Wakazi wa Butiama mkoani Mara na vitongoji vyake, wakitazama mabasi
mawili yaliyogongana katika eneo la Sabasaba na kusababisha vifo vya
watu 36 na wengine zaidi ya 79 kujeruhiwa.
Watu 39 wamefariki dunia huku 79 wakijeruhiwa kwenye ajali
iliyohusisha magari matatu eneo la Sabasaba, Wilaya ya Butiama, mkoani
Mara.
Miongoni mwa waliofariki dunia yumo Mratibu wa ugonjwa wa Ukimwi wa Mkoa wa Mara, Dk Anatoria Ntangeki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philip Kallangi
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana na kwamba marehemu ni 36 na
majeruhi 79.
Wakati Kamanda Kallangi akitaja idadi hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Samson Winani alisema amepokea maiti 34 na majeruhi 79.
Dk Winani alisema Dk Ntangeki na mumewe aliyemtaja
kwa jina moja la Sayi walikuwa wakisafiri katika moja ya mabasi hayo.
Alisema hata hivyo haikufahamika alikuwa akielekea wapi.
Alisema baadhi ya majeruhi wana hali mbaya, lakini hakutoa idadi yao kwani walikuwa bado wanaendelea kuwahudumia.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula alisema waliofariki dunia ni 39.
Wanajeshi wasimamia
Zoezi la kutambua maiti lilibidi kusimamiwa na
askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kutokana na umati wa watu
waliokuwa wamefurika nje ya eneo la hospitali.
Wanajeshi walilazimika kwanza kupanga maiti halafu saa 12:00 jioni waliruhusu watu kuingia kwa ajili ya kutambua ndugu zao.
Miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo wamo Mwandishi
wa gazeti hili Mkoa wa Mara, Florence Focus ambaye amejeruhiwa paji la
uso na miguu, mwingine ni Mwandishi wa Raia Tanzania, Pendo Mwakyembe
ambaye amejeruhiwa kichwani na miguuni.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema ilitokea jana saa
tano asubuhi, Barabara ya Musoma-Tarime-Mwanza na kuhusisha mabasi
mawili na gari ndogo aina ya Toyota Land Cruiser.
Mkazi wa Kijiji cha Sabasaba, Magori Daniel alisema ajali hiyo
ilihusisha basi la Mwanza Coach linalofanya safari zake kati ya Musoma
na Mwanza na basi lingine maarufu J4 linalofanya safari zake kati ya
Sirari-Tarime na Mwanza.
Daniel alisema wakati basi la Mwanza Coach
lililokuwa likitokea Musoma kwenda Mwanza lilipofika eneo hilo lilitaka
kulipita gari dogo lakini mbele yake kulikuwa na basi la J4, hivyo
Mwanza Coach lilipoteza mwelekeo.
Alisema dereva wa Land Cruiser alijitahidi kubaki
upande wake, lakini gari lake liligongwa na basi la Mwanza Coach hivyo
dereva alipoteza mwelekeo na kuanguka kwenye daraja.
Daniel alisema wakati hali hiyo inatokea ghafla
mabasi hayo yaligongana uso kwa uso hali iliyosababisha watu wengi
kufariki dunia papohapo, huku wengine wakijeruhiwa vibaya.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Jerome Mugingi
alisema Land Cruiser lilikuwa na watu watatu akiwamo dereva, wawili
walifariki dunia palepale huku dereva akiokolewa na wasamaria wema na
kumpeleka hospitali kwa matibabu zaidi.
Mugingi alisema baada ya ajali waliwasiliana na
polisi na muda mfupi baadaye kikosi cha uokoaji wakiongozwa na Kamanda
Kallangi, madaktari na watu wengine waliwasili eneo la tukio na kuanza
kuokoa majeruhi ambao walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Mwandishi wa habari hizi aliwasili hospitalini
hapo na kushuhudia umati wa watu, hali iliyolazimisha wasimamizi wa
usalama kuzuia watu kuingia ndani ya eneo hilo. Ofisa usalama ambaye
hakutaka kutajwa, alisema hawawezi kuruhusu umati wa watu wote kuingia
ndani ya eneo la hospitali, lengo ni kutoa nafasi kwa madaktari
kuhudumia majeruhi.
“Kama unavyoona umati ni mkubwa, unafikiri
tukiwaruhusu kuingia ndani kuna kitakachofanyika kwa hawa majeruhi,
tumewazuia kwa lengo la kuwapa nafasi madakati na wauguzi kufanya kazi
zao,” alisema.
Pia, mwandishi wa habari hizi alishuhudia miili ya
watu 34 iliyofikishwa chumba cha maiti Hospitali ya Mkoa na magari ya
watu binafsi, polisi na basi moja linalomilikiwa na Kampuni ya Mwanza
Coach.
0 comments:
Post a Comment