananchi. Sisi kwenye Tume hilo ndilo lilikuwa lengo letu.
Tulijipanga tulivyoweza mpaka tukatoa rasimu ambayo kwa kiwango kikubwa
ilizingatia maoni ya wananchi,” alisema.
Jaji Warioba alisema mwanzo wa Bunge waliamini
kuwa maoni ya wananchi yatazingatiwa, lakini baadaye walishangaa kuona
maoni ya vyama ndiyo yanazingatiwa badala ya wananchi.
“Lazima nikiri kwamba mwanzo wa Bunge hilo haukuwa
mzuri. Sisi tuliamini kwamba chochote kinachokuja kitaangalia
tulichofanya kwa msingi wa kuona wananchi wamesema nini….
“Lakini walivyoanza ikabidilika kabisa ikawa ni
kwa msimamo wa vyama. Tukatoka kwenye msingi wa maoni ya wananchi
tukaingia kwenye maoni ya vyama.”
Aliendelea kusisitza kuwa misimamo ya vyama ndiyo
imeua matumaini ya kupata Katiba Mpya licha ya Tume hiyo kutoa nyaraka
10 za randama zinazoonyesha maoni ya wananchi na sababu ya mapendekezo
ya rasimu hiyo.
“Nimewasikiliza kwa kirefu wajumbe wa Bunge la
Katiba, inaonekana wengi hawakusoma taarifa tulizowapelekea.
Tuliwapelekea nyaraka 10. Tuliwapelekea Rasimu, Randama inayoelezea kila
ibara, maoni ya wananchi kisha sababu za mapendekezo,” alisema na
kuongeza:
“Baada ya hapo kuna vitabu vikubwa viwili
vinavyoeleza maoni ya wananchi. Kuna kitabu kingine cha maoni ya
mabaraza. Kuna kile cha takwimu na kitabu cha utafiti. Sasa pamoja na
vitabu vyote hivyo, bado watu wanazungumza bila kuzingatia
yaliyoandikwa.”
Alisisitiza kuwa wajumbe wengi hawakusoma vitabu hivyo kwa sababu walikwenda bungeni na misimamo ya vyama vyao.
“CCM wana misimamo yao, Chadema yao, CUF na NCCR-Mageuzi nao wana yao.”
Kufutwa kwa vipengele muhimu
Kufutwa kwa vipengele muhimu
Akizungumzia kuhusu kuondolewa kwa mambo muhimu
katika rasimu hiyo ya Katiba, Warioba alisema hali hiyo inatishia
kupatikana kwa Katiba Mpya kama ilivyokusudiwa.
Alisema baada ya kuondolewa kwa vipengele muhimu
katika Rasimu ya Katiba ni wazi kwamba Katiba itakayopatikana haitakuwa
tofauti na iliyopo sasa.
“Katiba Mpya siyo kuandika waraka mpya, ni kuona
kuna tofauti gani kati ya katiba hiyo na ile ya zamani. Kuna maeneo
fulani ambayo ndiyo yaliyofanyiwa mabadiliko. Lakini kutokana na mambo
yanavyokwenda yale mabadiliko makubwa hayapo tena,” alisema.
Aliyataja maeneo makubwa yaliyobadilishwa katika
rasimu hiyo ni suala la maadili akisema kuwa wananchi walisisitiza
kuporomoka kwake na kupendekeza njia za kudhibiti.
“Wananchi walikuwa wanataka lazima tuwe na
mwongozo kwenye Katiba utakaowezesha kujenga utamaduni na maadili. Kwa
hiyo katika rasimu tukaona kwenye utangulizi unaobeba misingi mikuu ya
utaifa. Tukaona lazima kuimarisha misingi mikuu,” alisema.
Alisema katiba ya sasa inasema misingi mikuu ni uhuru, haki, udugu na amani na kwamba wananchi walitaka yaimarishwe hayo.
Jaji Warioba alisema wananchi walisema huwezi
kuzungumzia haki bila usawa, huwezi kuzungumzia amani bila umoja na
katika umoja lazima kuwe na mshikamano.
“Lakini wakasema msingi wa kwanza ni utu, kwa hiyo
Tume ikazingatia misingi yote ya utu na maadili ikafika misingi minane
badala ya minne.”
Alisema eneo lingine lililofanyiwa mabadiliko ni
tunu ya taifa, akieleza kuwa wananchi walitaka ziwekwe kwenye Katiba
kutokana na maelezo kwamba ndizo zinazojenga utamaduni wa Taifa.
Maadili ya Viongozi
Kuhusu maadili kwa viongozi, alisema
walipendekeza, madaraka ya viongozi yawe ni dhamana, hivyo yawekewe
kanuni, lakini Bunge badala ya kuheshimu maoni ya wananchi yamefanyiwa
mabadiliko.
Alisema Tume yake iliangalia sheria ya maadili wakaona haina nguvu sana na inategemea kiongozi mmoja.
Jaji Warioba alitoa mfano wa nchi ambazo hazikuwa
na maadili ya viongozi madhubuti na kujikuta zipo katika matatizo
makubwa kuwa ni Ufilipino.
Alisema katika nchi hiyo maadili ya viongozi
yalikuwa yameshuka sana, rushwa imezidi, hivyo walipomwondoa madarakani
rais wa nchi hiyo, Ferdnand Marcos, maadili ya viongozi wakayaweka
kwenye katiba.
Alitaja nchi nyingine ambazo zimeweka maadili ya viongozi kwenye katiba ni Afrika Kusini, Namibia na Kenya.
Aliendelea kusema kuwa hata zawadi wanazopewa
viongozi zinapaswa kuwa za Taifa ili kuepusha kuchanganya masilahi ya
Taifa na masilahi yao binafsi hasa pale viongozi wanapopewa zawadi
wakati wa kutia saini kwenye mikataba ya Serikali.
“Kwanza wananchi walisema zawadi anayopewa
kiongozi inakuwa ni mali ya Taifa. Wakasema viongozi wanaingia mikataba
na wanajifikiria wenyewe.
Pili, katika kuimarisha maadili kwa viongozi Tume ilipendekeza kiongozi asiwe na akaunti nje kinyume cha sheria.
Tatu, iwe ni wajibu wa kiongozi kutangaza mali
zake, kiongozi lazima atofautishe kati ya masilahi yake na masilahi ya
umma, na kiongozi aepuke kutumia mali ya umma kwa masiahi yake.
Hata hivyo, alisema mwelekeo wa Katiba Mpya umebadilika hasa baada ya mambo hayo kuondolewa na kuyafanya kuwa sheria za kawaida.
“Wenzetu yaliwashinda wakayaweka kwenye katiba,
sisi tunayaondoa. Nimeshangaa hata waliposema uwazi na uwajibikaji siyo
tunu. Lakini katika nchi yoyote lazima uzingatie uwazi na uwajibikaji
ili kuepuka ufisadi na wizi,” alisema.
Kuhusu madaraka ya wananchi katika Katiba
alifafanua haja ya wananchi kuwawajibisha viongozi wao wakiwamo wabunge
akisema kuwa mamlaka hayo yameporwa na kupewa vyama vya siasa.
“Wananchi walisema sisi ndiyo wenye madaraka ya
katiba, sasa tunataka mbunge wetu asiwe waziri. Pili tunataka ubunge uwe
na kikomo.
“Uchaguzi siku hizi siyo kitu ni kama mnada tu. Walisema kama
mbunge ameshindwa tuwe na madaraka ya kumwondoa hata kama muda
haujafika, kwa sasa hawawezi kuwaondoa kwa sababu ya rushwa,” alisema na
kuongeza:
“Lakini wamesema haiwezekani kumwondoa mbunge na
watu watafanya mbinu za kuwaondoa wabunge. Lakini vyama vya siasa
vimepewa mamlaka ya kuwaondoa wabunge na vimefanya hivyo. Wananchi
wanaomchagua wanasema italeta matatizo.”
Kuhusu wabunge kutokuwa mawaziri, alisema
walifanya utafiti na kuona ugumu wa kutenganisha madaraka ya Serikali na
madaraka ya Bunge kwa sababu Serikali iko ndani ya Bunge.
Alisema kwa mabadiliko waliyopendekeza wao rais
aondolewe bungeni abaki kuwa mtendaji na amiri jeshi mkuu na mawaziri
wake wasiwe wabunge.
Alisema hata hivyo mapendekezo hayo yamekataliwa
kwa madai kuwa mfumo wa sasa waliouzoea ni wa kibunge ambao Waziri Mkuu
anakuwa mbunge na anakaa bungeni.
“Kuna nchi zenye mfumo huo kama vile Uingereza,
Canada, Australia, ni nchi za Jumuiya ya Madola, mkuu wa nchi siyo
mtendaji mkuu, bali waziri mkuu ndiyo anakuwa mbunge. Lakini hapa
unakuwa na rais katika Bunge ambaye haingii bungeni. Kunakuwa na
mkanganyiko,” alisema na kuongeza:
“Kinachofanyika ni Serikali inalibana Bunge ama Bunge linaingia katika mambo ya Serikali,” alisema.
Muungano
Kuhusu suala la muungano alisema Bunge la Katiba
limekuwa likijadili udhaifu wa Serikali tatu badala ya kuangalia udhaifu
wa Serikali mbili, huku wakipanga kupunguza mambo ya muungano.
“Sasa hivi nasikia wanataka kuondoa mambo mengi
zaidi ya muungano. Sisi tuliyaondoa kwa kuwa na Serikali tatu. Lakini
kwa sasa watayaondoa bila kuweka utaratibu,” alisema na kuongeza:
“Serikali ya muungano inashughulikia tu mambo ya
Bara. Huoni Waziri wa muungano akivuka maji na kwenda kufanya kazi
Zanzibar. Hiyo imeleta matatizo makubwa. Kwa kuwa Serikali ya Muungano
inashughulikia zaidi mambo ya Bara,” alisema.
Alitoa mfano wa mikopo akisema kuwa Zanzibar
haiwezi kukopa kwa kuwa haitambuliki kama nchi kimataifa bali ni lazima
ije bara na ipate dhamana.
Huku akitoa mifano ya dira na mikakati ya maendeleo, Warioba aliendelea kufafanua kasoro za muungano.
“Chukua mfano wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025
ni ya Bara maana Zanzibar wao wana Dira ya Maendeleo ya 2020. Mikakati
ya maendeleo kama Mkukuta ni wa Bara, Zanzibar kuna Mkuza. Kama ni
hivyo, Wazanzibari wanakuja Bara kufanya nini? Kwa nini wanakuja
kushiriki katika maamuzi ya bara? Hilo limekuwa ni tatizo la kisiasa na
yamekuwapo malalamiko ya muda mrefu.”
Aliongeza suala la kuwapo kwa migongano ya Katiba
ya Muungano na ile ya Zanzibar huku moja ikisema nchi ni moja na
nyingine ikisema nchi mbili zilizoungana.
Jaji Warioba alisema kutokana na mabadiliko muhimu
yaliyopendekezwa na Tume yao kuondolewa, huenda kukawa na Katiba yenye
mabadiliko kidogo.
“Wamechukulia yale mambo ya uongozi tu, uwe na
muundo mpya wa Tume ya uchaguzi, uchaguzi wa rais, Rais achaguliwe kwa
asilimia 50 na zaidi, uchaguzi wa rais unaweza kuhojiwa mahakamani.
Lakini yale ya wananchi yameachwa.
Haki za binadamu
Kuhusu haki za binadamu, Warioba alisema kuwa
wananchi walitaka vikwazo vilivyokuwapo viondolewe, hivyo tume ilifanya
marekebisho ikiwamo kuweka mgombea binafsi.
Baada ya uchaguzi Katiba itapatikana?
Kuhusu suala la kuahirisha mchakato hadi baada ya
Uchaguzi Mkuu wa 2015, Jaji Warioba alisema rais ajaye atalazimika
kufuata sheria ya Mabadiliko ya Katiba ili kumalizia mchakato huo.
“Sheria ipo, sidhani kwamba akija atapingana nayo.
Tumekusanya maoni, tumekwenda bungeni na tunangoja kura za maoni, kwa
nini avunje sheria? Labda kwa kuwa sheria inasema wajumbe wa Bunge la
Katiba ni pamoja na wabunge wa muungano, sasa kama hawakurudi sijui
atafanyaje? Je, waendelee hao hao au wateuliwe wengine?” Alihoji.
Ardhi na Maliasili
Jaji Warioba pia ameshangazwa na Bunge hilo
kuingiza masuala ya ardhi, maliasili na Serikali za Mitaa kwa siri
akisema huko ni kuvuruga mchakato.
Alisema mambo hayo si ya Muungano na yanahitaji na yalipaswa kutolewa hadharani ili wananchi waone kwanza.
“Kuna mambo ambayo Bunge limeyafanya kwa siri.
Wameingiza sura mpya kwenye rasimu, kuhusu ardhi na maliasili na
Serikali za Mitaa,” alisema .
Alisema kuziingiza kwenye rasimu lazima muwe na
uhakika kwamba yatatumika pande zote, na kwamba bara wana utaratibu wao
wa Serikali za Mitaa na Zanzibar wana utaratibu wao wa ardhi na
maliasili ambao ni tofauti kabisa na ule wa Bara.
Alisema kuweka kwenye Katiba ya Muungano mambo
hayo ni kuvuruga. Huku akitoa angalizo kuhusu umiliki wa ardhi na
rasilimali zake, Warioba alisema kuwa hilo ni suala linalopaswa
kujadiliwa na kila upande wa muungano:
“Sisi tuliliona suala la ardhi na maliasili,
lakini kwa kuwa siyo suala la muungano tukaliacha. Wananchi walisema
Serikali haithamini ardhi yao, mtu anahamishwa kwa lengo zuri tu la
kujenga shule au barabara, lakini fidia anayopewa hailingani na thamani
ya ardhi yake. Wanahesabu miti tu, hatuwezi kumletea maisha mtu huyu,”
alisema na kuongeza:
“Wanasema kama Serikali inapendelea wawekezaji wa
nje na wa ndani. Hata hapa mjini matatizo yanatokea, watu wanahamishwa
mtu mwenye uwezo akishatokea. Kwa mfano, mahali kuna madini wanaondolewa
anapewa mwekezaji, mwananchi anaendelea kuwa masikini. Ilitakiwa kuwe
na utaratibu ambao mwananchi mwenye ardhi awe anapewa asilimia tano,
Serikali za Mitaa asilimia 10 na Serikali Kuu asilimia 25, wanataka
wafaidi. Ndiyo siri ya mambo ya Mtwara.”
Jaji Warioba ambaye amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa
Tume ya kuchunguza rushwa ya mwaka 1996, alisema kuwa anafarijika kuona
kuwa anaaminiwa na Serikali na matokeo ya kazi zake yanafanyiwa kazi
ndani na nje ya nchi.
Alimtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kukubali kukosolewa kama yeye anavyokubali kukosolewa katika kazi zake.
“Nilipoanza wakati ule mengi yalisemwa, lakini
nilijua, ukipewa kazi maalumu lazima upate mrejesho wa kila aina. Kuna
wale ambao watakusifu na wengine watakusema na nilisemwa mengi sana.
Lakini kwa kuwa nimefanya kazi ya Taifa siwezi kuhangaika na mtu mmoja
mmoja.
“Alivyosema Sitta nakubaliana naye, kazi ya
binadamu haikosi kasoro na sisi hatukuamini kwamba kazi yetu haikuwa na
kasoro. Ilikuwa nazo, kulikuwa na mambo labda tulipitiwa. Ningefikiri,
hayo anayosema angeyatumia na kwake, asifanye mambo kama hivi
anavyofanya… Asikilize wale wanaosema kuwa ana kasoro, asije akafikiri
kuwa hana kasoro.
Lakini mimi nashangaa sana mambo yanavyoendelea kwenye Bunge, hata siku hizi siangalii… ni kweli.
“Ni wakati fulani fulani mtu anaweza kunipigia
simu, hebu angalia wanavyosema. Bado nina matumaini, wananchi hawa
wametoa mawazo ya msingi, tukiyazingatia tutapata Katiba bora,
tusipoyazingatia tutapata Katiba itakayoanzisha mgogoro,” alisema Jaji
Warioba.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment